ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 11, 2018

WAZIRI MKUU MAJALIWA AIPONGEZA KAMPUNI YA PREMIUM AGRO CHEM LTD KWA KUSAMBAZA MBOLEA KIASI KIKUBWA NCHINI

Na Dotto Mwaibale

WAZIRI Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa, ameipongeza Kampuni ya Premium Agro Chem Limited inayojihusisha na mbolea, kutokana na kazi nzuri na kutia ya kusambza kiasi kikubwa cha mbolea kwa wakulima nchini na hivyo kusaidia kupunguza adha iliyokuwa ikiwasumbua baadhi ya wadau wa sekta hiyo.


Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo ya pongezi jana alipokuwa akikagua zoezi la upakiaji wa mbolea na usafirishaji ili kufikia malengo ya kutekeleza agizo la hivi karibuni lililotolewa na Rais Dkt.John Pombe Magufuli, Ikulu Jijini Dar es Salaam.



Rais Magufuli, alimuagiza Waziri Mkuu kusimamia zoezi hilo kwa ajili ya kumaliza malalamiko ya wakulima wa mazao ya chakula na biashara kwa mikoa yenye uzalishaji mkubwa wa chakula.



Mikoa maarufu kwa uzalishaji huo inafahamika kama The Big  ni Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe na Ruvuma.



Akizungumza na watendaji wa kampuni hiyo, Waziri Mkuu aliipongeza kutokana na uamuzi wao wa kukubali kufanya kazi hiyo usiku na mchana na kusaidia kupunguza malalamiko ya wakulima.



"Kwa kweli ninawapongeza kwa kazi nzuri, mmetusaidia kwa kiwango cha juu, tunawashuru kwa kazi mliyoifanya na mnayoendelea kuifanya kwa nia njema, huu ni uzalendo mkubwa na unaostahili kupongezwa na kuungwa mkono na kila mpenda maendeleo," alisema Waziri Mkuu Majaliwa.



Alisema wakulima wa mazao ya chakula wanahitaji huduma ya kufikishiwa mbolea kwa wakati, lakini kwa taarifa nilizozipata, kazi kubwa imefanywa na kampuni yenu ndani ya siku mbili hizi, yamesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza kama sio kumaliza kabisa malalamiko ya wadau wenu.



Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba, alitumia muda huo kumweleza Waziri Mkuu, kwamba kampuni hiyo imefanyakazi kubwa usiku na mchana kupakia mbolea kwa ajili ya mikoa iliyokuwa na changamoto nyingi.



Alisema mpaka jana usiku, magari makubwa ya kubeba migizo mali ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), yalipakiwa kwa ajili ya kusambaza mbolea zaidi ya tani 600 kwa mikoa ya Rukwa na Katavi.



Lakini pia Mheshimiwa Waziri Mkuu, mawakala wa kampuni hii ya Premium wameendelea kuja hapa na kuchukua mbolea kwa ajili ya kukabilia na hali ya mahitaji makubwa yanayowakabili wakulima vijijini," alisema Waziri Tizeba na kuongeza kwamba kampuni hiyo imeendelea kushirikiana bila masharti na Kampuni ya Taifa ya Mbolea kusambaza mbolea hizo katika maeneo ambayo wao hawana mawakala ama hawana matawi ya kuuzia.


(Imeandaliwa na mtandao wa www.habari za jamii.com)

No comments: