Novemba 22, mwaka 2016, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, aliweka picha yake mtandaoni ikimwonyesha akiwa ndani ya Ikulu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwa miongoni mwa wageni walioalikwa kwenye tafrija ya rais mpya wa nchi yetu, John Magufuli.
Katika picha waliyopigwa inaonyesha dhahiri kuwa, kazi ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete ilikuwa kumtambulisha Zitto Kabwe kwa Rais Magufuli. Ni heshima.
Mara kadhaa Zitto amesema picha hiyo inaonyesha ‘Rais wa 6” akiwa na marais wa awamu ya nne (Kikwete) na tano (Magufuli). Ni ndoto ya kila mwanasiasa kuwa kiongozi mkuu wa nchi. Lakini kuna sura tofauti kati ya Zitto Kabwe wa serikali ya awamu ya nne na awamu ya tano ya John Magufuli.
Katika utawala wa Kikwete, Zitto amepitia katika matukio mbalimbali ya kusisimua na kushangaza, huku mengine yakitawaliwa na utata machoni pa wanasiasa wenzake. Hata hivyo, hizo si hoja za msingi kwa leo. Swali kubwa la leo ni kwanini baadhi ya wanasiasa wa chama chake cha ACT-Wazalendo wanamkimbia Zitto?
Mwaka 2012 Zitto aliungana na wabunge kupaza sauti kutaka mawaziri nane wang’oke kutokana na ufisadi. Zitto alikusanya saini za wabunge, kutimiza 70, ili awasilishe hoja ya kumng’oa aliyekuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda. Baadaye Rais Kikwete aliwang’oa mawaziri waliokuwa wanatakiwa kuwajibishwa, hivyo akafanikiwa kumwokoa Pinda.
Mwaka huo huo, Kamati ya POAC ilivunjwa na Spika wa Bunge la 10, Anne Makinda, ambapo aliunganisha na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto akashinda uenyekiti wake.
Aidha, ni Zitto Kabwe ambaye alihakikisha anapigania masilahi ya Watanzania baada ya kukubali kutimuliwa bungeni kutokana na tuhuma zake dhidi ya aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, ambaye alidaiwa kusaini mkataba wa Buzwagi akiwa hotelini huko jijini London, nchini Uingereza. Kutokana na tuhuma hizo, aliyekuwa Spika wa Bunge 2005-2010, Samuel Sitta, alimfukuza bungeni.
Zitto pia amechangia pakubwa kupatikana kwa sheria ya Capital Gain kwenye sekta ya madini nchini.
Mapito ya Zitto
Zitto ni mwanasiasa aliyeibuliwa na Chadema chini ya uenyekiti wa Freeman Mbowe.
Ndicho kipindi ambacho Zitto aliibuka kuwa mwanasiasa mahiri na aliyetikisa kwa matukio mbalimbali. Tuhuma za usaliti wa Zitto dhidi ya Chadema zilijiri zaidi wakati akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali, ambapo alimwagiza Msajili wa Vyama vya Siasa kufanya ukaguzi wa hesabu zao za fedha.
Zitto aliagiza hilo akiwa Naibu Katibu Mkuu Chadema, hali ambayo ililalamikiwa kuwa anakisaliti chama, kwani alitakiwa “kuwatonya” juu ya mpango huo wa ukaguzi. Wapo walioudhika juu ya mpango huo na kudai Zitto ni msaliti.
Pili, mwaka 2009 Zitto alitangaza bayana kumuunga mkono mgombea wa NCCR- Mageuzi katika Jimbo la Kigoma Kusini, David Kafulila, licha ya chama chake hicho cha zamani, Chadema kuweka mgombea wao.
Tatu, uamuzi wa Zitto Kabwe kugombea uenyekiti mwaka 2009 dhidi ya Freeman Mbowe lilikuwa jaribio ambalo Chadema kilitakiwa kukabiliana nalo na kulitatua. Zitto akiwa na kambi yake ya kisiasa ndani ya Chadema, alichukua fomu na kugombea uenyekiti, hali ambayo iliibua malumbano makali, na kuitwa msaliti.
Kambi ya Zitto Kabwe ilikuwa pamoja na Samson Mwigamba na Profesa Kitila Mkumbo. Kwa muda mrefu Zitto alituhumiwa kutoshiriki majukumu mbalimbali ya kichama, hali ambayo ilitokana na jaribio lake la kugombea uenyekiti.
Inaelezwa kuwa, Zitto hakuwa karibu tena na Chadema, ingawa mwaka 2010 aliruhusiwa kugombea ubunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya chama hicho. Kuutaka uenyekiti kulitajwa kama usaliti ndani ya Chadema.
Nne, M4C ni moja ya operesheni inayotumiwa na Chadema ambayo Watanzania wanahamasishwa kujiunga katika chama ili kuleta mabadiliko. Zitto alidaiwa kutoshiriki kikamilifu katika operesheni hiyo.
Mwishowe Zitto na Chadema wakapelekana mahakamani, licha ya katiba ya chama kukataza wanachama wake kutokwenda mahakamani kwa suala la chama. Ndiyo kusema Zitto alikuwa amekiuka katiba ya Chadema, ndipo mwaka 2015 akafukuzwa uanachama na baadaye akajiunga na chama cha ACT-Wazalendo.
Ndani ya Chadema, Zitto Kabwe anatafsiriwa kama msaliti ambaye alikuwa anakihujumu chama. Kwa Chadema, Zitto, Profesa Kitila Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, walitajwa kuwa wasaliti na walikihujumu chama hicho. Mtazamo wa Chadema ulijengwa zaidi na matukio yote ambayo yalisababisha malumbano ndani ya chama, hata kama yalikuwa ya kidemokrasia. Hujuma yao kubwa ilitajwa kuandaa mkakati wa ushindi ambao ungemwondoa Mbowe madarakani kupitia sanduku la kura.
Ndani ya chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alikuwa na washirika wake wa karibu, Profesa Kitila Mkumbo, Samson Mwigamba na wakili maarufu Alberto Msando. Zitto alijiunga ACT- Machi 20, 2015 na kukabidhiwa kadi na Mwenyekti wa Tawi la Tegeta.
Cha kustaajabisha ni kwamba, Zitto amekimbiwa na washirika wake ndani ya chama kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo kutoeleweka kwa miongozo ya Kiongozi Mkuu wa Chama (Party Leader).
Profesa Kitila Mkumbo aliteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji. Kitila alikuwa mshauri wa ACT-Wazalendo na mshirika wa karibu wa Zitto kwa muda mrefu. Kitila na Zitto walifukuzwa pamoja ndani ya Chadema sambamba na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.
Aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Anna Mghwira, ameteuliwa na Rais Magufuli kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro. Mara baada ya uteuzi huo, chama cha ACT-Wazalendo kilitangaza kumwengua katika nafasi yake ya uenyekiti.
Sasa hali imekuwa mbaya zaidi, kwani Samson Mwigamba ambaye alikuwa Kiongozi wa Kamati ya Uchaguzi ya chama hicho, naye amemkimbia Zitto Kabwe na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi – CCM.
Mwigamba amekimbilia CCM ambako aliwahi kukibeza na kuishambulia kwa lugha kali ambazo baadhi zilimfikisha mahakamani kwa madai ya kuwachochea askari kuasi. Awali Mwigamba alijiuzulu wadhifa wake wa Katibu Mkuu kwa sababu alikuwa akielekea masomoni na kufanya kazi mjini Arusha katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.
Sasa Mwigamba amekikimbia ACT-Wazalendo na kwenda CCM, huku akiacha shutuma mbalimbali dhidi ya viongozi wenzake.
Uamuzi wa Mwigamba ulitokea siku chache baada ya Profesa Kitila Mkumbo kujivua uanachama wa ACT-Wazalendo, kwa madai anashindwa kuaminiwa na kutekeleza vizuri majukumu yake ndani ya wizara kwa kudhaniwa kuwa mpinzani.
“Mnamo Aprili 25, 2016, nilipokuwa nang’atuka ukatibu mkuu, nilipotoa nasaha zangu mbele ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama nilisema, salama ya chama chetu ni kubaki kwenye misingi ya uanzishwaji wake.
“Hii haikuwa bahati mbaya, bali nilimaanisha kwa kuwa nilishaanza kuona mwelekeo wa baadhi ya viongozi kuchepuka nje ya misingi ya chama. Na kutokea hapo nimekuwa nikiwalalamikia sana viongozi juu ya kuacha misingi na mambo ya msingi yaliyotufanya tuanzishe chama hiki, mara nyingine nikifikia kutofautiana sana hata na wewe binafsi (Kiongozi Mkuu wa Chama).
“Kwa kuwa hali hiyo kwa sasa inazidi kuongezeka na jambo ambalo binafsi naamini ndiyo sababu hasa ya Prof Kitila Mkumbo kujivua uanachama,” ilisema barua ya Mwigamba kwenda kwa Kiongozi Mkuu wa Chama, Zitto Kabwe.
Swali la kujiuliza hapa je; Zitto Kabwe amesalitiwa na washirika wake au yeye amewasaliti? Kwa sababu washirika wake wamekuwa wakilalamika, huku yeye akiwa ndiye kiongozi mwenye sauti ya mwisho ndani ya chama.
Hii inaleta mantiki juu ya malalamiko ya Chadema kuwa mwanasiasa huyo alikuwa akikihujumu chama, na sasa anakiongoza chama ambacho yeye ndiye taswira kuu, huku wengine wakikosa umuhimu. Udhaifu huu umechochea ACT-Wazalendo kuonekana kama chama cha mtu mmoja na kufifisha umahiri wa wengine.
1 comment:
Wakati wa Nyota ya Zitto Umetimia
Post a Comment