ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 21, 2018

MAHAKIMU WAPYA WAFUNDWA

 Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali (wa pili kulia) akiongea na Mahakimu wapya 78 wa Mahakama za Mwanzo (hawapo pichani) walioripoti katika Ofisi za Mahakama Kuu- Kanda ya Dar es Salaam, wa pili kushoto ni Msajili-Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ilvin Mugeta, wa kwanza kushoto ni Bw. Edward Nkembo, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu-Mahakama ya Tanzania na wa kwanza kulia ni Mtendaji-Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha.

 
 Baadhi ya Mahakimu wapya 78 wa Mahakama za Mwanzo (hawapo pichani) walioripoti katika Ofisi za Mahakama Kuu- Kanda ya Dar es Salaam wakimsikiliza Mhe. Jaji Kiongozi katika mkutano huo.
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali (Katikati), Bw. Edward Nkembo, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu-Mahakama ya Tanzania (aliyeketi kushoto) na Mtendaji-Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha (kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Mahakimu wapya wa Mahakama za Mwanzo walioajiriwa hivi karibuni.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)

Na Mary Gwera, Mahakama
MAHAKIMU wapya wanaotarajia kuanza kazi rasmi ndani ya Mhimili wa Mahakama wametakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na taratibu za Mhimili huo.
Akizungumza na baadhi ya Mahakimu wapya wa Mahakama za Mwanzo walioajiriwa hivi karibuni katika Ukumbi wa Mahakama Kuu-Dar es Salaam mapema Machi 20, Jaji Kiongozi- Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali amewaasa Waajiriwa hao kufanya kazi kwa maadili na kutojihusisha na vitendo vya rushwa.
“Katika ufanyaji kazi wenu wa Uhakimu, mnatakiwa kuzingatia mambo makuu manne ya msingi ni; Ujuzi wa taratibu na mazoea ya Kimahakama, Uelewa kuhusu Sheria za Msingi ‘Substantive law’ na Sheria za Mwenendo ‘Procedural Law’ kuangalia mazingira ya utoaji haki na kadhalika,” alieleza Mhe. Wambali.
Aidha Jaji Kiongozi pia aliwataka Mahakimu hao pia kufanya kazi kwa kuwaheshimu Wadau wote wanaojumuika nao katika mchakato mzima wa utoaji wa haki, ikiwa ni pamoja na Makarani, Wazee na Baraza na wengineo.
“Heshimuni kila mtu mnayeingia naye Mahakamani, kila mtu ana mchango katika upatikanaji wa haki, na moja ya sifa ya Hakimu ni upole lakini upole sio udhaifu,” alisisitiza Mhe. Jaji Wambali.
Mbali na kuwaasa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili, Mhe. Jaji Kiongozi aliwaasa pia Mahakimu hao kutojihusisha na masuala ya siasa katika kazi zao.
“Ibara ya 113A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inasema, Hakuna Jaji au Hakimu anayeruhusiwa kuwa Mwanachama wa Chama chochote cha Siasa” alisisitiza Mhe. Jaji Kiongozi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu-Mahakama ya Tanzania, Bw. Edward Nkembo amesema kuwa jumla ya Mahakimu wapya 78 kati ya 100 wameripoti kazini.
“Jumla ya Mahakama wapya 78 wa Mahakama za Mwanzo wameripoti, hata hivyo baadhi wametoa taarifa ya kushindwa kuripoti kutokana na dharura mbalimbali,” alisema Mkurugenzi huyo.
Bw. Nkembo ameeleza kuwa baadhi ya Mahakimu na Watumishi wa Kada watakaoshindwa kuripoti ndani ya siku 14 tangu Machi 20, nafasi zao zitatafutiwa watu wengine watakaoomba na kukidhi vigezo.
Mahakimu hao na Watumishi wengine wa Kada mbalimbali walioajiriwa na Mahakama  hivi karibuni watasambazwa katika Mahakama mbalimbali nchini lengo likiwa ni kuongeza nguvu kazi katika kuendelea kuboresha huduma ya utoaji haki kwa wananchi. 

No comments: