Jengo la Halmashauri ya Pangani muonekano wake ambalo
mpaka sasa halijakamilika
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Suleiman Jafo amemsimamisha kazi Mkandarasi wa Kampuni ya Wesons Tanzania (ltd) ya Jijini Dar Mhandisi Emamnuel Norbert kwa kutokumaliza mradi Shilingi Milioni 641 wa Jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Pangani na kumtaka Mkuu wa Wilaya hiyo kushirikiana na mamlaka husika kupata mkandarasi mpya.
Jafo alichukua maamuzi hayo wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo baada ya kutembelea baadhi ya miradi na kukuta ubadhilifu wa fedha za Serikali uliopelekea baadhi ya miradi kutokukamilikia kwa wakati.
Alisema hakuna sababu kwa mkandarasi huyo kuendelea na mradi huo kutokana na kukosa uwezo wa kujenga jengo hilo jambo ambalo linaweza kuitia zaidi hasara serikali kwa kuendelea kupoteza fedha kwa ajili ya kuilipa kampuni isiyokuwa na uwezo.
“Ipo miradi mingi hapa nchini na mienendo yake iko vizuri na mingi imemalizika na nimekagua mwenyewe leo mradi huu wa jengo la Halmashauri tangu mwaka jana hapa hakuna mkandarasi ni ujanja ujanja tu muondoeni na tafuteni mkandari mwengine”alisema jafo.
Waziri Jafo alitaka kupewa maelezo toka kwa mshauri mwelekezi wa mradi toka kampuni ya Y &P Architects(T)ltd ya Jiji Dar Benjamin Kasiga alisema hatua zimekwisha anza kuchukuliwa ikiwa pamoja na kuanza kutafutwa mkandarasi mwenye uwezo.
Katika hatua nyingine Waziri Jafo aliitaka ofisi ya Mkuu wa Wilayani Pangani kwa kushirikiana na Takukuru kuwabaini wale waliohusika na ubadhilifu wa shilingi Milioni 150 za ujenzi wa mabweni mawili ya shule ya sekondari ya Tongani iliyopo kata ya Mkaramo ambayo hayajamilika na hatua kali zichukuliwe dhidi yao.
Alisema Serikali ilitoa kiasi cha shilingi Milioni 259 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa manne,mabweni mawili na matundu ya vyoo 11 mradi ambao utekelezaji wake ni mbovu kuliko matarajio huku mabweni hayo yakiwa bado kukamilika tangu machi mwaka jana.
“Haiwezekani Wilaya hiyo ishindwe kutekeleza miradi hiyo huku watendaji na wasimamizi wakiangalia bila ya kuchukua hatua zozote za kisheria na ni sababu iliyopeleka Halmashauri hiyo kupata hati chafu.” Alisema Jafo.
Waziri Jafo alisema miradi yote hiyo inachangamoto ya utekelezaji wake huku madarasa yakiwa na nyufa,vyoo havina milango huku wataalam wa Halmashuari wakiangalia miradi hiyo ikijengwa chini ya kiwango.
Mhandisi wa Halmashauri hiyo Malulu Martin alisema sababu za kuta hizo za madarasa kupata nyufa zinatokana na aina ya ardhi iliyopo katika eneo hilo ni la mchanga na kusababisha madarasa hayo kupata nyufa.
Jafo alionekana kughadhibika baada ya kumsikia mhandisi huyo alipotoa sababu isiyokuwa ya msingi iliyopeleka kuta za madarasa kupata nyufa na kusema huna sababu ya kuwa mhandisi ikiwa hujui namna ya kukabiliana na tatizo hilo la udongo.
Awali akizungumzia changamoto za miradi hiyo Mkuu wa Wilaya hiyo Zainab Abdallah alisema alifanya ziara ya mwezi mzima ili kujionea mwenendo wa miradi hiyo ambayo haikuwa katika hali mzuri. Abdallah alimueleza Waziri Jafo kuhusiana na swala la mabweni ya shule ya Tongani kuwa alikwisha wapa maelekezo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa wilayani humo (Takukuru) ili waweze kuchunguza juu ya ubadilifu wa fedha hizo na hatua kali zitaendelea kuchukuliwa kwa watakaohusika.
No comments:
Post a Comment