ANGALIA LIVE NEWS

Monday, October 30, 2017

SERIKALI YATAIFISHA KUNDI LINGINE LA NG’OMBEKUTOKA RWANDA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina (kulia) akiongea na team ya Wilaya ya Kasulu iliyoshiriki katika zoezi la kukamata ng’ombe aina ya nyankole kutoka Rwanda,  waliovamia katika kijiji cha Kakere, kushoto kwake ni kaimu Mkuu wa Wilaya hiyo Bi. Mwanahawa Mrindoko.
Ng’ombe aina ya nyankole kutoka Rwanda, waliotaifishwa na serikali katika kijiji cha Kakere wilayani Kasulu wakisubiri kukamilika kwa taratibu za mahakama kwa ajili ya kupigwa mnada.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina, akiangalia Ng’ombe aina ya nyankole waliopo katika kijiji cha Kakere baada ya kutaifishwa na serikali.
Waziri Mpina akiongea na wanahabari hawapo katika picha baada ya zoezi la kutaifisha kundi la ng’ombe waliovamia katika kijiji cha Kakere wilayani Kasulu.

Kufuatia zoezi linaloendelea la oparesheni kamata mifugo linaloongozwa na Waziri mwenye dhamana ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina, serikali kwa mara nyingine imetaifisha kiasi cha ng’ombe 171 waliokamatwa katika kijiji cha Kakere wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
Akiongea katika zoezi hilo Waziri Mpina amesema Wilaya za mipakani mwa Nchi jirani ziko katika tishio kubwa la kuvamiwa na mifugo na kuelekeza mwanasheria wa Wilaya ya Kasulu kuanza kuandaa utaratibu wa mahakama kuzipiga mnada. “Hatua ya kwanza sisi kama Serikali tunataifisha ng’ombe hawa na kufanya utaratibu wa kuzipiga mnada na mwanasheria wetu wa Serikali aanze taratibu ambapo ng’ombe hao tutawapiga mnada kwa mujibu wa sheria ya magonjwa ya wanyama No. 17 ya mwaka 2003.” alisema Mpina.
Mpina aliongeza kusema kuwa, ng’ombe hao kwa sasa wataendelea kuwa chini ya Serikali mpaka taratibu zitakapo kamilika, na kuitaka  kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kasulu  kuelendelea kwa kasi kubwa kukamata mifugo katika mapori na kuhakikisha mifugo yote inapatikana.
Sambamba na hilo, Waziri Mpina aliwataka wananchi kujiadhari  na kuondoka katika kununua kesi zisizokuwa za kwao kwa kuikubali mifugo kutoka nje ya nchi kuwa ni ya kwao, kwani ni kujitaftia matatizo na kuisadia serikali katika jitahada hizi za kukamata mifugo inayoingia ndani ya nchi kinyume na taratibu.
 “Kwa hiyo wananchi wawe namba moja kuwafichua watu hao, na wale tunaowabaini  kuwa wanaitikia mifugo toka nje ya nchi kuwa ni mali yao lazima wachukuliwe hatua.” alisisitiza Mpina.
Awali akitoa taarifa ya ng’ombe hao waliokamatwa katika Wilaya hiyo mkuu wa wilaya hiyo Mwanahawa Mrindoko alisema ng’ombe hao ni mali ya  raia wa Rwanda kwani Serikali ya wilaya ilikuwa inawatafuta Raia  wahamiaji haramu  na kuwapata, hivyo sheria itachukua mkondo wake, na aliongeza kwa kusema kuwa kamati ya ulinzi na usalama itaendelea na zoezi la kuwatafuta wafugaji ambao ni wahamiaji haramu.
Akiwa katika wilaya ya Kakonko Waziri Mpina aliagiza kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo  kupitia Mkuu wa Wilaya Kanali Hosea Ndagalla kuanza mara moja zoezi la oparesheni ya kukamata mifugo toka nje ya nchi kwani tarifa za awali zinasema kuwa Wilaya hiyo ilikuwa haijaanza kabisa kutekeleza agizo hilo na ni moja ya Wilaya ya mpakani mwa nchi jirani ya Burundi.

No comments: