ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 11, 2018

KWENYE UHUSIANO KUNA MAZOEZI NA MECHI, UPO WAPI ?

UNAPOBAHATIKA kuingia kwenye uhusiano bila kupitia sarakasi za kutosha mshukuru Mungu. Wengi sana wamejikuta wakiangua vilio kwa kuteswa na mapenzi. Mapenzi yanaumiza. Utalia na kusaga meno pindi tu utakapokuwa kwenye uhusiano na mtu ambaye si sahihi. Atakufanyia vituko, atakufanyia kila hila ilimradi tu sababu hana mpango wa kuwa na wewe.

Ndio maana siku zote nimekuwa nikisisitiza katika makala zangu mbalimbali, hakikisha unaingia kwenye uhusiano na mtu ambaye ni sahihi. Usikurupuke, msome mtu kabla ya kuruhusu moyo wako uzame penzini maana ukishazama, ni vigumu sana kutoka. Zaidi utabaki unalia tu peke yako kama mtoto pale mwenzako atakapokuacha solemba.

Dunia ya leo imejaa matapeli wa mapenzi wenye mioyo migumu. Mtu anaingia kwenye uhusiano na wewe, anakujaza maneno matamu ya kukufanya uamini kwamba upo peke yako na hakuna mwingine kumbe si kweli. Moyoni anakuwa na lake jambo, anazuga tu kama anakupenda kumbe akili yake haipo kwako. Anakufanya wewe kama uwanja wa mazoezi, mechi anajua atakuja kucheza na nani.

Bahati mbaya sana mapenzi huwa yanakuja na upofu fulani, wakati mwingine unapokuwa kwenye uhusiano unakuwa kama kipofu. Mtu una akili, umesoma na unajua kung’amua mazuri na mabaya lakini mwisho wa siku mapenzi yanakupeleka yanakuziba na kukufanya usione mabaya unayotendewa na mwenzako.

Watu wa aina hii wapo wengi, kinachotakiwa ni kuwa makini. Kwa nini ukubali kufanywa uwanja wa mazoezi? Utakuwa uwanja wa mazoezi mpaka lini? Mkatae mtu mwenye mlengo huo. Kwa kutumia utashi uliopewa na Mungu, fanya utafiti wa kina kabla ya kuingia kwenye uhusiano na mtu.

Huyo mtu ana mapenzi ya dhati na wewe? Jiulize je ana hofu ya Mungu? Sio kigeugeu? Hakutumii kwa maslahi fulani labda fedha, uzuri wa sura na mambo mengine ya anasa? Wapo wengi ambao wanaingia kwenye uhusiano kwa maslahi fulani. Watu hao ni hatari sana hivyo ni vyema kujiridhisha kabla ya kuruhusu moyo wako kuzama penzini.

Akili yako ina uwezo mpana sana wa kupambanua mambo endapo tu utaamua kuishughulisha. Kataa kupelekwa puta na mapenzi hadi pale utakapokuwa umejiridhisha vya kutosha. Ukishajiridhisha kwamba upo na mtu sahihi basi sasa unaweza kuzama penzini maana una uhakika uliye naye ni sahihi.

Tapeli wa mapenzi ni rahisi sana kumgundua maana waswahili wanasema siku zote njia ya muongo ni fupi. Ataigiza mwezi mmoja, miwili lakini hawezi kuigiza mwaka mmoja au miwili. Utamgundua tu kwamba huyu mtu kweli mpo pamoja safarini au ana mpango wake wa siri.

Ukigundua ana mpango wa siri, muepuke. Mshukuru Mungu kwa kubaini ukweli na unachopaswa kufanya ni kukaa naye mbali. Mruhusu aende na wala wewe usiumie.

Chukulia safari mliyopita ni kama mazoezi na mechi inakuja. Muda wako upo, kupitia safari yake hiyo utakuwa pia umejifunza kitu maishani. Usiwachukie watu wa jinsia tofauti na yako ukiamini wote ni kama huyo uliyekuwa naye. Huyo hakuwa wa kwako. Mtu sahihi maishani mwaka yupo mahali, muda wake utafika na utasahau yote uliyopitia.

Utampata mwenza ambaye kweli amezaliwa kwa ajili yako, atakupenda, atakujali na kukuthamini. Utampata tu kwa kujiridhisha, kumpima na mwisho wa siku Mungu atasimama na wewe. Tukutane wiki ijayo, unaweza kunifuata kwenye mitandao yangu ya kijamii. Instagram na Facebook natumia Erick Evarist, Twitter natumia ENangale.

GPL

No comments: