Advertisements

Saturday, May 12, 2018

KAMATI YA BUNGE YA UTAWALA NA SERIKALI ZA MITAA YAIPONGEZA SERIKALI

Wajumbe wa Kamati ya Utawala za Serikali za Mitaa wakiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Selemani Jafo walipotembelea kukagua ujenzi wa shule ya sekondari Ihungo.
Wajumbe wa Kamati ya Utawala za Serikali za Mitaa wakiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Selemani Jafo katika shule ya sekondari Nyakato.
Majengo ya madarasa ya shule ya sekondari Ihungo.
Majengo ya madarasa ya shule ya sekondari Ihungo.
Majengo mapya wa shule ya Sekondari ya Nyakato.

Angela Msimbila, Kagera.

Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa imeipongeza Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa na nzuri inayoifanya ya kuzijenga upya shule mbili za sekondari za Ihungo na Nyakato ambazo ziliathiriwa na maafa ya tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera mwaka 2016.

Kamati hiyo imetoa pongezi hizo leo baada ya kuzitembelea shule hizo na kujionea namna zilivyojengwa upya kisasa.

Kamati hiyo ilikuwa katika ziara maalum mkoani Kagera ya kukagua ujenzi wa shule hizo ambazo kukamilika kwake kutawezesha Vijana watakaochaguliwa kujiunga na kidato cha tano mwaka huu.

Ujenzi wa shule hizo umegharimu zaidi ya sh.Bilioni 12.6 ambapo kwa shule ya Ihungo ujenzi huo unagharimu Sh.bilioni 10 huku Nyakato ikigharimu Sh.Bilioni 2.6.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa kamati hiyo Jasson Rweikiza akiwa na wajumbe wa kamati hiyo, amesema kuwa wameridhishwa na Mradi wa ujenzi wa shule hizo na kuitaka Wakala wa Majengo(TBA) kuhakikisha changamoto ndogondogo zilizopo zinafanyiwa kazi ikiwemo malalamiko ya vibarua kutolipwa fedha zao kwa wakati.

Ameitaka serikali kuhakikisha changamoto hizo zinaisha ili shule hizo ziweze kufunguliwa mapema kabla ya msimu wa masomo ya kidato cha tano kuanza mwaka huu.

Amesema wajibu wa Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa ni kutatua kero za Wananchi na kuleta maendeleo kwa Taifa.

Naye, Waziri Jafo wameishukuru kamati kwa kutembelea shule hizo sambamba na kuzishukuru Wizara za Elimu, Wizara ya Ujenzi, na Wizara ya Ulinzi kwa kuhakikisha ujenzi wa shule hizo unakamilika.

Hata hivyo Waziri Jafo ametoa angalizo kwa uongozi wa Mkoa wa Kagera kutoruhusu shule ya Ihungo kwa siku za usoni kugeuzwa kuwa Chuo Kikuu kwa kuwa imejengwa kwa lengo la Vijana wa kidato cha tano na sita.

Aidha, Waziri Jafo wameishukuru serikali ya Uingereza kwa msaada wa sh.Bilioni 10 zilizofanikisha ujenzi wa sekondari ya Ihungo.

No comments: