ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, September 20, 2018

UGONJWA WA DOGO JANJA UWOYA ATAJWA

UKURASA wa maisha ya ndoa ya Dogo Janja na Irene Uwoya uko wazi, unasomeka mengi wanayoyapitia mastaa hao; kubwa kabisa ni kwamba hawaelewani. Uwoya alipoposti picha mitandaoni hivi karibuni kuonesha kwamba yuko Dubai anakula bata; watu wakasema Dogo Janja emeshaporwa mke na wanjanja zaidi yake. Jibu la Uwoya kuhusu hilo lilikuwa ni kutofuatwafuatwa na wasioila pilipili ya ndoa yake. Wachagiza mada mitandaoni lao lilikuwa ni kumpa pole Dogo Janja

“Dogo angalia huyo mwanamke atakutoa uhai.”Hivi karibuni mwanamuziki huyo alipougua ghafla na kukimbizwa hospitali kisha kuposti picha akiwa amelazwa huku anapumulia mashine; watu wakarudia tena kumuonya kwa kumwambia aangalie Irene Uwoya asije akamuua kwa presha. Kama kawaida yake Uwoya alipoinusa michapo ya mitandaoni akaibuka na posti hii: “Vyovyote unavyosikia kuhusu mimi amini, sina tena muda wa kujielezea mwenyewe, pia unaweza kuongezea baadhi ya vitu kama unataka.”

Hapo sasa baadhi ya watu wakaanza kumtolea povu mrembo huyo kwa kuhoji ni mke wa namna gani ambaye anapata muda wa kuposti vitu vingine hadi picha za ajabuajabu lakini anashindwa kumpa pole mumewe kwa kuumwa. Ukifuatilia mlolongo wa maisha ya Uwoya na Dogo Janja utagundua kuwa; Uwoya ana wakati mgumu zaidi kwenye ndoa hiyo kuliko hata mumewe ila mwenyewe hajajijua.

Angelikuwa anafahamu hilo angeliongeza umakini zaidi wa kuilinda ndoa kwa ajili ya kuiponya nafsi yake. La hawezi kufanya hivyo; angeamua moja, kwamba ayamwage maji ya ndoa kama alivyofanya kwa mume wake wa kwanza na kuwa ‘single’ pengine ingemsaidia zaidi kuliko iivyo hivi sasa. Pamoja na mengine; chachu inayochachua donge la ndoa ya Uwoya na Dogo Janja kwa mtazamo wa wengi ni umri wao kupishana, wengi wanamtazama mrembo huyo kuwa ni mkubwa mno kwa mumewe.

Huko majuu suala la mwanamke kumzidi mume au mwanaume kuoa mwanamke mkubwa zaidi yake ni jambo la kawaida, lakini desturi za Kibongo zinakataa; anayeolewa na ‘Serengeti Boy’ ni kama kucheza na mtoto; akilia utalaumiwa umempiga hata kama mchanga umemwingia machoni. Ndicho kinachotokea kwa Uwoya, kila Dogo Janja akilia watu wanamlaumu kuwa atamuua kwa presha, mara oooh ni mfupa uliomshinda fisi Dogo Janja hatauweza na mambo mengine meeeengi.

Kama nilivyosema; Uwoya anatakiwa kujitazama upya na kuamua kuchagua moja acheze na mtoto vizuri ili asilie au amlejeshe kwa mama yake akanyonye. Inawezekana Uwoya anashindwa kutangaza kuwa hamtaki mumewe kwa sababu anaogopa wapiga miruzi, lakini lipi jema kuishi umepiga magoti au kufa umesimama? Leo sitasema mengi ila naomba sana yasitokee mabaya!

Makala: Mwandishi Wetu, Amani GPL

No comments: