ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, May 9, 2018

UZINDUZI WA COPA UMISSETA SINGIDA WAFANA


 Wawakilishi wa shule za sekondari wakipokea vifaa vya michezo vilivyotolewa na kampuni ya Coca-Cola kutoka kwa Mkuu wa Mkoa, Dkt. Rehema Nchimbi
Mkuu wa mkoa wa singida, Dkt. Rehema Nchimbi, akifurahia zawadi ya mpira wa kufanyia mazoezi wakati wa hafla hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi, akijiandaa kupiga penati wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo. 

Mashindano ya Copa Umisseta ngazi ya mikoa yanaendelea ambapo yamezinduliwa mkoani Singida, katika uwanja wa Namfua ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa mkoa huo, Dk. Rehema Nchimbi, aliyemwakilisha Waziri wa TAMISEMI, Seleman Jafo.

Hafla ya uzinduzi huo wa michezo hiyo ambayo inadhaminiwa na kampuni ya Coca-Cola pia ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali mkoani humo, wadau wa michezo, walimu na wanafunzi wa shule za sekondari ambao walishiriki kucheza michezo mbalimbali.

Mkuu wa mkoa, Dkt. Rehema Nchimbi katika hotuba yake ya ufunguzi,aliishukuru kampuni ya Coca-Cola kwa kutoa udhamini kwa michezo hiyo na amewaasa washiriki ambao ni wanafunzi kuyatumia kuboresha afya na akili ili kuepuka kushiriki katika matendo ya kihalifu kama matumizi ya madawa ya kulevya na kutojihusisha na mapenzi kabla ya wakati.

Alisema mashindano hayo ni jukwaa kubwa la kuibua na kuendeleza vipaji vya michezo na Ushahidi wa suala hili upo kwa kuwa kuna wanamichezo wengi wanaotokea mkoani Singida ambao vipaji vyao viliibuliwa na Umisseta vilevile mkoa huo katika mashindano ya mwaka jana ulifanya vizuri katika ngazi ya kitaifa kwa kushika nafasi ya tatu.

Kwa upande wake, Meneja Mauzo wa bidhaa za Coca-Cola mkoani Singida, Joseph Simplis ,amesema Coca-Cola imekuwa ikidhamini mashindano haya kwa kipindi cha miaka 3 na lengo kubwa ni kuhakikisha inawashirikisha wanafunzi wengi zaidi nchini sambamba na kuibua na kukuza vipaji vya michezo.Aliwaasa wanafunzi wa Mtwara kuchangamkia fursa hii.

Katika kufanikisha michezo hii, kampuni ya Coca-Cola imekuwa ikitoa udhamini wa vifaa vya michezo ambapo imelenga kusambaza vifaa kwa shule za sekondari 4,000. Katika uzinduzi huo alikabidhi vifaa vya michezo vilivyotolewa na kampuni kwa wawakilishi wa shule mbalimbali mkoani humo.

Uzinduzi wa Copa Umisseta mkoani Singida ni wa tano kufanyika baada ya kufanyika katika mikoa ya Dodoma, Tanga, Mtwara na Zanzibar. Mashindano hayo ngazi ya kitaifa yatafanyika mwezi Juni mwaka huu mkoani Mwanza.

No comments: