ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 12, 2018

ELIMU JUMUISHI, NGUZO YA KUWALINDA WENYE UALBINO.

Na Shushu Joel, Simiyu


KATIKA jamii mbalimbali, awali ilikuwa imejengeka dhana ya kuwa mwanamke akizaa mtoto mwenye ualbino inawezekana akawa amerogwa, au katika uzao wake wamelaaniwa, pasipo kujua kuwa mtoto mwenye ualbino anaweza kuzaliwa endapo wazazi wawili wanapokuwa na vinasaba vya ualbino.

Hali hiyo iliwafanya wanawake kutaliki kwa kukataliwa na waume zao au watoto hao kuuwawa bila sababu na kukosa haki yao ya kuishi kama watoto wengine, huku wengine wakiuwawa kwa lengo la kutajirisha watu, jambo ambalo sio kweli.

‘’nimewahi kushuhudia mama mmoja alijifungua mtoto mwenye ulemavu wa ngozi (albino) akakataa katu kumnyonyesha, hatimaye mtoto akafariki dunia kwa madai kuwa mtoto huyo ni mkosi kwake na laana akidai amerogwa na wachawi’’ anasimulia Alex Julius Katekista wa kanisa katoliki Mhunze wilayani Itilima mkoani Simiyu.

Julius anaendelea kueleza kuwa mama huyo (ambaye hakumtaja jina) alijifungua tena mtoto wa pili na yeye akiwa na ulemavu wa ngozi baada ya kubaini hali ile ilibidi kumnyonyesha na kumlea.

Anasema kitendo kile kilimuumiza sana kwani ni jambo lisilovumilika na kufumbiwa macho ndani ya jamii kutokana na kwamba watu wote ni sawa na wanastahili kutendewa haki bila kujali hali walizonazo.

Anaongeza kuwa jamii ya Simiyu ilikuwa imejengeka katika dhana ya kuwa mwanamke akizaa mtoto mwenye tatizo la ukosefu wa madini ya mellanin (albino)anakuwa amerogwa ndani ya uzao wake bila kujua kuwa miongoni mwa wazazi wa mtoto huyo wanakuwa na vinasaba vya ualbino.


Anaongeza kuwa jamii nyingi imekuwa haina elimu ya uzazi hasa jinsi watoto wenye ualbino wanavyozaliwa, ya kuwa wanatokana na wazazi wawili kukutana wakiwa na vinasaba vya ualbino.

Julius anabainisha kuwa baada ya kuona hali hiyo katika jamii inayomzunguka, alianza kutoa elimu ya uzazi kwa njia ya ibada kanisani kwa kuwabainishia kuwa mtoto mwenye ualbino anaweza kuzaliwa katika familia yeyote.


‘’jamii inatakiwa kubadilika ili kuondokana na unyanyapaa, maana baadhi yao wamekuwa hawawapendi watoto wenye ualbino bila kujua jinsi mtoto huyo anaweza kupatikana (kuzaliwa)’’ alisema Julius.

Sitta Kibinza mkazi wa Nanga wilayani Itilima, mkoa humo anasema kuwa katika kijiji chao suala la unyanyapaa limekithiri kwa wazazi wenye watoto wa kariba hiyo hiyo ya ualbino.

Anasema kuwa, wao waliwahi kupeleka mtoto mmoja mwenye ualbino katika kituo cha kulelea watoto cha Buhangija mkoani Shinyanga, kupitia ufadhili wa wordvision, kutoka familia ya Ng’habi Polini lakini hadi leo wazazi hao hawajawahi kwenda kumtembelea na kumjulia hali mtoto wao.

Kibinza anongeza kuwa mambo ya unyanyapaa yapo katika jamii nyingi zisizokuwa na uelewa juu ya malezi ya watu wenye ualbino, elimu inahitajika ili kuwa na jamii yenye uelewa unaofanana.

‘’katika familia ya Mzee Polini wamezaliwa watoto wawili wenye ulemavu wa ngozi (albino), wazazi wamekuwa hawana mwamko wa kuwapeleka watoto hao shule, hivyo tulilazimika kumchukua mtoto mmoja kwenda Buhangija, hadi sasa wazazi hawajaenda kumwona, huo nao ni unyanyapaa na uelewa mdogo’’ anasema.

Kutokana na hali halisi ya tatizo hilo Mkoani Simiyu Shirika la Mass Media Bariadi, linalotekeleza Mradi wa kupinga mauji ya wenye ualbino kupitia Kampeni ya Tokomeza Mauji ya Walemavu wa Ngozi Simiyu limeamua kujikita kikamilifu katika utoaji wa elimu juu ya suala hilo katika wilaya za Bariadi, Itilima na Maswa.

Mradi huo unaotekelezwa katika kata 23 mkoani hapa unaendeshwa kwa kipindi cha miezi sita ili kuoengeza uelewa wa pamoja katika jamii na kutokomeza mauaji ya watu wenye ualbino yaliyokuwa yamekithiri.

Aidha, mradi huo unaolenga kutoa elimu kwa kujumuisha kwa viongozi wa dini, waganga wa tiba asili, watu mashuhuri, jeshi la polisi, viongozi wa serikali (watendaji wa vijiji na kata), walimu, madiwani na wananchi ili kuweza kuwalinda kwa pamoja watu wenye ualbino.

Lakini pia, kuihimiza jamii kuwashirikisha watu wenye ualbino katika shughuli za maendeleo hasa kulekea uchumi wa kati wa Tanzania ya viwanda kwa makundi ya wawakilishi wa Waganga wa jadi, wenyeviti wa vijiji, viongozi wa dini na kimila,watu mashuhuri, polisi kata na walimu.

Mratibu wa mradi huo, Frank Kasamwa anasema kuwa hadi sasa jamii imeshaanza kupata mwamko kuwa, mtoto mwenye ualbino anaweza kuzaliwa katika familia yeyote endapo wazazi wao watakuwa na vinasaba vya ualbino.


Anasema kuwa hadi sasa wameshaanza kuona matokeo chanya juu ya mabadiliko katika jamii ili kuimarisha ya ulinzi ambapo kamati za ulinzi za vijiji na kata kwa kuanza kushirikiana ili kuwalinda watu wenye ualbino na kuhakikisha usalama unapatikana katika maeneo ambayo wenye ualbino wanaishi.

Anaongeza kuwa kata za Nkololo, Ihusi na Mwaumatondo wameanza mkakati wa kuimarisha kamati za ulinzi za kata ili kuhakikisha wanazungukia kamati za vijiji na kuhakikisha zinatimiza wajibu wao, na kuongeza kuwa wenye ualbino wamekuwa wakishirikishwa katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

‘’suala la unyanyapaa umeisha na tunahakikisha wanashirikishwa katika uchumi wa viwanda na shughuli mbalimbali za ujenzi wa taifa ambapo hofu itatoweka na ulinzi wao utakuwa umeimarika’’ anasema Kasamwa.

Aidha mradi huo, unajikita kubuni mbinu za ushawishi na utetezi wa kuwalinda na kuwatetea wenye ualbino pamoja na mbinu za kuishawishi jamii kuwashirikisha watu wenye ualbino katika huduma muhimu za kijamii ikiwemo kuhudhulia kliniki lkwa ajili ya matibabu kwa kuzingatia hali yao ya ngozi na kuondoa unyanyapaa miongoni mwa jamii.

Mradi huo pia unayolenga kutoa elimu ya kupinga mila potofu za mauaji ya watu wenye ualbino, kiuhimiza jamii yenye watu wenye ualbino kwenda kujisajili ofisi ya ustawi wa jamii ili waweze kutambulika.



Watu wenye Ualbino (WWU) 31 kati yao wanaume 15 na wanawake 16 wamenufaika kutokana na elimu inayoendelea kutolewa mkoani hapa kuanzia shuleni hadi ngazi ya jamii, na mabadiliko hayo yanaweza kuwa ya kudumu kutokana na jamii kubabadili mtazamo dhidi ya mauaji ya watu wenye Ualbino katika jamii.

Katika kuwashirikisha viongozi wa serikali na waganga wa jadi ili kukemea kwa pamoja mila potofu zinazopelekea mauji ya watu wenye ualbino na kuwafanya waganga hao kuwa mabalozi wazuri katika jamii kwa sababu walikuwa wanatuhumiwa kuwa wanajihusisha na mauaji hayo.

Kupitia mabaraza ya maendeleo ya kata hizo, wameazimia kutunga sheria ndogo ndogo kwa kushirikiana na vijiji husika zitakazolenga kuwalinda, kuwatetea na kupinga unyanyapaa kwa watu wenye ualbino, pia kuelimisha jamii ili iweze kuondokana na imani potofu ya mauaji ya watu wenye ualbino.

Afisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Bariadi Samwel Temba anasema kuwa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi akipatikana katika jamii siyo laana au mkosi kama ilivyokuwa imejengeka katika jamii.


Anaongeza kuwa kibailojia, mzazi anaweza kuwa na tabia tatu, ambapo moja mzazi anaweza kuwa hawezi kabisa kuzaa mtoto mwenye ualbino (AA), pili hana ualbino lakini anaweza kuazaa mtoto mwenye ualbino (Aa) na tatu ambaye ana ualbino na anaweza kuzaa mtoto mwenye ualbino (aa).

‘’kuzaliwa mtoto mwenye ualbino ni pale wazazi wawili (mke na mme) wanapokutana wakiwa na vinasaba vya ualbino, lakini kama mzazi mmojawapo hana vinasaba na mmojawapo ana vinasaba, hawawezi kupata mtoto mwenye ualbino, jamii inatakiwa kujenga uelewa juu ya suala hilo’’ anasema Temba.

Temba anawataka viongozi katika maeneo mbalimbali kupeleka elimu katika jamii ili kuondokana na tatizo la mauaji na ukataji wa viungo vya watu wenye ualbino linaloendelea kuibukia katika maeneo mbalimbali.

Nae mkazi wa Bariadi Victor Masunga anasema kuwa hali kwa sasa inaanza kubadilika matukio ya unyanyapaa na mauaji ya ualbino yanapungua kwa kasi tofauti ya miaka ya nyuma.


Victor anasema elimu inayotolewa imewafanya wananchi na jamii kwa ujumla kuthamini haki za walemavu hao wa ngozi kuendelea kuishi na kushiriki shughuli za kimaendeleo ipasavyo.

Sambamba na hilo ameiomba serikali izidi kutoa elimu juu ya namna watu wenye ulemavu wa ngozi unavyopatikana ili kila wananchi ajue kuwa tatizo hilo ni la kitaalam na si vinginevyo.


Afisa Maendeleo wa wilaya ya Maswa Abakus Kaluletela anasema kuwa Walemavu wa Ngozi (albino) Wilayani humo wamekuwa hawahudhurii kliniki ili kupata vipimo na matibabu ya kuwakinga na Magonjwa ya ngozi.

Anaongeza kuwa walemavu hao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya matibabu kwa kuwa wanaishi kwa maradhi hasa yatokanayo na mionzi ya jua kwa kuwa ngozi zao zina upungufu wa mellalini.

Abakus anasema kuwa Walemavu wamekuwa hawajitokezi kwa wingi pindi yanapotokea mashirika na wafadhili kwa ajili ya kuwapatia huduma za kiafya ikiwemo vipimo na matibabu.

‘’walemavu wa maswa wamekuwa hawafiki wote katika vituo vya afya ili kupata vipimo na matibabu…wilaya nzima tuna walemavu 43, lakini waliofika kupata huduma mwezi wa tano ni 18 tu, hivyo wajitokeze kwa wingi ili kufanyiwa vipimo na kupata huduma za kiafya’’ anasema Abakus.

Anaongeza kuwa shirika la standing Voice hutoa huduma hiyo kila baada ya miezi sita kwa kuwapatia miwani na mafuta kwa ajili ya kulainisha ngozi zao na madaktari wa vipimo na wakibainika wanapelekwa muhimbili au KCMC kwa matibabu.

Mradi huo wa kutokomeza Mauaji ya watu wenye Ualbino unatekelezwa katika wilaya za Maswa, Itilimaa, Bariadi vijijini na halmashauri ya mji wa Bariadi kwa kuzihusisha kata 23, wilaya ya Maswa hizo ni Mwamashimba, Buchambi, Kadoto, Ngw’ang’onoli, Mwabayanda na Shishiyu.


Wilaya ya Itilima kata zilizohusishwa ni Mhunze, Budalabujiga, Sagata, Chinamili, Ikindilo na Ndoleleji, Wilaya ya Bariadi vijijini kata zilizo husishwa ni Dutwa, Sapiwi, Ikungulyabashashi, Banemhi, Nkololo, Mwaumatondo na Ihusi na kwa Halmashauri ya mji Bariadi ni kata ya Nyakabindi na Guduwi.


Mradi huu unaendeshwa kwa kipindi cha miezi sita kwa ufadhili wa shilika la The foundation for civil society lengo ikiwa ni kuwa sauti ya pamoja juu ya kuwalinda wenye ualbino.

No comments: