ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 30, 2018

Rais Magufuli aikaribisha Dunia Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Mabalozi wa nchi mbalimbali pamoja na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa maara baada ya kuwakabidhi Hati za Viwanja vilivyopo Makao makuu ya Serikali mkoani Dodoma kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za Balozi pamoja na Mashirika hayo ya kimataifa. 

Na. Immaculate Makilika- MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekabidhi hati 67 za viwanja kwa Mabalozi na Mashirika ya Kimataifa kwa ajili ya kujenga makazi na matumizi mbalimbali.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi hati hizo leo Ikulu jijini Dar es salaam, Rais Magufuli

Amewapongeza viongozi wa Mkoa wa Dodoma kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kukamilisha zoezi la kuwapatia viwanja mabalozi, ambapo amesema kuwa gharama zote za umiliki wa ardhi na hati za hizo za viwanja 67 ambavyo wamepewa Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini Tanzania pamoja na Mashirika ya Kimataifa, zimelipwa na Serikali.

“Hati miliki hizi zimetolewa bure ili kuonesha kuwa tunathamini urafiki wetu na nchi mnazoziwakilisha na tungependa kudumisha urafiki wetu”.Alisema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli amesema kuwa ameagiza kutangazwa kwa tenda ya kujenga Uwanja mkubwa wa ndege wa Kimataifa wa Msalato wenye urefu wa kilomita 3 na ujenzi huo uanze mara moja, ikiwa ni katika jitihada za kuboresha mji wa Dodoma kwa ajili ya kubebea taswira ya kuwa makao makuu ya nchi.

Huku akisisitiza “tunataka kujenga Tanzania mpya yenye uchumi mzuri na maendeleo makubwa kupitia ushirikiano na nchi za nje na sekta binafsi”.

Kwa upande wake, Waziri Wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga amesema kuwa mabalozi wengi wameitikia wito wa kuhamia Jijini Dodoma.

Waziri Mahiga amesema kuwa kipindi hiki ambacho wanajiandaa kuhamia jijini Dodoma, anawahakikishia mabalozi wote kuwa mawasiliano kati yao na Wizara ya Mambo ya Nje yataendelea kama kawaida wakati wakiendelea na mchakato wa kuhamia jijini Dodoma.

Naye, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesisitiza kuwa Serikali ipo tayari kutekeleza maombi ya mabalozi wanaohitaji ziada ya ardhi Jijini Dodoma, licha ya serikali kuwapatia ekari tano kwa kila Balozi na Mashirika ya Kimataifa.

Vile vile, Balozi wa Rwanda nchini Tanzania Eugene Kayhura, kwa niaba ya Mabalozi waliopo nchini ameishukuru serikali ya Tanzania kwa kuwakabidhi hati miliki za viwanja hivyo vilivyopo Jijini Dodoma.

“Tunaahidi kuziwasilisha hati hizi kwenye nchi zetu kwa ajili ya hatua za utekelezaji” amesema Balozi Kayhura.

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge amewahakikishia Mabalozi na Mashirika ya Kimataifa kuwa Dodoma ni salama, wamejipanga vizuri kuhakikisha hakuna matukio ya uvunjifu wa amani.

Akitaja mikakati iliyowekwa katika kuendeleza jiji la Dodoma amesema kuwa “kwa sasa tunauwezo wa kuzalishaji wa maji kwa siku lita milioni 61.5, huku mahitaji yakiwa ni lita milioni 46, umeme megawati 48 kwa siku, mahitaji ni megawati 20 huku jitihada za kuongeza uzalishaji wa umeme zikiendelea ili kuendana na mahitaji ya baadae”.

Aidha, ameongeza kuwa “Jiji la Dodoma lina hospitali 6 ikiwemo hospitali kubwa ya kisasa ya Benjamin Mkapa yenye vipimo vya kisasa ikiwemo CT-SCAN na MRI, Agosti mwaka huu itafunguliwa shule ya Kimataifa itakayotumia mtaala wa Cambridge na wawekezaji wengine wanakaribishwa kuwekeza katika elimu, amesema Dkt. Mahenge

Jiji la hilo la Dodoma linatarajiwa kuwajengwa stendi za kisasa, ambapo Serikali imetoa Bilioni 77.8 kwa ajili ya ujenzi wa stendi ya kisasa ya mabasi itakayochukua mabasi 250 kwa wakati mmoja na ujenzi huo utakamilika Oktoba 2019.

Mwisho.

No comments: