ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, October 7, 2017

4 WAUAWA UVAMIZI KWA MEJA JWTZ

Kamanda wa Kanda Maalum ya Kipolisi ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa
Kamanda wa Kanda Maalum ya Kipolisi ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limefanikiwa kuwaua majambazi wanne kati ya 20 waliodaiwa kuvamia nyumba ya Meja wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Makala Erasto (44) huko maeneo ya Toangoma Mbagala.

Kabla ya kuingia katika nyumba hiyo majambazi hao walitumia mlipuko kubomoa geti. Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Lazaro Mambosasa alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 6, mwaka huu majira ya saa saba.

Alisema askari wakiwa doria walipata taarifa kuwa kuna majambazi wapatao 20 wamevamia nyumba ya Meja huyo na kukimbilia eneo la tukio. Walipofika askari, majambazi walianza kuwafyatulia milipuko hali iliyosababisha askari kujibu mashambulizi.

Aliongeza kuwa askari walifanikiwa kuwadhibiti majambazi hao ambao walitawanyika huku wakiendelea kufyatua milipuko na katika mashambulizi hayo majambazi wanne walijeruhiwa kwa risasi sehemu mbalimbali za miili na kukimbizwa Hospitali ya Temeke ambapo walikufa wakipatiwa matibabu.

Mambosasa alisema katika eneo la tukio kumepatikana nyaya mbili za shaba, betri moja kwa ajili ya kutengeneza milipuko na mapanga matano. Hata hivyo alisema ofisa huyo wa jeshi na familia yake wapo salama. Aidha alisema juhudi za kuwatafuta majambazi waliokimbia zinaendelea.

Pikipiki zakamatwa Katika tukio jingine jeshi hilo limekamata pikipiki 10 na watuhumiwa 12 kwa unyanga’anyi wa kutumia silaha. Tukio hilo lilitokea Juni 23, mwaka huu saa moja usiku huko maeneo ya Buza baada ya mtoa taarifa Andrew John (20), mwanafunzi akiwa na pikipiki yenye namba za usajili MC 908 BQL aina ya Fekon rangi nyekundu yenye thamani ya Sh 2.2 kuvamiwa na majambazi wawili waliokuwa na pikipiki aina ya Boxer rangi nyeusi ambayo haikutambulika namba.

Alisema Majambazi hao walimpiga risasi kwenye mguu wa kushoto eneo la goti na kupora pikipiki. Baada ya tukio hilo ulifanyika msako mkali kwa maeneo mbalimbali ya Jiji na kupata taarifa huko maeneo ya Buguruni Malapa kuna watu wanaohusika na matukio hayo.

Askari walifika eneo la tukio na kufanikiwa kukamata watuhumiwa 12 waliokutwa wakibadilisha vipuli vya pikipiki kutoka kwenye pikipiki moja na kuzifunga kwenye pikipiki nyingine kwa lengo la kubadilisha mwonekano.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Hassan Bakari (28) mkazi wa Temeke, Daud Augusto (20) mkazi wa Buguruni Malapa, Tido Daudi (22) mkazi wa Buguruni Malapa na watuhumiwa wengine tisa.

Alisema pikipiki zilizokamatwa 10 ni zenye namba za usajili MC 178 BFZ Baja Honda rangi nyeupe, MC 190 AAE Boxer rangi nyeusi, MC 671 AZA Boxer rangi nyekundu na pikipiki nyingine saba. Watuhumiwa watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.

HABARI LEO

No comments: