ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, February 3, 2018

ZAIDI YA CHUPA MIL 1.5 ZA VIUWADUDU ZASAMBAZWA KWA WAKULIMA WA PAMBA KUDHIBITI MAGONJWA

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa akijibu maswali bungeni Mjini Dodoma, Leo 2 Februari 2018

Na Mathias Canal, Dodoma

Serikali imesema kuwa Zoezi la upokeaji na usambazaji wa viuwadudu linaendelea na hadi kufikia tarehe 24 Januari, 2018 jumla ya chupa 1,733,139 za viuwadudu zimekwisha kusambazwa kwa wakulima na chupa nyingine 7,287,216 zitaendelea kusambazwa kati ya sasa na  mwezi Machi, 2018 ili kukidhi mahitaji katika msimu huu wa kilimo.

Hayo yamebainishwa leo 8 Februari 2108 na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa wakati akijibu Swali la Mhe Khadija Hassan Aboud Mbunge wa Viti Maalumu Zanzibar aliyetaka kufahamu namna ambavyo serikali imejipanga kukidhi mahitaji ya viuwadudu kwa wakulima wa Pamba nchini.

Alisema kuwa Katika Msimu wa Kilimo 2017/2018 wakulima wameitikia kwa vitendo azma ya Serikali ya kuimarisha kilimo cha pamba nchini kwa kuongeza eneo linalolimwa pamba kutoka wastani wa ekari 1,000,000 hadi wastani wa ekari 3,000,000, Kutokana na mwitikio huo, hadi tarehe 22 Desemba, 2017 jumla ya ekari 1,500,000 zilikuwa zimelimwa na kupandwa zao la Pamba na kuhitaji chupa (acrepacks) 4,500,000 za viuwadudu.

Alisema, kwa kuwa mvua zinaendelea kunyesha wakulima wameendelea kupanda pamba ambapo hadi tarehe 24 Januari 2018 taarifa zinaonyesha kuwa jumla ekari 3,006,785 zimelimwa pamba ambapo Kutokana na eneo hilo kulimwa pamba, makisio ya chini ya uzalishaji wa pamba ni kilo milioni 600 sawa na tani 600,000 za pamba.

Eneo lote lililo limwa pamba linahitaji jumla ya chupa 9,020,355 za viuwadudu zenye thamani ya shilingi bilioni 36 ambapo Serikali kupitia Bodi ya Pamba Tanzania imenunua jumla ya chupa 5,300,000 na Kampuni binafsi zimenunua chupa 450,000. 

Aidha, jumla ya vinyunyizi vipya 16,500 vimenunuliwa ambapo kati ya vinyunyizi hivyo 10,157 vimekwisha kusambazwa kwa wakulima na usambazaji unaendelea huku vinyunyizi 6,000 vikiwa vimekarabatiwa ili kutosheleza mahitaji ya wakulima.


MWISHO

No comments: