Advertisements

Friday, September 22, 2017

WAZIRI ALAANI KITENDO CHA MWALIMU KUMPA MIMBA MWANAFUNZI WA DARASA LA SABA WILAYA YA KALAMBO MKOANI RUKWA

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy A. Mwalimu (Mb) amepokea kwa masikitiko makubwa kitendo cha mwalimu mmoja wa Shule ya Msingi Samanzi, iliyoko kijiji cha Samanzi, Kata ya Kisumba, wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa kumpa ujauzito mwanafunzi wa darasa la saba (jina limehifadhiwa), na kushindwa kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi. Mhe. Waziri amesema kitendo hicho ni ukatili na unyanyasaji dhidi ya mtoto wa kike na ni ukiukwaji wa Haki za Msingi za Mtoto ikiwemo haki ya Kuendelezwa na Kulindwa. Waziri Ummy amewaasa walimu kuacha tabia ya kuwa na mahusiano ya kingono na wanafunzi maana shule kama taasisi, ni chombo madhubuti cha kujenga uelewa kwa jamii kuhusu ulinzi na usalama wa Mtoto katika jamii. Aidha, amewataka walimu, walezi na jamii kuhakikisha wajibu wa kuwalinda na kuwalea watoto bila uwanyanyasaji na ukatili wa aina yoyote. Ameongeza kuwa, inapotokea mwalimu amehusishwa na tuhuma ya kumpa mimba mtoto wa kike kitendo hicho kinatia doa dhamana ya mwalimu na nafasi ya shule katika malezi ya mtoto.
Waziri Ummy, ameitaka jamii kuboresha ushirikiano wa wazazi, walezi na walimu maana wanamchango mkubwa katika makuzi na maendeleo ya watoto. Kadhalika, amesisitiza kutambua kuwa madhara ya mwalimu kumpa mimba mwanafunzi anamfanya kuwa mwathirika wa vitendo vya ukatili katika maisha yake yote. Aidha, Waziri Ummy ameelekeza vyombo vya dola mkoani Rukwa kuhakikisha suala hili linachunguzwa kikamilifu na kumfikisha mtuhumiwa mbele ya vyombo vya sheria ili haki iweze kutendeka.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

22/09/2017

No comments: