ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 17, 2018

Kamera tukio la kutekwa Mo Dewji mjadala mzito

By Waandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kitendawili cha kutekwa kwa mfanyabiashara tajiri zaidi miongoni mwa vijana Afrika, Mohammed Dewji (43), kinaweza tu kuteguliwa kwa kujua sababu za kamera za usalama (CCTV) katika hoteli aliyonyakuliwa, kutochukua tukio hilo vizuri.

Wakati Taifa lipo katika sintofahamu kuhusu mazingira yanayozunguka utekaji huo na nia ya watekaji, suala la kushindwa kwa kamera za usalama za hoteli hiyo kusaidia kutoa majibu limeendelea kuwa mjadala kwa wengi.

Wakati baadhi ya watu wakihoji sababu za kamera hizo kutofanya kazi au Jeshi la Polisi kutoomba ushirikiano kutoka majirani katika eneo hilo ambalo pia wanaishi viongozi wa nchi, Mwananchi imeongea na wahusika ambao baadhi wamesema chombo hicho cha dola kimeshaangalia kamera za majengo jirani, lakini bado suala hilo linaonekana kuwa kitendawili.

Mo alitekwa saa 11:30 alfajiri ya Alhamisi iliyopita akiwa Hoteli ya Colosseum, eneo la Oysterbay jijini Dar es Salaam katika uhalifu ambao polisi wanasema ulifanywa na Wazungu wawili.

Tangu siku hiyo, hakuna taarifa iliyotolewa ama na mamlaka za upelelezi au ndugu zinazoonyesha matumaini ya kupatikana kwa mbunge huyo wa zamani wa Singida Mjini na mwekezaji katika klabu ya Simba.

Familia yake imetangaza dau la Sh1 bilioni kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazowezesha kupatikana kwa ndugu yao.

Polisi waliwakamata na kuwahoji watu 26 kuhusiana na tukio hilo, lakini jana walisema 19 kati yao wameachiwa kwa dhamana. Chombo hicho cha dola kimesema kinafanya msako katika maeneo muhimu, kama ukanda wa Bahari ya Hindi, katika hoteli kubwa na kwingine ikiwamo mipaka ya nchi.

Hata hivyo, swali kubwa ni kwa kiasi gani kamera za CCTV ambazo zimetapakaa katika eneo la tukio na nyumba za maeneo ya jirani zinatumika kusaidia kuwabaini watekaji na mahali walikotokomea.

Mara baada ya kuanza kusambaa kwa habari ya kutekwa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliwaambia waandishi wa habari kuwa taarifa za awali zinaonyesha watekaji walikuwa ni Wazungu.

Hakueleza kama Wazungu hao walitambuliwa kwa kamera za usalama za hoteli hiyo au mashahidi wengine.

“Leo hii kungekuwa na surveillance camera (camera za ulinzi) jeshi lisingepata taabu kutumia nguvu kubwa kumfuatilia mtu. Za huku (kamera za CCTV) ndani tayari zimetuonyesha nini kilichopo, lakini barabarani? Je? wanapopita?” alihoji.

Muda mfupi baadaye kamanda wa polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema akiwa eneo la tukio kuwa waliomteka Mo walitumia gari aina ya Toyota Surf, lakini hakuweka sawa kama gari hilo lilitambulika kwa kutumia kamera au mashahidi.

Hata hivyo, kauli zake zilizofuata ziliashiria kuwa hawatazitegemea sana kamera za hoteli hiyo kuwabaini watekaji.

“Haiwezekani mahali hapa watu wanaingia kirahisi namna hii, CCTV Camera haionyeshi ni wapi walipoingilia. Pengine yalikuwa ni maandalizi ya kufanya huu utekaji,” alisema Mambosasa.

Siku moja baadaye, Mambosasa aliliambia Mwananchi kuwa kamera za usalama za hotelini hapo hazitoi mtiririko mzima wa tukio kwa kuwa hazisomi.

“Bado tunaendelea na upelelezi. Dada (mwandishi) kama kitu hakionekani huwezi kumuona mtu, huwezi kujua gari ni ya aina gani, ndicho kitu ambacho hatujakiona, kamera hazisomi,” alisema.

Alisema pia wanapata taarifa kutoka kwa watu walioona na kushuhudia tukio hilo kufanya uchunguzi wa kuwapata watekaji.

Kauli ya Mambosasa inaibua maswali ni wakati gani na ni nani alizichezea kamera katika hoteli ya Colosseum kiasi cha kushindwa kuonyesha mtiririko wa matukio.

CCTV zimetapakaa njia nzima

Hata hivyo uchunguzi uliofanywa na Mwananchi umebaini kuwa gari lililotumiwa na watekaji lilipita barabara iliyozungukwa na kamera za usalama za nje.

Kuna umbali wa kilomita moja tu kutoka njiapanda ya Barabara ya Ali Hassan Mwinyi na Haile Selassie hadi hotelini hapo kabla ya kuendelea hadi klabu maarufu ya zamani ya Maisha.

Upande wa kulia wa barabara hiyo ya Haile Selassie ukitokea makutano hayo umepakana na makazi, Shule ya Msingi ya Oysterbay na jengo kubwa la makazi linalopangishwa na Aga Khan Foundation. Pia kuna makazi ya waziri mkuu wa zamani yanayotazamana na hoteli ya Colosseum.

Upande wa kushoto wa barabara hiyo ukitokea njiapanda, kuna Kanisa la Mtakatifu Petro, makazi ya Balozi wa Baba Mtakatifu na makazi ya Makamu wa Rais, kama mita 200 kabla ya kufika hotelini.

Ukielekea Masaki, upande wa kushoto kuna jengo la biashara la Saphire Heights, ubalozi wa Nigeria, karakana ya ubalozi wa Uingereza kabla ya kufika Maisha Club.

Ufuatiliaji wetu umebaini kuna nyumba zaidi ya nne upande wa kushoto kutoka Colesseum kuelekea Masaki ambako watekaji wanaelezwa kuelekea, zimefungwa kamera zinazoweza kunasa picha za magari yanayopita Haile Selasie.

Mlinzi katika nyumba moja ya makazi karibu na hoteli hiyo aliyeomba kutotajwa jina, anasema kamera zilizofungwa katika nyumba hiyo zina uwezo wa kuonyesha magari yanayopita barabarani, kuanzia hotelini hapo (Colosseum) hadi Maisha Club.

Kamera iliyonasa gari la watekaji

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, kamera za hotelini hapo zilionekana kuzibwa upande mmoja siku ya tukio na kusababisha kukamatwa kwa baadhi ya wafanyakazi na walinzi.

Hata hivyo, chanzo cha kuaminika kimeliambia Mwananchi kuwa mara baada ya tukio hilo, polisi walifika katika jengo la makazi la kupangisha upande wa pili wa hoteli hiyo na kukusanya baadhi ya taarifa, kama za kutambua gari la wahalifu.

“Polisi walikuja hapa siku hiyo hiyo ya tukio. Mimi nilikuwa zamu hapa kazini. Walipoona kamera kule zimezibwa wakaja kuangalia za hapa, kisha wakaondoka,” alieleza mtoa taarifa wetu kutoka moja ya majengo jirani.

Jengo hilo liko upande wa kulia kutokea Kanisa la Mtakatifu Petro, wastani wa mita 100 kabla ya kufika hoteli ya Colosseum.

Alipoulizwa na Mwananchi kuhusu kamera za usalama za majengo jirani jana jioni, Mambosasa alisema walitumia kamera za hotelini ingawa hazikuonyesha vizuri tukio, pamoja na kamera nyingine walizoamini zinaweza kusaidia upelelezi.

“Za hoteli zilionyesha kwa kufifia, lakini tuli-trace (tulifuatilia) na tulitumia kote na za nje ya hoteli,” alisema.

Ni kamera au mashahidi?

Akitoa taarifa ya kutekwa Mo kwa mara ya kwanza, Makonda alisema: “Kwa mwonekano wa haraka Wazungu ndio walikuja kumkamata Mo na kumwingiza kwenye gari yao, manake hawa sio raia, watakuwa ni wageni.”

Katika eneo la tukio pia, Mambosasa alisema: “Lakini niseme tukio hili limefanywa kwa kusimamiwa na hao wageni, Wazungu wawili. Yeyote atakayewajua hawa Wazungu waliofanya kitendo hiki cha kinyama, shughuli wanazozifanya hapa, basi watupe taarifa ili tuweze kuwafikia.”

No comments: