ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, December 24, 2017

WARATIBU ELIMU KATA WASHUSHWA VYEO KUTOKANA NA ULEVI

Waratibu wawili wa elimu kata za Njoge na Lenjulu wilayani Kongwa mkoani Dodoma wameshushwa vyeo kwa ulevi na kutowajibika kwa maendeleo ya shule.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deogratias Ndejembi alitoa agizo hilo jana Jumamosi Desemba 23,2017 alipozungumza na waratibu elimu wa kata 22.
Amewataja waratibu hao kuwa ni Emmanuel Chiluluse wa Kata ya Lenjulu na Venance Mwangasa wa Njoge.
"Hawatambui majukumu yao hivyo naagiza ofisa elimu msingi na sekondari muwatafutie kazi nyingine za kufanya na mtafute watu wengine wa kuziba nafasi zao," ameagiza Ndejembi.
Amesema, "Waratibu wa namna hii hawafai katika wilaya yangu kwa kuwa wanachochea kushuka kwa kiwango cha elimu na kukiuka ilani ya CCM. Waratibu wengine wa kata acheni kufanya kazi kwa mazoea. Badilikeni ili muendane na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano."
Akizungumza katika kikao hicho, Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Kongwa, Nelson Milanzi amesema wanafunzi 3,863 wamepangwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za sekondari 26 wilayani humo.
Amesema wakuu wa shule wameshapatiwa majina ya wanafunzi hao.
Mwenyekiti wa kamati ya huduma za jamii na diwani wa Sejeli, Chilingo Chimeledya amesema kuna upungufu wa madarasa 20 katika shule zote za sekondari, hivyo amewataka viongozi wa kata kushirikiana na wananchi kutatua changamoto hiyo.

Chanzo: Mwananchi

No comments: