Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (wa tatu kushoto), akitoa maelekezo kwa Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), Mkoa wa Rukwa, Mussa Mchola (wa pili kulia), wakati alipokagua Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga, Mkoani Rukwa.
Muonekano wa barabara ya kuruka na kutua ndege katika Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga, Mkoani Rukwa. Upanuzi wa Uwanja huo unatarajiwa kuanza mapema mwezi Ujao.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (wa nne kushoto), akimsikiliza Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), Mkoa wa Rukwa, Mussa Mchola alipokuwa akimwonyesha mipaka ya uwanja huo Mkoani humo.
Muonekano wa Barabara ya Sumbawanga-Matai-Kasanga KM 112, mkoani Rukwa, ambayo ujenzi wake unatarajiwa kukamilika mwakani.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akichanganya zege katika Mizani ya Singiwe katika Barabara ya Sumbawanga-Matai-Kasanga KM 112, Mkoani Rukwa wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo.
Muonekano wa eneo korofi katika sehemu ya Barabara ya Matai-Kasanga, mkoani Rukwa, ambayo ujenzi wake unatarajiwa kukamilika mwakani.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kulia), akikagua eneo korofi katika sehemu ya Matai-Kasanga, Mkoani Rukwa wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema ujenzi wa uwanja wa ndege wa Sumbawanga utaanza kujengwa kwa kiwango cha lami kuanzia mwishoni mwa mwaka huu baada ya taratibu za kumpata mkandarasi kukamilika.
Akizungumza na wananchi wanaozunguka Uwanja huo Prof. Mbarawa amewahakikishia wananchi wote wanaostahili kulipwa fidia kutokana na kupisha ujenzi huo watalipwa fidia zao katika kipindi kisichozidi miezi miwili kuanzia sasa.
“Jumla ya wananchi 97, ndio wanaostahili kulipwa fidia na kiasi cha shilingi bilioni 3.3 kimetengwa na wataanza kulipwa hivi karibuni kabla ya zoezi la ujenzi wa uwanja huo kuanza” amesema Prof. Mbarawa.
Amewataka wananchi hao kuacha kupita katika uwanja huo kwani ni hatari kwa usalama wa ndege na usalama wa wananchi wenyewe.
Ujenzi wa uwanja wa ndege wa Sumbawanga unajengwa kwa kiwango cha lami na kuongezwa urefu kutoka kilomita 1.5 had 1.7 ili kuwezesha ndege kubwa zaidi kutumia uwanja huo na hivyo kuufungua mkoa wa Rukwa na mikoa mingine hali itakayochochea maendeleo na ukuaji wa uchumi kwa mkoa huo.
Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), Mkoa wa Rukwa, Mussa Mchola amemshukuru Waziri Prof. Mbarawa kwa hatua ya kulipa fidia na kumhakikishia kuwa watamsimamia mkandarasi huyo kikamilifu ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati na kwa ubora unaostahili.
Katika hatua nyingine Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof Mbarawa amekagua Ujenzi wa Barabara ya Sumbawanga-Matai-Kasanga Port KM 112 na mizani ya Singiwe na kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa miradi hiyo ambapo amemtaka mkandarasi China Railway 15, Bereau Group Corporation (CR15G) na Henan Provincial Newcentry Road na Bridge Consultants Limited JV anaejenga kuongeza kasi katika maeneo korofi kabla ya Mvua za masika kuanza.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Mwl. Julieth Binyura amezungumzia umuhimu wa ukamilishaji wa barabara hiyo utakavyonufaisha wilaya hiyo kwa kuwa inaunganisha Wilaya hiyo na bandari ya Kasanga na mpaka wa Kasesha unaounganisha Tanzania na Zambia na hivyo kuchochea uzalishaji na uchukuzi kati ya Tanzania, Kongo na Zambia.
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano iko katika mchakato wa kuunganisha kwa kiwango cha lami barabara zinazoingia katika bandari za mipakani ili kukuza huduma za uchukuzi kati ya Tanzania na nchi jirani kwa njia za magari, ndege na meli.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment