ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, June 2, 2018

Sehemu ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki 2018-19: Diaspora

May 23, 2018- Dodoma Tanzania

KURATIBU NA KUSIMAMIA MASUALA YA WATANZANIA WAISHIO UGHAIBUNI

Link




106.     Mheshimiwa Spika, kwa kutambua Watanzania wanaoishi ughaibuni kama wadau muhimu wa maendeleo, Wizara yangu imeendelea kubuni mbinu mbalimbali za kuwashirikisha katika kuchangia maendeleo ya nchi. Moja ya mbinu hizo ni kuandaa makongamano ndani na nje ya nchi ambapo mwezi Agosti 2017, Wizara yangu kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliandaa Kongamano la Nne la Diaspora lililowakutanisha Watanzania zaidi ya 200 kutoka nchi mbalimbali na wadau wa maendeleo hapa nchini. Kupitia kongamano hilo, Diaspora walihimizwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa letu kwa kuhamasisha uwekezaji wa mitaji kutoka nje.
107.    Mheshimiwa Spika, mwezi Aprili 2018 lilifanyika kongamano lingine lililoandaliwa na Diaspora jijini Dallas Marekani, ambalo pamoja na masuala mengine, lililenga kutangaza vivutio vya utalii nchini pamoja na kuhamasisha wawekezaji kwenye sekta mbalimbali ikiwemo utalii.
108.        Mheshimiwa Spika, mchango wa Diaspora katika maendeleo ya nchi unajidhihirisha katika maeneo mbalimbali ya kiuchumi na kijamii. Yafuatayo ni baadhi ya maeneo hayo:
i.       Diaspora imenunua nyumba zenye thamani ya Shilingi bilioni 29.7 kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa ajili ya nyumba za makazi, ofisi, maeneo ya biashara na viwanja mbalimbali kati ya mwaka 2011 hadi 2017.
ii.      Takwimu za Benki Kuu ya Tanzania zinaonesha kuwa kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita 2013-2017, Diaspora kwa ujumla wao walituma nchini kiasi kisichopungua Dola za Marekani bilioni 2.3.
iii.     Timu ya madaktari wa kitanzania waishio Marekani kupitia taasisi ya afya, elimu na maendeleo (Head Inc.) ilitoa huduma ya afya bila malipo na vifaatiba katika hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar, vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja;
iv.     Jumuiya ya Watanzania nchini Marekani (DICOTA) iliandaa jukwaa la afya mwezi Novemba 2017 ambalo lilihudhuriwa na wataalam wa afya zaidi ya 130 kutoka Tanzania na Marekani ili kubadilishana ujuzi, uzoefu na kutathmini njia madhubuti za kuendeleza sekta ya afya nchini Tanzania. Juhudi hizi ziliwezesha kupatikana kwa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi na wafanyakazi zaidi ya 60 kutoka vyuo vikuu na hospitali nchini ikiwemo Chuo Kikuu cha Tiba KCMC, Hubert Kairuki, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili na hospitali ya Bugando.
v.      Aidha, Dkt. Frank Minja mtanzania mtaalam wa Radiolojia wa Chuo Kikuu cha Yale Marekani amesaidia kuimarisha mfumo wa teknolojia ya kisasa ya radiolojia katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
109.    Mheshimiwa Spika, wakati ambapo kipaumbele cha kitaifa ni viwanda, tunahitaji kufikiria ujuzi maalum walionao Watanzania wanaoishi katika Diaspora, na vile vile mchango wa kifedha ambao wanaweza kuchangia kutoka kwenye vyanzo vyao binafsi au kwa kushirikiana na raia wa nje, mabenki na taasisi nyingine za nje. Ili kuwezesha viwanda vyetu kuuza nje, tunahitaji kutambua, kupima na kupenya katika masoko mbalimbali ya kigeni. Watanzania walioishi nchi za kigeni na watoto wao wanaweza kuchangia zaidi kutokana na ujuzi wao kwa kupata masoko kwa kutumia ujuzi wao wa lugha za kigeni.
110.    Mheshimiwa Spika, watanzania wengi walio Diaspora wanachangia sana maendeleo ya kijamii na uchumi wa familia zao na Tanzania kwa ujumla, na wako tayari kushiriki katika jukumu kubwa la kujenga uchumi wa Taifa hili. Pengine tunahitaji kuwa na mfumo wa kisheria na sera ya kutoa huduma hiyo kwa uhalali na uhakika.

No comments: