Kama unadhani Balozi mteule, Dk Willibrod Slaa amekuja nchini kwa ajili ya kuapishwa utakuwa umekosea sana. Yupo nchini kushughulikia usajili wa Hospitali ya CCBRT.
Katibu mkuu huyo wa zamani wa Chadema, ametoa kauli hiyo leo Februari 6, 2018 wakati akihojiwa katika kipindi cha 360 kinachorushwa na Kituo cha Televisheni ya Clouds.
“Familia yangu nimeiacha Canada, wengine wanajua, sikuja kwa sababu ya ubalozi. Mimi ni mwenyekiti wa CCBRT ndicho kimenileta na wengine mnafahamu katika nchi yetu mengi yanafanyika,” amesema.
Novemba 23 mwaka jana, Rais John Magufuli alimteua Dk Slaa kuwa balozi, lakini mpaka sasa hajaapishwa na kupangiwa kituo cha kazi.
Dk Slaa ambaye kwa sasa anaishi Canada alitangaza kuachana na siasa kutokana na kutofautiana na chama chake katika kumpokea Edward Lowassa aliyehama kutoka CCM na baadaye kupitishwa kuwa mgombea urais kupitia muungano wa Ukawa.
Alisema chama chake hakikutekeleza makubaliano waliyoafikiana ya kuwapokea baadhi ya makada wa CCM akiwamo Lowassa.
Katika kipindi hicho, Dk Slaa ameulizwa kama amekuja kula kiapo na kupangiwa kituo cha kazi, lakini amepinga jambo hilo na kubainisha kuwa amekuja kushughulikia usajili wa hospitali hiyo kwa kuwa yeye ni mwenyekiti wa bodi.
Amesema kwa mujibu wa mabadiliko ya sheria, CCBRT inatakiwa kujiandikisha upya vinginevyo itafutwa.
Kuhusu taarifa kuwa ameajiriwa katika duka kubwa la bidhaa za nyumbani (Supermarket) la Costco lililopo Oakville, Toronto nchini Canada, amesema: “Hizo ni propanganda nisingependa kuzizungumza lakini Supermarket inayozungumzwa si kama mnavyofikiri ni kubwa.
“Kitu kikubwa tunatofautiana katika mtazamo, fikra tunavyofanya vitu vyetu. Canada haina mwenyewe kuna raia wa kutoka kila nchi. Sisi hapa tunasema hapa kazi tu lakini kule ni maisha. Unakuta waziri anatoka ofisini kwake anakwenda kufanya kazi nyingine, baadaye anatoka na kwenda kufanya nyingine. Kufanya kazi tatu ni kawaida.”
Ametolea mfano ufanyaji kazi wa Canada na Tanzania amesema baadhi ya Watanzania huingia ofisini na kusoma magazeti, au kutumia simu kufanya biashara zao.
“Canada utaingia ofisini na simu au ipad lakini utaiacha getini na matokeo yake nchi ile ni matajiri. Watu ni matajiri kila mtu ana utambuliso wa maisha mazuri ni kwa sababu wanafanya kazi na huduma zote ziko vizuri,” amesema.
Kuhusu kufunga ndoa amesema: “Siasa za Tanzania zilichangia mimi kutokufunga ndoa kwa kipindi chote lakini Februari 2016 kule Canada nilifunga ndoa (na Josephine Mushumbusi), ile si ndoa kwani tulishakaa, kanisa ilichokuja kufanya ni kuhalalisha tu.”
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment