Advertisements

Wednesday, October 17, 2018

JITIHADA ZA SERIKALI NA SEKTA BINAFSI KUTOKOMEZA KIFUA KIKUU

Na. Immaculate Makilika – MAELEZO

UGONJWA wa kifua kikuu ni kati ya magonjwa matatu ikiwemo malaria na ukimwi yanayotokea sana kwa watu masikini duniani, ambapo asilimia 98 ya wagonjwa wanapatikana katika nchi zinazoendelea.

Tanzania ni ya 15 kati ya nchi 22 ambazo zimeathiriwa sana na ugonjwa huu, ambapo takwimu zinaonesha ya kuwa, ambapo takribani asilimia kati ya 30 na 50 ya watanzania wote tayari wameambukizwa Kifua kikuu.

Takwimu za Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto zinaonyesha kuwa kwa mwaka 2016 jumla ya watu 65,908 waligundulika na kuwekwa katika matibabu ya kifuu, ambapo asilimia 90 ya waliopata matibabu ya TB walipona.

Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na tatizo la Kifua Kikuu nchini ikiwemo kuimarisha huduma za uchunguzi na ugunduzi wa kifua kikuu katika vituo vya afya.

, Ili kuongeza msukumo wa mapambano na ugonjwa huo, Serikali imeendelea kubuni mikakati mbalimbali ikiwemo kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo sekta binafsi ili kuleta mabadiliko na tija katika hatua muhimu ya kutokomeza TB.

Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2018/19, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasema katika kukabilina na ugonjwa wa kifua kikuu nchini, mwaka 2017/18 Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ilinunua na kusambaza mashine za “genexpert” 189 ikilinganishwa na mashine 66 zilizokuwepo mwaka 2015.

Anaongeza kuwa mashine hizo zilisaidia katika kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za ugunduzi wa ugonjwa wa kifua kikuu kwa kutumia vipimo vya vinasaba.

“Malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano katika sekta ya Afya ni kushirikiana na sekta binafsi katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa kifua kikuu hasa kuongeza idadi ya wagonjwa wa TB wanaogunduliwa kutoka asilimia 40 hadi asilimia 70 mwaka 2020” anasema Waziri Ummy.

Kwa mujibu wa Waziri Ummy anasema mashine za genexpert zina uwezo wa kupima usugu wa dawa za kifua kikuu na wakati huo huo zinatumika katika kupima makohozi, na hivyo kugundua kifua kikuu sugu kwa urahisi zaidi.

Waziri Ummy, anasema kuwa mashine hizo zimesambazwa katika hospitali zote za rufaa za kanda, mikoa, wilaya na baadhi ya vituo vikubwa vya afya nchini pamoja na hospitali binafsi tano (5) zilizopo jijini Dar es salaam ambazo ni Aga Khan, Hubert Kairuki, Regency Medical Center, TMJ na Hindul Mandal.

Akifafanua zaidi, Waziri Ummy anasema ushirikishwaji huo wa sekta binafsi kutambua wagonjwa wa kifua kikuu umeonesha ongezeko la wagonjwa wa kifua kikuu wanaoibuliwa na sekta binafsi kutoka wagonjwa 3,476 mwaka 2014 hadi wagonjwa 7281 mwaka 2017 ambao ni sawa na asilimia 10.4 waliogunduliwa na sekta binafsi.

Akifafanua zaidi anasema kuwa kipindi cha mwaka 2017 hadi Machi 2018 Serikali imeongeza vituo 41 na kufanya jumla ya vitu vinavyotoa huduma hiyo kufikia vituo 63 ikilingalishwa na kituo kimoja cha hospitali Maalum ya Kibong‟oto mwaka kilichokuwepo mwaka 2015.

Sekta binafsi ni wadau muhimu wanaopaswa kushirikiana kwa karibu zaidi na Serikali katika kutambua, kudhibiti na kutokomeza ugonjwa wa TB sambamba na kuongeza wigo wa huduma za matibabu ya wagonjwa wa kifua kikuu sugu nchini.

MWISHO

No comments: