Advertisements

Saturday, February 17, 2018

Madiwani Watatu wa CHADEMA wahamia CCM


ZIARA ya kwanza ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha, Lootha Sanare katika Wilaya ya Ngorongoro, imeanza kwa kimbunga na kuvunja ngome ya Chadema baada ya madiwani watatu wa chama hicho kujiengua na kuhamia chama tawala.

Sanare ameanza ziara juzi ya kutembelea wilaya zote saba za Mkoa wa Arusha kuangalia uhai wa chama na kuangalia kama ahadi za madiwani wa CCM kama zimeanza kutekelezwa pale walipoomba ridhaa ya kutaka kuchaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Katika ziara hiyo iliyoanza katika Tarafa ya Ngorongoro, ilianza kwa madiwani hao watatu kujiengua Chadema katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Wilaya ya Ngorongoro kilichohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa wilaya hiyo wakiongozwa na Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, William Ole Nasha.

Madiwani waliojiengua Chadema na kuhamia CCM kwa ridhaa yao ni Diwani wa Kata ya Ngorongoro, Daniel Orkeriy, Mwenyekiti wa Vijana wa Chadema Wilaya hiyo na pia Diwani wa Kata ya Ngoile, Lazaro Saitoti na Diwani wa Kata ya Loitole, Sokoine Moiv.

Viongozi hao walisema kujiengua kwao kumetokana na kukengeuka na kujikuta wakiwa Chadema bila kutafakari na uamuzi huo umewaathiri katika utendaji wao na kurudi kuijenga CCM na kuwa kitu kimoja kwa maslahi ya nchi.

Pili walisema uamuzi waliochukua ni utashi wao na siyo kushawishiwa kwa namna yoyote bali ni kuona yale waliyokuwa wakitaka kuyafanya sasa yanafanywa kwa kasi ya hali ya juu na Rais John Magufuli, hivyo kumewafanya kushawishika kurudi nyumbani baada ya kupotea mbugani kwa kufuata mkumbo.

Akizungumzia uamuzi huo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Sanare alisema ziara yake imeanza kwa mafanikio na kuongeza kuwa wakati wa kuizika Chadema wilayani Ngorongoro na Mkoa wa Arusha kwa ujumla umefika na kuwataka wana CCM kuwafungulia mlango wale wote waliopotea kurudi nyumbani kujenga nchi.

Aliwataka walioamua kung’ang’ania Chadema kama kupe kujitafakari na kuchukua uamuzi kuikubali kazi ya Rais Magufuli na kurudi CCM kwani kwa kufanya hivyo hakutakuwa kwa ajabu, bali uamuzi wa kijasiri.

Alisema mgombea wa Urais kupitia Ukawa, Edward Lowassa alikwenda Ikulu na kumsifu Rais Magufuli kwa kazi nzuri ya kujenga, na kuwataka wengine wenye roho ngumu kufanya hivyo kwani siyo dhambi. “Tufungue milango wanaCCM wenzangu na kuwapokea kwa mikono miwili wale waliokengeuka na kwenda Chadema kwani wameshakubali kuwa mziki wa Rais Magufuli siyo muziki wa kawaida,” alisema Sanare.

Mbunge wa jimbo hilo, Ole Nasha ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, aliwashukuru madiwani hao kwa uamuzi huo na kuwakaribisha kufanya kazi yenye lengo la kukijenga chama katika wilaya hiyo.

No comments: