Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imelaani vitendo vilivyofanywa na askari ambavyo havina maadili ya kazi.
Taarifa ya polisi ya jana Jumanne Oktoba 24, 2017 imesema jalada limeshafunguliwa na uchunguzi unaendelea ili kuwabaini waliohusika kuwapiga wananchi.
Imeelezwa askari hao walijichukulia sheria mikononi baada ya mwenzao Charles Yanga kukutwa ameuawa na mwili wake kuachwa pembezoni mwa uzio wa kambi ya Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) iliyoko Ukonga.
Kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema Jumapili Oktoba 22,2017 walipokea malalamiko ya watu wanaosadikiwa kuwa askari kufanya msako na kuwapiga wananchi wanaoishi jirani na kambi ya FFU ambao hawana hatia.
“Jeshi la Polisi linalaani vitendo hivyo ambavyo havina maadili ya kazi za polisi. Jalada limefunguliwa na uchunguzi unaendelea ili kuwabaini watuhumiwa wa tukio hilo. Tunaomba wananchi watoe ushirikiano kutoa taarifa za wahusika waweze kuwachukulia hatua watu au askari waliohusika na matukio hayo,” alisema.
Kamanda Mambosasa amesema Oktoba 21,2017 saa sita usiku maeneo ya kambi hiyo askari wakiwa kazini walikuta mwili wa askari huyo, huku pikipiki aliyokuwa akiendesha ikiwaka taa za tahadhari.
Amesema mwili wa askari huyo ulikuwa na majeraha kwenye paji la uso na sikio moja likiwa limekatwa.
Kamanda Mambosasa amesema walipofuatilia wamebaini askari huyo aliuawa na watu wasiojulikana na kutelekezwa katika maeneo ya kambi ya polisi.
Amesema kupitia kikosi kazi cha polisi wanaendelea na msako kuhusu tukio hilo la kikatili li kuwabaini watuhumiwa waliohusika.
No comments:
Post a Comment