Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dustun Kitandula (katikati) akiwasha umeme katika Kijiji cha Nyabange wilayani Butiama, Machi 15 mwaka huu, wakati wa ziara ya Kamati hiyo mkoani Mara kukagua miradi ya umeme. Kushoto ni Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu.
Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu (kulia) na Kamishna wa Nishati Mhandisi Innocent Luoga (kushoto) wakitoka katika nyumba ya mkazi wa kijiji cha Idala wilayani Nzega (inayoonekana pichani), ambayo iliwashiwa umeme wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kijijini hapo, Machi 16 mwaka huu.
Mbunge wa Jimbo la Chumboni Zanzibar ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Ussi Pondeza akiwasha umeme katika Kijiji cha Kisaki Mkoa wa Singida, wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kijijini hapo Machi 18 mwaka huu. Kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu.
Kazi ya kufunga umeme ikiendelea kwa hatua za mwisho katika Kijiji cha Kisaki mkoani Singida, kama taswira hii ilivyochukuliwa wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini katika eneo hilo, Machi 18 mwaka huu.
Na Veronica Simba
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imepewa heshima ya kuwasha umeme katika vijiji vitatu ambavyo huduma ya kupeleka umeme imekamilika.
Zoezi hilo lilifanyika kwa nyakati tofauti, Machi 15 hadi 18 Mwaka huu, wakati wa ziara ya Kamati hiyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya sekta za nishati na madini katika Mikoa kadhaa nchini.
Vijiji vilivyowashiwa umeme ni Nyabange kilichopo Wilaya ya Butiama mkoani Mara, Kijiji cha Idala wilayani Nzega pamoja na Kijiji cha Kisaki kilichopo Mkoa wa Singida.
Akitoa ufafanuzi kwa Kamati husika, Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu alisema kwamba, Vijiji hivyo vimepata huduma ya umeme kupitia mpango wa upelekaji umeme vijijini unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na Mradi mkubwa wa umeme wa Backbone.
Mbali na kuwasha umeme katika Vijiji hivyo vitatu, Kamati pia ilitembelea na kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme katika vijiji vya Muryaza na Busegwe wilayani Butiama, vijiji vya Negezi, Mwaweya na Bulimba wilayani Kishapu Mkoa wa Shinyanga, kijiji cha Kitangiri wilayani Nzega pamoja na vijiji vya Kisaki na Nkunikana Mkoa wa Singida.
Aidha, Kamati ilikagua Kituo cha Kupooza Umeme cha Singida ambapo ujenzi wa Mradi wa Singida, Arusha, Namanga utaanzia ikiwa ni pamoja na upanuzi wa kituo hicho unaoendelea kupitia Backbone.
Katika ziara hiyo, viongozi mbalimbali wa Wizara walishiriki, akiwemo Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, Kamishna wa Nishati Mhandisi Innocent Luoga pamoja na viongozi kutoka REA na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Ziara hiyo ni moja ya majukumu ya kawaida ya Kamati.
No comments:
Post a Comment