Kauli hiyo ilitolewa na Mbunge wa Jimbo la Lushoto (CCM) Shabani Shekilindi alimaarufu Bosnia wakati wa ziara yake wa kuwatembelea wananchi katika vijiji mbalimbali iliyokuwa na lengo la kuhamasisha kujikita kwenye shughuli za uzalishaji na kusikiliza kero zinazowakabili.
Akiwa kwenye kijiji cha Lwandai Kata ya Mlola, Mbunge huyo alisema wapo baadhi ya maafisa ugani wamekuwa wakikaa ofisini badala ya kwenda wa wananchi ambao wanajishughulisha na kilimo ili waweze kuwapa elimu ya namna ya kulima kisasa jambo ambalo limekuwa likichangia kurudisha maendeleo yao nyuma.
“Ndugu zangu maafisa ugani tambueni kuwa mnajukumu kubwa la kuhakisha mnakwenda kwa wananchi kuwaelimisha juu ya kulima kilimo chenye tija kwao kwani hiyo itawasaidia kuweza kupata mafanikio kuliko wanavyofanya sasa lakini pia acheni kukaa ofisini “Alisema.
“Kwani elimu ambayo mnaweza kuitoa inaweza kuwa chachu ya wakulima kuweza kulima mazao mazuri yatakayokuwa ya ushindani na soko la kisasa hivyo jambo hilo ni muhimu sana “Alisema.
Alisema iwapo wakulima wataweza kufikiwa kwa wakati wataweza kuongeza tija kwenye uzalishaji ili kuweza kujiandaa vema na ujio ya fursa mbalimbali za miradi mikubwa inayokuja mkoani hapa ikiwemo bomba la mafuta ghafi kutoka hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga.
“Niwaambie ndugu zangu hii ni fursa muhimu kwa mkoa wa Tanga na wakulima ambao walikuwa wanazalisha mazao yao na kupeleka Dar es Salaam kwa kutumia usafiri wa laki nane hadi tisa lakini sasa mtakuwa mkitumia hata laki nne mpaka Tanga mjini kwani mradi ukianza kutakuwa na soko la uhakika”Alisema.
Aidha pia mbunge huyo alitumia nafasi hiyo kuwataka wakulima
kubadilika kwa kuongeza uzalishaji kutokana na uwepo wa soko la uhakika kwenye mazao yao katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya mkoa kwa lengo la kuinua vipato vyao.
Naye kwa upande wake,Mwenyekiti wa Kijiji cha Lwandai Kata ya Mlola wilayani humo,Juma Khamisi alimuhaidi mbunge huyo kuwa watashirikiana na maafisa ugani waliopo kwenye maeneo yao ili kuhakikisha wananchi wanapata elimu juu ya kulima kilimo chenye tija ili waweze kunufaika.
“Mh Mbunge tumepokea kauli yako kwa mikono miwili na sisi kama viongozi wa kijiji hiki tutahakikisha tunashirikiana na maafisa ugani,wakulima kwa lengo la kuongeza uzalishaji ambao utakuwa chachu ya kuweza kuwainua kiuchumi kwa kuchochoea kasi ya maendeleo kwao “Alisema.(Habari kwa Hisani ya Blog ya Kijamii ya Tanga Raha)
No comments:
Post a Comment