Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikizindua Rasmi Kituo cha Watu wenye Ulemavu wa Jimbo la Shaurimoyo kilichojengwa pembezoni mwa Skuli ya Sekondari ya Ufundi Mikunguni Mjini Zanzibar. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mheshimiwa Ayoub Mohamed Mahmoud.
Blozi Seif na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud wakishangiria kwa kupiga kofi mara baada ya akikizindua Rasmi Kituo cha Watu wenye Ulemavu wa Jimbo la Shaurimoyo.
Balozi Seif akiangalia na kufurahia bidhaa zinazozalishwa na Watu wenye Ulemavu wa Jimbo la Shaurimoyo ndani ya Kituo kipwa alichokizindua rasmi.
Mjumbe wa Kamati ya Mradi wa Kituo cha Watu wenye ulemavu cha Jimbo la Shaurimoyo Bibi Mrashi Mikidadi akiwasilisha Risala kwenye hafla ya uziduzi wa Kituo chao cha kazi za ujasiri amali pamoja na Ofisi.
Balozi Seif akizungumza na Wananchi wa Jimbo la Shaurimoyo katika hafla ya uziduzi wa Kituo chao cha kazi za ujasiri amali pamoja na Ofisi hapo pembezoni mwa Skuli ya Sekondari ya Ufundi Mikunguni.
Balozi Seif akimkabidhi Baskeli Mtoto mwenyeulemavu wa Jimbo la Shaurimoyo Feisal Mbarouk kwenye hafla ya uziduzi wa Kituo chao cha kazi za ujasiri amali pamoja na Ofisi hapo Mikunguni.
- Mtoto Lutfia Mohamed ambae ni mlemavu akifurahia Baskeli mpya aliyokabidhiwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi zilizotolewa na Wafadhili mbali mbali.
Fundi Seremala wa Kituo cha Watu wenye ulemavu cha Jimbo la Shaurimoyo Bwana Juma Abdulaah Juma akipokea Baskeli yake itakayomsaidia katika harakati zake za Kimaisha. Picha na – OMPR –ZNZ.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati umefika kwa Serikali Kuu kwa kushirikiana na Taasisi na Mashirika megine ya Kitaifa na Kimataifa kujenga Kituo cha Taifa kitakacholenga kuwahudumia Watu wenye ulemavu katika kuwajengea nguvu na maarifa ya kuendelea kujitegemea Kimaisha.
Alisema Ulimwengu wa sasa umebadilika kwa kubeba harakati nyingi zinazoibua matukio mbalimbali yanayosababisa Jamii kukumbwa na ajali tofauti katokana na kasi ya maisha na hatimae kuzalisha Walemavu wanaohitaji huduma za matunzo na maarifa mengine ya Kimaisha.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati wa hafla maalum ya kuzindua rasmi Kituo cha Jumuiya ya Watu wenye Ulemavu cha Jimbo la Shaurimoyo kiliopo pembezoni mwa Skuli ya Sekondari ya Ufundi Mikunguni Mjini Zanzibar.
Alisema tabia ya kuwatenga Watu wenye Ulemavu haipendezi na nidhambi jambo ambalo halikubaliki katika Jamii yoyote ile. Hivyo aliwahimiza wahusika hao wasikubali kukata tamaa katika kupigania haki zao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliushukuru Uongozi wa Kampuni ya Peny Royal na Kumpongeza Mwakilishi wa Jimbo la Shaurimoyo kwa jitihada zao zilizopelekea kujengwa kw kituo hicho muhimu kwa Watu wenye mahitaji Maalum.
Balozi Seif alifarajika kuona kwamba Ujenzi wa Kituo hicho umelenga kuwajengea Uwezo na maarifa Watu wenye Ulemavu wa Jimbo la Shaurimoyo ili wawe Wajasiri Amali watakaokuwa na nguvu za kujiendesha wenyewe Kimaisha.
Akisoma Risala ya Wanajumiya hiyo ya Watu wenye Ulemavu ya Jimbo la Shaurioyo Mjumbe wa Kamati ya Mradi wa Kituo hicho Bibi Mrashi Mikidadi alisema Jengo hilo limebuniwa kutokana na changamoto kubwa iliyokuwa ikiwakabili ya kukodi sehemu za kuendeshea Kazi zao.
Bibi Mrashi alisema uwepo wa Kituo hicho hivi za utatoa fursa na afueni kwa Wanajumiya hiyo kuendelea na shughuli zao kwa Amani, faraja na utulivu utakaowaongezea nguvu na ari ya kufanikisha malengo yao.
Akitoa salamu katika hafla hiyo Mwakilishi wa Kampuni ya Peny Royal Bwana Brian Tomsom ambayo ndio iliyofadhili ujenzi wa Kituo hicho alisema Uongozi wa Taasisi hiyo ya Uwekezaji utaendelea kusaidia huduma za Kijamii kama ulivyoainisha katika muelekeo wake wa Uwekezaji.
Bwana Brian alisema mkazo zaidi utawekwa katika kuwasaidia Wanawake na Watoto wenye mahitaji Maalum na kwa kuanzia imepanga kuwafungulia Bima ya Afya Watoto wapatao 50 hapa Zanzibar.
Naye Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud akimkaribisha Mgeni rasmi kwenye hafla hiyo alitahadharisha kwa Maskani kwa lugha nyengine Vijiwe vitakavyoonyesha dalili ya kutaka kuwasumbua Wanajumuiya hiyo vinapaswa kuondoshwa mara moja na Uongozi wa Shehia.
Mh. Ayoub alisema hakuna Mtu wala Kikundi chochote kinachoweza kuitisha Serikali kwa kusimama juu ya sheria jambo ambalo aliahidi kufanya ziara za kushtukizia katika maeneo hayo ili kujiridhisha na uwepo wa salama na Amani utakaowapa faraja Wananchi wa maeneo hayo kuendelea na harakati zao kama kawaida.
Alisisitiza umuhimu wa kila jambo la Kijamii kufanywa kwa kuzingatia Sheria na Utaratibu ili masuala yote yanayoihusu Jamii husika yaende bila ya vikwazo au pingamizi za Kisheria.
Katika Kuunga mkono harakati hizo wa Jumuiya ya Watu wenye ulemavu Jimbo la Shaurimoyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliahidi kutoa Mchango wa Shilingi Milioni 2,000,000/- kusaidia Mfuko wa Kituo hicho, Mkuu wa Mkoa Mjini akaahidi kuchangia Shilingi Milioni 1,000,000/-.
Wengine walioahidi kuchangia ni Chama cha Mapinduzi Afisi Kuu Shilingi Laki 550,000/-, Mwakilishi wa Jimbo la Shaurimoyo Mh. Hamza Hassan Juma Shilingi Laki 500,000/- na CCM Mkoa Mjini Shilingi Laki 400,000/-.
Katika Hafla hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikabidhi msaada wa Baskeli za Watu wenye ulemavu wa Jimbo hilo kutoka kwa Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan, Kampuni ya Peny Royal, Uongozi wa CCM Mkoa Mjini pamoja na Mwakilishi wa Jimbo la Shaurimoyo.
Jengo la Kituo cha Watu wenye Ulemavu cha Jimbo la Shaurimoyo kimegharimu jumla ya shilingi za Kitanzania Milioni28,000,000/- hadi kukamilika kwake rasmi.
No comments:
Post a Comment