
Wanaotaka kuwa waandishi wa habari hufunzwa kuwa msingi mkuu wa kazi yao ni ukweli. Wale ambao tayari ni waandishi hukumbushwa msingi huo mara kwa mara.
Falsafa ya mawasiliano basi imejengwa kwenye ukweli. Kuandika, kama kutangaza, ni kuwasilisha taarifa kwa shabaha ya kujulisha au kufahamisha. Shabaha ya kufahamisha ni kuweka uelewa. Ni shabaha hiyo inayofanya kila mpasha taarifa au habari kuzingatia ukweli.
Kila anayefanya mawasiliano ana nia na shabaha ya kuwasilisha ukweli; basi kila anayepokea mawasiliano anatarajia kupewa, na yeye kusambaza ukweli.
Kwahiyo, kwakuwa taarifa siyo mali ya mtu mmoja; na kwa kuwa tayari imetolewa; na aliyeipokea anajisikia kumegea wengine taarifa hiyohiyo; basi hata wale watakaomegewa au wenye shauku ya kupata taarifa hiyo, watakuwa au wanatarajia iwe ya kweli na iliyosheheni ukweli.
Kama yupo anayesubiri kisicho cha ukweli; basi hakuna haja ya kusubiri. Afadhali akae chini na kubuni “vitu vyake” kwa shabaha ya kujipasha taarifa na kujiridhisha kuwa anawasiliana.
Na hilo lingekuwepo, basi kila mmoja angebuni “vitu vyake” na kujipasha taarifa na kujiaminisha kile alichoumba na ambacho anajua siyo kweli au hakina ukweli isipokuwa kujiliwaza. Huo ungekuwa wendawazimu.
Lakini huduma na biashara ya kutoa na kusambaza taarifa na habari, duniani kote na miongoni mwa watu wenye akili timamu, imejengwa kwenye msingi wa ukweli. Kila anayesubiri taarifa au habari, anasubiri ukweli juu ya kile anachotarajia.
Ukweli huu unahitaji kuonekana kwa njia ya kuwasilishwa kwa usahihi. Kwahiyo, kuna njia ya kweli ya kuandika au kutangaza au kuwasilisha ukweli. Njia hiyo ni: usahihi.
Huduma na biashara ya kusambaza taarifa na habari inazingatia uhalisi, uhakika wa taarifa zinazothibitika juu ya vitu, hali, mazingira na fikra zilizopo. Ukienda nje ya mstari huu unakemewa na wanataaluma au weledi wanaoaminika.
Hii ndio maana vyombo vya mawasiliano huomba radhi pale vinapothibitisha kutokuwepo usahihi katika uwasilishaji; hata kama ukweli uko palepale.
Waweza kusema hiyo ni nadharia juu ya upashanaji taarifa au habari. Kuna vyombo vya habari vya aina hiyo; lakini pia kuna watu binafsi wanaozingatia mambo hayo katika maisha yao ya kawaida: ukweli na ukweli unaowasilishwa kwa usahihi.
Ukweli wenyewe hauna tatizo; bali kuna wanaoweza kuutumia kwa shabaha tofauti. Wakati ukweli unaweza kutumika kumimina usahihi miongoni mwa jamii na kuleta furaha, faraja na matumaini kwa wengi; kuna wanaoweza kuutumia kuziba furaha, kufinyaza faraja na kuondoa matumaini.
Hili ndilo linawapa shida viongozi wa Mwananchi Communications Limited (MCL), wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti.
Wanaona magazeti yao yanafanya kile wanachoita “kazi nzuri kitaaluma.” Yanachunguza, yanaripoti, yanaibua, yanachambua – habari za kawaida, michezo na burudani. Lakini inatokea mwandishi wao “anachukuliwa” kutoka ofisini kwake Kibiti, mkoani Pwani na kupotezwa kwa siku 25 sasa.
Hii ndiyo maana MCL imeomba serikali, wadau wa habari, mashirika na asasi za kijamii na jamii kwa jumla, kuongeza juhudi katika kumtafuta na kumpata mwandishi wake Azory Gwanda; tena akiwa hai.
Kutoweshwa kwa Gwanda kunaleta wasiwasi mkubwa miongoni mwa waandishi wa habari. Kwenye mkutano wa MCL na waandishi wa habari wiki iliyopita, ambako kampuni ilitoa kilio, waandishi watatu nilioongea nao walinieleza kuwa wanaanza “kuogopa kuandika habari.”
Hapa ndipo panahitajika hatua za haraka kumpata Azory Gwanda; na ombi la MCL kwa serikali, asasi na jamii kuongeza juhudi za kumtafuta mwandishi huyu, zinasimama kwenye msingi wa kuendeleza utamaduni na misingi ya ukweli.
Waandishi wakiogopa kuandika habari za kweli, ukweli na kwa usahihi; maadui wa ukweli – wa ndani na nje ya nchi – watashangilia na kutamba kwamba hawashikiki. Huko basi ndiko kuingia au kuishi gizani moja kwa moja; katika umbeya au uongo.
Meza ya Mhariri wa Jamii haijapokea malalamiko kutoka kwa yeyote juu ya mwandishi huyo kuandika uongo, uzushi, uchochezi wala fitina. Hii ndio maana MCL imesema kama anadaiwa kutenda kosa afikishwe mahakamani.
Bila shaka waliomteka mwandishi wanajua umuhimu wa ukweli; lakini sasa hawatapata ukweli mwingine iwapo waandishi wataogopa kuandika; na iwapo mateka hatapata fursa ya kuandika tena. Kilio cha kumtafuta Gwanda ni muhimu kwa wote wanaojua thamani ya mwandishi na ukweli.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment