Advertisements

Tuesday, October 10, 2017

Odinga ajiondoa, aiingiza Kenya katika mgogoro wa kikatiba

Mgombea urais kwa tiketi ya muungano wa upinzani cha National Super Alliance (Nasa) Raila Odinga amejiondoa katika uchaguzi wa marudio uliopangwa Oktoba 26 akitoa wito Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) kuitisha mpya.

Kiongozi huyo wa Nasa amesema uamuzi huo ni kwa maslahi ya Kenya na ni wa ushindani kwa kila upande.

Waziri Mkuu huyo wa zamani alisema kwa kujiondoa kwake nchi itapata fursa ya kushiriki uchaguzi mkuu mpya uliohuru na haki kwa mujibu wa sheria.

Lakini IEBC walipoulizwa kuhusu hatua ya kiongozi huyo wa upinzani walisema amechelewa kwani alitakiwa kuchukua hatua hiyo katika kipindi cha siku tatu tangu uchaguzi wa marudio ulipotangazwa kwenye Gazeti la Serikali.

Kujiondoa kwa Odinga kumekuja siku moja tangu Rais Uhuru Kenyatta kumtaka kiongozi huyo wa ODM kujiondoa kwenye mbio hizo kuruhusu nchi kusonga mbele.

Hata hivyo, Raila alisema mwaka 2013, Mahakama ya Juu ilipanua maana ya Ibara ya 138(8) (b) kuruhusu mgombea urais kujiondoa.

"Mahakama ya Juu ilifafanua kwamba Ibara muhimu ni ya 138 (8) (b) inayoshughulika na ufutwaji wa matokeo ya urais endapo kitatokea kifo kwa rais au makamu au kabla ya tarehe husika. Mahakama ya Juu ilipanua kifungu hicho kujumuisha wakati mgombea akijiondoa kwenye uchaguzi wa rais,” alisema Raila.

"Kwa tafsiri ya kifungu hicho ni kwamba kwa kujiondoa kwetu,ina maana kuwa uchaguzi uliopangwa Oktoba 26 utakuwa umefutika."

Raila alisema kwa kujiondoa kwake kunaitaka IEBC chini ya Mwenyekiti Wafula Chebukati kuanzisha upya mchakato wa kupokea majina ya wagombea kama ilivyoelekezwa kwa Sheria ya Uchaguzi ya 2011, Kifungu cha 13 (1).

Kifungu hicho kinasema: "Chama cha siasa kitateua wagombea wake kwa ajili ya uchaguzi chini ya sheria hii walau siku tisa kabla ya uchaguzi mkuu kwa kuzingatia katiba na kanuni."

Tangazo la kujitoa


Katika uamuzi uliotangazwa jana mchana Odinga alisema pia mgombea mwenza wake Kalonzo Musyoka hatashiriki uchaguzi huo.

“Baada ya kufikiria sana juu ya nafasi yetu kuhusiana na uchaguzi wa marudio na kwa kuangalia maslahi mapana ya watu wa Kenya, ukanda na ulimwengu kwa ujumla, tunaamini kwamba ni bora Nasa tujiondoe kugombea uchaguzi uliopangwa kufanyika Oktoba 26, 2017,” amesema Odinga.

Odinga amesema Nasa imekuwa ikitoa wito uchaguzi uwe huru na wa haki kwa kuzingatia matakwa ya Katiba lakini hakuna mwitiko mwema.

“Tumefikia hitimisho kwamba hakuna nia njema kutoka (Tume ya Taifa ya Uchaguzi) IEBC kuhakikisha kwamba dosari na ukiukwaji wa sheria ulioshuhudiwa kabla hautajitokeza tena,” amesema.

Ameishutumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa “kupiga teke” maamuzi ya kuwa na uchaguzi wa marudio wa kuaminika. “Tumefikia uamuzi wa mwisho kwamba hakuna nia njema kwa upande wa IEBC kufanya mabadiliko yoyote katika shughuli zao na watumishi kuhakikisha kwamba ‘dosari na kasoro’ zilizosababisha uchaguzi wa Agosti 8, 2017kubatilishwa hazitajirudia tena,” amesema.

Odinga aliongeza; “Dalili zote zinaonyesha kwamba uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Oktoba 26 utakuwa mbaya zaidi kuliko ule wa awali.”

Alimgeukia Rais Uhuru Kenyatta na chama chake cha Jubilee kwa kushinikiza mabadiliko ya sheria za uchaguzi akisema hatua hiyo inaonyesha kwamba hakuna nia njema ya ushindani katika uwanja uliosawa.

“Uchaguzi pekee ambao utawala wa Jubilee inapendelea ni ule ambao wao lazima washinde hata kama ni kwa kukiuka sheria,” amesema.

Amewashutumu Rais Kenyatta na makamu wake William Ruto kwa kujigamba kwamba wana wingi wa watu katika Bunge la Taifa na Seneti akisema viongozi wawili hao “wanakusudia kupindua utaratibu huu mpya na kuurejesha wa zamani.”

Mjadala bungeni


Nasa wametoa uamuzi huo wakati Bunge lenye wabunge wengi wa Jubilee linahaha kukamilisha mchakato wa kujadili miswada miwili tata na kuipitisha kabla ya siku ya mwisho ya kufanya hivyo kesho Alhamisi.

Mabunge yote mawili yaani Bunge la Taifa na Seneti yanajadili ripoti ya miswada miwili inayolenga Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, na Sheria ya Uchaguzi na Makosa ya Uchaguzi kuelekea uchaguzi wa marudio.

Hata hivyo wabunge wa Nasa wamekataa kushiriki mjadala wa mabadiliko tata ya sheria ya uchaguzi yaliyowasilishwa katika vikao vya Bunge la Taifa na Baraza la Seneti. Wabunge hao walisisitiza pia kwamba kiongozi wao Odinga hatashiriki uchaguzi huo.

Uamuzi wa kutoshiriki mjadala huo ulifikiwa Jumatano iliyopita katika vikao vya wabunge wa Nasa.

Kamati zote mbili za Bunge la Taifa na Seneti chini ya uenyekiti wa Mbunge wa Baringo Kaskazini William Cheptumo na Fatuma Dullo mtawalia walifanya kikao cha pamoja wiki iliyopita kuchukua maoni ya wananchi kuhusu sheria hizo.

Kiongozi wa wachache bungeni katika Bunge la Taifa, Mbunge wa Suba Kusini John Mbadi alisema hatua yao ya kutoshiriki mjadala huo imelenga kukwepa kuhalalisha “mchakato uliokosewa.”

“Baada ya kupitia miswada yote miwili, tumejiridhisha kwamba ni miswada hatari. Miswada hii haiku kikatiba na iko katika msingi uliokosewa kwa maudhui yake na mchakato mzima,” alisema Mbadi.

Akipinga miswada miwili kujadiliwa kwa pamoja na mabunge mawili, Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Jnr alisema, “Hatutashiriki katika uchaguzi ambao Jubilee wanatoka jasho kubadili magoli. Tunataka kuwaambia Jubilee hatutaruhusu hilo kutokea.”

MWANANCHI

No comments: