ANGALIA LIVE NEWS

Friday, July 20, 2018

Kongamano la wadau sekta ya maji

Image result for water
Na. Abraham Nyantori - MAELEZO

Wadau wa Sekta ya Maji zaidi ya 200 wamehitimisha Kongamano la siku mbili leo na kuazimia kujenga mazingira ya yatakayoleta mwelekeo mpya wa kufanikisha sekta ya maji nchini haraka iwezekanavyo kwa serikali kupanua wigo wa kuihusisha sekta binafsi nchini huku wakiongozwa na Sera ya Taifa Maji ya mwaka 2002 na Mpango wa Pili Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP II)

Kongamano hilo lililoandaliwa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji ikihusisha Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imewahusisha, wakandarasi, washauri, wawekezaji na wadau wa maendeleo kwa maana ya kuleta mahusiano rasmi kama sekta ya umma na sekta binafsi nchini; Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Stella Manyanya, na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso wameshiriki Kongamano kwa siku zote mbili, Katibu Mkuu wa Maji na Umwagiliaji Profesa Kitilya Mkumbo kadhalika ameshiriki siku zote.

Kabla ya kuweka saini ya makubaliano wakati wa kufunga Kongamano hilo, jana washiriki waliangalia maeneo kadhaa ya kujenga uhusiano baina ya serikali na sekta binafsi, ambapo walibaini changamoto kadhaa zikiwemo kuimarisha menejimenti ya ugavi serikalini pia kuhakikisha manunuzi toka viwanda vilivyoko nchini yanapewa kipaumbele; kukutana mara kwa mara ili kujenga mawasiliano ya karibu katika ngazi zote katika sekta.

Katika makubaliano hayo, yamo masuala ya kuimarisha mahusiano na wadau wa maendeleo ili kuimarisha tekenolojia na rasrimali klatika sekta ya maji na maji taka na kamati maalumu imeandaliwa kuandaa mwendelezo wa andiko la jinsi ya utekelezaji wa dhamira hiyo ambayo awali Profesa Mkumbo alisema dhamira ya serikali kuongeza wigo wa kuishirikisha sekta binafsi katika Nyanja zote ni moja ya agenda muhimu katika andiko la WSDP II.

Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya, Naibu Waziri wa Maji na Umwagilaiji, Jumaa Aweso, na Mwakilishi wa Sekta Binafsi, Bw. Louis Akaro wameweka saini Azimio hilo na kusisitiza kuwepo na uzalendo wa kuona umuhimu wa kuliendeleza Taifa, “ Sisi serikali tuna wajibu wa kuhakikisha wananchi wanapata maji safi, salama na yakutosha bila kufikiria gharama, wewe mfanyabiashara unawaza fedha, lakini sote tuwe na utashi wa kitaifa kwa jamii yetu” alisistiza Profesa Mkumbo.

Ili kufanikisha mahusiano ya sekta binafsi na serikali pande zote mbili lazima zijenga tabia ya kujulishana kila jambo, akasema , “Mshauri anapoandaa pendekezo la mradi asifanye maamuzi ya ushauri wa mitaani kuwa bidhaa zinazozalishwa nchini hazifai, manunuzi ni muhimu yaanzie toka viwanda vyetu na wawekezaji nchini na wizara yetu italisimamia hilo ili wawekezaji wan je na ndani wawe na uhakika wa masoko”

Akifunga Kongamano hilo kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa, Naibu wake Jumaa Aweso, amesisitiza kwa kila kundi katika sekta; wakandarasi; washauri; wagavi na menejimenti za ufundi kutambua umuhimu wa kutimiza wajibu kwa ueledi ili kila jambo linalopangwa litimizike pasipo kukwama, akasema, “kila mradi unaoanzishwa, uandaliwe kwa ufanisi na usikwame kwa visingizio vya makosa ya nyuma na hivyo basi kila mradi ukamilike kwa wakati.”

No comments: