Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akisisitiza jambo wakati akiongoza kikao baina yake na wadau mbalimbali wanaotekeleza miradi ya usambazaji umeme vijijini awamu ya tatu. Kushoto ni Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu na kulia ni Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara, Haji Janabi.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (aliyesimama) akizungumza wakati wa Mkutano na wadau mbalimbali wanaotekeleza miradi ya usambazaji umeme vijijini awamu ya tatu. Kushoto kwake ni Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani.
Wakandarasi mbalimbali wanaotekeleza miradi ya usambazaji umeme vijijini awamu ya tatu, wakielezea hatua waliyofikia katika utekelezaji wake katika kikao baina yao na Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, Dodoma mwishoni mwa Juma.
Sehemu ya wajumbe wakiwa katika Mkutano wa Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani na wadau mbalimbali wanaotekeleza miradi ya usambazaji umeme vijijini awamu ya tatu, Dodoma mwishoni mwa Juma.
- Mkandarasi asiyeanza kazi ifikapo Machi 2 kukiona cha moto
- Viongozi TANESCO, REA wawasilishe taarifa kila robo mwaka
Na Veronica Simba – Dodoma
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amekutana na watendaji mbalimbali wanaosimamia na wanaotekeleza miradi ya awamu ya tatu ya kusambaza umeme vijijini na kutoa maagizo mazito yanayolenga kufanikisha mradi huo kikamilifu.
Mkutano huo uliofanyika mwishoni mwa Juma, Januari 13 mwaka huu, Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma, ulihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Kalemani alitoa maagizo kwa wajumbe ambao ni wazalishaji na wasambazaji wa nguzo, transfoma na nyaya za umeme, wakandarasi wanaotekeleza mradi husika katika maeneo mbalimbali nchini na wataalam wanaosimamia utekelezaji wa mradi huo kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA); kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake ipasavyo.
Kwa upande wa wakandarasi, Dkt. Kalemani aliwaagiza kuhakikisha kila mmoja anaanza utekelezaji wa kazi halisi (physical work) kabla ya tarehe 2 Machi mwaka huu vinginevyo Serikali itawachukulia hatua za kisheria. “Asiwepo mkandarasi yeyote ambaye atakuwa hajaanza kazi baada ya tarehe hiyo, alisisitiza.”
Aidha, Waziri alitoa maagizo kwa wakandarasi kuwasilisha kwa TANESCO mpango-kazi unaobainisha namna watakavyotekeleza kazi husika ifikapo mwisho wa mwezi huu wa kwanza. Akifafanua kuhusu agizo hilo, alisema kwamba uwasilishaji wa mpango-kazi utarahisisha ufuatiliaji wa utekelezaji wa kazi husika. Sambamba na agizo hilo, aliwaagiza pia viongozi wa ngazi za juu wa TANESCO na REA kwa kushirikiana na Wajumbe wa Bodi zao, kuhakikisha wanatembelea maeneo inapotekelezwa miradi ya umeme vijijini na kuandaa taarifa kila robo mwaka ambayo wataiwasilisha wizarani.
“Pamoja na kwamba wahandisi wanaosimamia kazi wako huko, lakini ninyi pia mnapaswa mtembelee miradi hiyo kujionea utekelezaji wake na mtuletee taarifa kila robo mwaka. Mtueleze changamoto gani mmezikuta na hatua gani mmechukua kusawazisha mambo pale inapobidi. Ni vema ninyi kukagua na kuchukua hatua mapema kabla sisi hatujafika huko.”
Agizo jingine alilolitoa Waziri Kalemani ni kwa wazalishaji na wasambazaji wa nguzo za umeme, transfoma na nyaya za umeme kuwaandikia barua TANESCO itakayoeleza uwezo wao katika kutekeleza kazi hiyo. Aliagiza barua hizo ziwasilishwe ifikapo Jumatano tarehe 17 Januari, 2018 na kuwataka TANESCO kuziwasilisha barua hizo wizarani, siku mbili baada ya wao kuzipokea yaani ifikapo Ijumaa, Januari 19 mwaka huu.
Vilevile, Dkt. Kalemani aliwataka wakandarasi wote, kuandika barua REA wakieleza mpango wao wa mahitaji ya vifaa walivyoagiza kwa wazalishaji na wasambazaji. “Barua hiyo ibainishe umeweka oda lini kwa mzalishaji na ni vifaa gani hasa umeagiza na ziwasilishwe REA ifikapo Ijumaa, Januari 19 mwaka huu.” Aidha, Waziri Kalemani aliagiza wataalam wa serikali wanaosimamia miradi hiyo kuzipitisha barua husika kabla hazijawasilishwa REA.
Waziri alisisitiza kuwa ni lazima vifaa vyote zikiwemo transfoma, nguzo na hata nyaya za umeme vitoke ndani ya nchi kama Serikali ilivyoagiza. Alisema kuwa Serikali imejiridhisha kwamba vifaa vyote hivyo vinapatikana ndani ya nchi hivyo alitahadharisha kuwa asitokee yeyote akaagiza kutoka nje ya nchi.
Suala jingine ambalo Waziri alizungumzia ni kuhusu umuhimu wa wazalishaji na wasambazaji wa nguzo za umeme kuhakikisha wanazingatia viwango vya ubora. Alisema kuwa ubora wa bidhaa hizo ni lazima uzingatiwe kutokana na umuhimu wake. Akifafanua zaidi, alisema kuwa Serikali haitamvumilia mzalishaji anayesambaza nguzo ambazo zinaoza na kuharibika ndani ya muda mfupi tofauti na matarajio kwani hiyo itailetea hasara Serikali.
Aliwataka wakandarasi kuhakikisha wanasambaza umeme pasipo kuruka kijiji chochote na kuyapa kipaumbele maeneo muhimu kama vile vituo vya afya, shule, miradi ya maji, masoko na taasisi mbalimbali za umma.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mgalu aliwasisitiza wakandarasi kutumia nguvukazi iliyopo katika maeneo yao ya kazi kwa kuwaajiri wananchi wa maeneo husika kufanya kazi zisizohitaji utaalam. Alisema kuwa hakuna haja ya kuajiri vibarua kutoka sehemu za mbali wakati wapo wananchi katika maeneo husika wanaoweza kufanya kazi hizo.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Haji Janabi, Kaimu Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli James Andilile, Mkurugenzi Mkuu wa REA Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka ambao wote waliahidi kutekeleza maagizo yaliyotolewa kwao na Waziri pamoja na Naibu Waziri.
No comments:
Post a Comment