Mugabe mwenye umri wa miaka 93, anatakiwa kujiuzulu ifikapo saa 6 mchana leo Novemba 20, 2017, vinginevyo bunge la nchi hiuyo ambalo lina wafuasi wengi kutoka chama chake cha ZANU-PF litapiga kura ya kutokuwa na imani nae na hivyo kumuondoa madarakani.
Emmerson Mnangagwa, ambaye alitimuliwa na Mugabe hivi karibuni kwenye nafasi ya umakamu wa Rais, ametangazwa kuwa kiongozi wa ZANU-PF baada ya wanachama wa chama hicho kumng’oa madarakani Mugabe ambaye ndiye alikuwa Mwenyekiti wa taifa wa ZANU-PF.
Katika hotuba yake ya maandishi aliyoisoma kwa dakika 20 kwenye televisheni ya taifa, hakuna mahala alipotaja, msukosuko wa sasa kutoka kwenye chama chake au raia wa nchi hiyo ambao majuzi walijitokeza barabarani na kuhanikiza jiji la Harare huku wakimtaka Mugabe aondoke madarakani.
Badala yake Mugabe alisema jeshi la nchi hiyo halijafanya makosa kutwaa madaraka na kumuweka kwenye kizuizi cha nyumbani.
“Kwa vyovyote vile ambavyo jeshi lilitekeleza operesheni zake, mimi kama Amirijeshi Mkuu, ninatambua kuguswa kwao” Alisema Mugabe akirejea jinsi jeshi la nchi hiyo lilivyozingira Shirika la Utangazaji la Taifa jijini Harare.
Mugabe pia alisema, “Mkutano Mkuu wa ZANU-PF unatarajiwa kufanyika wiki chache zijazo na mimi nitauongoza mkutano huo hatua kwa hatua”. Alisema
Kabla ya hotuba hiyo ya Mugabe, Zanu-PF tayari ilimtangaza Mnangagwa kuwa kiongozi mpya wa chama hicho na pia mgombea wake wa kiti cha urais kwenye uchaguzi mkuu ujao huku mke wa Mugabe, Grace, akitimuliwa chamani.
No comments:
Post a Comment