Advertisements

Saturday, December 16, 2017

TEWW Kuendelea kuwa Kitovu cha Elimu ya Watu Wazima

 Naibu Waziri Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Tate Ole Nasha akizungumza na Wahitimu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (hawapo pichani)  wakati wa mahafali ya 53 ya Taasisi hiyo yaliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam ambapo alikuwa mgeni rasmi.
 Mkurugenzi  Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW)  Dkt. Fidelice Mafumiko akizungumzia  mikakati ya Taasisi hiyo katika kukuza kiwango cha elimu nchini wakati wa mahafali ya 53 ya Taasisi hiyo yaliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
 Naibu Waziri Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Tate Ole Nasha akimtunuku cheti cha uongozi bora kiongozi wa Serikali ya Wanafunzi TEWW, Thomas Amos wakati wa mahafali hayo yaliyofanyika katika Viwanja vya Taasisi hiyo  Jijini Dar es Salaaam.
 Baadhi ya Wahitimu wakiwa kwenye picha ya pamoja wakati wa mahafali hayo.
 Naibu Waziri Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Tate Ole Nasha (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Sehemu ya wahitimu hao mara baada ya mahafali yaliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam.(Picha na TEWW)

Na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW).
Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) imetakiwa kuendelea kuwaandaa wataalamu katika fani za Elimu ya Watu Wazima na Maendeleo ya Jamii wenye ubunifu wa kutatua changamoto za ufundishaji na ujifunzaji wa Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa vijana na watu wazima.

Akizungumza wakati wa mahafali ya 53 ya Taasisi hiyo jijini Dar es Salaam leo, Naibu Waziri Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Tate Ole Nasha amesema ili kudhibiti ubora wa elimu inayotolewa kuna umuhimu wa kuwa na Sheria ya Elimu ya Watu Wazima itakayotoa mamlaka kwa Taasisi kuweza kusajili na kuthibiti ubora wa Vituo vya Elimu nje ya mfumo rasmi.

Akieleza mikakati ya Serikali kuboresha elimu hapa nchini  Mhe. Ole Nasha  amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano mara tu baada ya kuingia madarakani ilianza utekelezaji wa Mpango wa  Elimu bila malipo ambapo kiasi cha shilingi bilioni 23 hutumika kila mwezi katika mpango huo.

Aidha mhe. Ole Nasha alitoa wito  kwa wazazi  kuendelea kuwaandikisha shule watoto wote waliofikisha umri wa kujiunga na shule ili waendane na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano inayosisitiza uwajibikaji katika kuchochea maendeleo ya Taifa.

Akizungumzia swala la kukuza elimu nchini Ole nasha amesema kuwa kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, idadi ya Watanzania wasiojua Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) ni asilimia 22 ambapo asilimia hii bado ni kubwa na ni changamoto katika kufikia azma ya kuwa na Watanzania walioelimika na wanaoweza kuchangia kwa haraka katika maendeleo ya Taifa letu kama inavyobainishwa katika Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014. 

“Naipongeza Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kwa kazi nzuri katika kuwaandaa wataalamu na Uwajibikaji wenu ndio umewezesha kuwapata wahitimu hawa 962 ambao naamini wameandaliwa vizuri na wameiva katika taaluma zao, hivyo watashiriki kikamilifu katika kutekeleza majukumu yao kwa weledi” Alisisitiza Mhe.  Ole Nasha

Akifafanua Mhe. Ole Nasha amesema kuwa wahitimu hao hawana budi kutekeleza  kwa vitendo kauli mbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano  Mhe. Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli ya HAPA KAZI TU kwa vitendo.

Mahafali ya 53 ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima yameshirikisha wahitimu wa Astashahada, Stashahada na Shahada na yamefanyika katika Viwanja vya Taasisi hiyo ambapo Dhamira ya Serikali Awamu ya Tano ya kuleta mapinduzi ya kiuchumi na kuibadili Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati inayotegemea viwanda ifikapo 2025.

No comments: