Kabla ya kauli ya Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi kuwa hakuna mgongano wa Katiba ya Muungano na Katiba ya Zanzibar wakereketwa na muungano na katiba mpya ni kama walikuwa wamekaa kimya.
Lakini, baada ya kauli hiyo aliyoitoa wakati akijibu swali la Mbunge wa Wingwi (CUF), Juma Kombo Hamadi lililohusu mgongano wa katiba hizo, kuwa hakuna mgongano unaosababisha ongezeko la kero za Muungano wala mgongano wa kimamlaka baina ya pande hizo mbili, wakereketwa hao wameibuka na kuibua hoja mpya za kupigania katiba mpya, itakayowezesha Zanzibar kupata mamlaka kamili.
Hata hivyo, tayari Profesa Kabudi katika jibu lake amekwishasema hakuna haja ya kuleta mapendekezo ya kubadilisha Katiba.
Waziri ambaye pia ni msomi wa sheria, anasema Katiba ya Jamhuri ya Muungano imeweka utaratibu mahususi wa kushughulikia tafsiri na utekelezaji wa mambo yanayobishaniwa kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“Hadi sasa hakuna upande wowote baina ya Serikali hizi mbili ambao unatafsiri tofauti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano au utekelezaji wake. Hivyo kwa kuzingatia kuwa hakuna mgongano wa Katiba kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Serikali haina sababu ya kuleta mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba ili kuondoa changamoto hiyo ambayo haipo.” alifafanua Profesa Kabudi.
Baada ya kauli hiyo, Jukwaa la Katiba kupitia mwenyekiti wake, Hebron Mwakagenda lilitoa tamko likieleza kusikitishwa na kauli ya Profesa Kabudi, licha ya kumtambua kama msomi aliyebobea katika sheria na Katiba.
“Jukata na Watanzania wanatambua mchango wa Profesa Palamagamba Kabudi alipokuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba (TMK) kipindi cha mchakato wa Katiba Mpya.
Jukata na Watanzania kwa ujumla wanaamini kuwa tamko la Profesa Kabudi halijatoka moyoni mwake bali ni kwa ajili ya kutimiza matakwa ya kisiasa ya sasa,” limesema jukwaa hilo.
Jukwaa hili limeongeza kuwa endapo kauli ya Profesa Kabudi inatoka moyoni mwake, basi alikuwa na uwezo na nafasi ya kukataa uteuzi wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete wa kuingia kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba mwaka 2011 na alikuwa na nafasi na uwezo wa kuishauri nchi hayo anayosema sasa.
“Kwa mshangao wa Watanzania walio wengi alikubali uteuzi na alipokea posho na stahili zote kama Kamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambazo zilitokana na fedha za walipa kodi na wavuja jasho wa nchi hii,” limesema jukwaa hilo.
Jukwaa hilo limesema Profesa Kabudi si wa kwanza kuisaliti kauli yake kwani hata baadhi ya wasomi wamewahi kuripotiwa kukana misimamo yao kutokana na nyadhifa wanazopewa.
Jukwaa hilo limesema linaamini bado kuna sababu nyingi za kuandika Katiba na zimeongezeka baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kuliko hata ilivyokuwa wakati wa mchakato mwaka 2011-2014.
“Watanzania wasikatishwe tamaa na tamko la Profesa Kabudi kwani maslahi ya Taifa ni muhimu kuliko maslahi ya mtu mmoja na kuwa Katiba ni ya Watanzania wote na si ya viongozi na vyama vya siasa pekee,” alisema.
Jukwaa hilo pia linamkumbusha Rais John Magufuli kufikiria upya juu ya uamuzi wake wa awali kuhusu kuanzisha mchakato wa Katiba Mpya ili kipindi hiki cha uongozi wake akamilishe mchakato huo.
Katika uamuzi wa awali, Rais Magufuli alisema suala la Katiba Mpya si kipaumbele chake na kwamba katika kampeni zake hakuahidi popote Katiba Mpya.
Mbali na Jukwaa la Katiba, Wazanzibari kadhaa nao walionyesha kutokubaliana na kauli ya Profesa Kabudi, akiwemo Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Saleh ambaye ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa, Waziri huyo alikiri kuwepo kwa mgongano wa Katiba alipokuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Nimefadhaishwa na Profesa Kabudi kuwa hakuna mgongano wa Katiba Zanzibar na Katiba Tanzania, ambapo tukiwa katika Tume ya Warioba (Jaji Joseph) tulitoka kauli moja kuwa kuna mgongano mkubwa kiasi cha kutishia Muungano na tukaamua kuwepo Serikali tatu,” alisema mbunge huyo. Alisema kauli ya waziri huyo ni ujumbe kuwa Zanzibar iendelee kuwa mfukoni mwa Tanganyika.
Ally Saleh aliyekuwa pia mjumbe wa Tume hiyo, aligusia suala la Rais John Magufuli kuwaagiza Waziri wa Uchukuzi wa Muungano, Profesa Makame Mbarawa na mwenzake wa Zanzibar, Balozi Ali Abeid Karume, kusitisha usajili wa meli mpya hapa nchini mpaka hapo itakapotangazwa vinginevyo.
Rais Magufuli alitoa agizo hilo hivi karibuni jijini Dar es Salaam baada ya kufanya mkutano na wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje kutokana na taarifa za kukamatwa kwa dawa za kulevya katika meli zinazopeperusha bendera ya Tanzania, ambazo hadi sasa zimefikia meli tano, nyingi zikiwa na usajili wa Zanzibar.
“Leo nimerudishwa darasa la katiba na Mwalimu wangu Profesa Kabudi alilojibu bungeni kuwa ilikuwa ni sawa Rais Magufuli kumwita Dar es Salaam, kumpa hadharani maelekezo Waziri Karume juu ya jambo ambalo sheria yake si ya Muungano na waziri asiye mteule wake na wizara isiyo ya muungano. Profesa amepotoka,” alisema Ally Saleh.
Mzanzibari mwingine aliyechangia mjadala huo ni Mwakilishi wa Mji Mkongwe, Ismail Jussa ambaye pia aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter:
“Ikiwa tafsiri ya Muungano ni ile iliyotolewa leo na Profesa Palamagamba Kabudi (ambaye si Waziri wa Muungano na wala hana mamlaka Zanzibar), basi Wazanzibari hatuoni ufumbuzi mwingine zaidi ya kuyarudisha mamlaka kamili ya nchi yetu,” alisema na kuongeza:
“Sheria Kuu ndani ya Jamhuri ya Muungano si Katiba, bali ni mkataba wa Muungano ambao ni Mkataba wa Kimataifa kati ya Tanganyika na Zanzibar ulioanzisha Muungano. Katiba zote mbili zimezaliwa na zinapaswa kuakisi mkataba huo.”
Vilevile Wakili maarufu, Awadh Said alitumia mtandao wa Jamiiforums akisema alichokifanya Profesa Kabudi amewaelewesha Wazanzibari kuwa Rais waliyemchagua anatambuliwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano kuwa waziri wa kawaida tu katika Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano.
“Kwa Zanzibar anakuwa “Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi” na kwenye Uchaguzi Wazanzibari walimchagua hivyo; kisha anaunda Serikali yake kwa kuteua Makamu wa Rais wawili na anateua mawaziri na anakuwa Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,” anasema na kuongeza:
“Katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano anakuwa Waziri wa kawaida tu. Kwenye hilo Baraza la Mawaziri, Rais wa Jamhuri ya Muungano ndiye anaongoza vikao na ikitokea hayupo vikao vinaongozwa na makamo wa Rais; na ikitokezea wote hawapo vikao vinaongozwa na waziri mkuu.”
Anakumbushia wakati Zanzibar inaungana na Tanganyika mwaka 1964, Mkataba wa Muungano ulieleza wazi kuwa Rais wa Zanzibar atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na iliendelea hivyo hadi mwaka 1994 ambapo hadhi yake ilishushwa kutoka kuwa Makamu wa Rais hadi Waziri wa kawaida.
“Mwaka 1992 wakati Tanzania inarejesha Mfumo wa vyama vingi iliibuka hofu kuwa endapo Serikali za pande hizi mbili zingekamatwa na vyama tofauti hali hiyo ingeleta sokomoko katika masuala ya Muungano.
“Ikaundwa Kamati ya Jaji Bomani ambayo ilipendekeza kuanzishwa kwa utaratibu wa mgombea mwenza ili kama mgombea akitokea upande mmoja wa Muungano basi mgombea mwenza atokee upande wa pili wa Muungano - na kuwa huyu mgombea mwenza ndiye atakuwa Makamu wa Rais wa Muungano badala ya Rais wa Zanzibar,” anasema Awadh.
Akifafanua zaidi anasema kuliibuka utata mwingine kuwa Rais wa Zanzibar atakuwa ametolewa kabisa katika mfumo wa kiuongozi wa Jamhuri ya Muungano. Ikaamuliwa aingizwe, ila awe waziri tu.
“Bunge la Muungano likarekebisha Katiba kukidhi mabadiliko hayo. Baadhi ya Wazanzibari walilipinga mno hili. Mnamo mwaka 1995, Wazanzibari 50 wakiongozwa na Mtumwa Said Haji (Kesi No 2 ya 1995) walikwenda kufungua kesi Tanzania Bara kupinga jambo hili. Kesi yao ilipigwa chini,” anakumbusha Awadh.
“Ulipofika wakati wa mawaziri kula kiapo cha utiifu na uaminifu kwa Rais wa Muungano, kukawa na ukakasi kwa Rais wa Zanzibar (wakati huo Dk Salmin Amour ‘Komandoo’ kwenda kula kiapo kwa “Rais mwenziwe”.
Utaratibu ukabuniwa kuwa Rais wa Zanzibar ale kiapo cha uaminifu mbele ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano,” anaongeza.
Akifafanua madaraka makubwa aliyonayo Rais wa Jamhuri ya Muungano, Awadh anasema ndiye mwenye mamlaka makuu kwa Tanzania nzima na kuwa ni sahihi kwake kutoa maagizo kwa mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa vile yeye ni Mkuu wa Nchi na yeye ni Amiri Jeshi Mkuu.
“Tanzania Bara kuna wapiga kura zaidi ya milioni 20. Zanzibar kuna wapigakura laki tano tu. Mgombea anaweza kuwa Rais wa Muungano kwa kura za Tanzania Bara tu, hata kama kura zote za Zanzibar zimemkataa na hakuambulia hata kura moja,” anasema na kuongeza:
“Kinadharia mgombea anaweza kushinda bila kura za Zanzibar na anaweza hata asiende kufanya kampeni Zanzibar na akanadi hadharani kuwa hataki kura yoyote kutoka Zanzibar. Aliyechaguliwa na wenzetu ana mamlaka juu yetu,” anasema.
No comments:
Post a Comment