ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 17, 2018

Kigogo wa polisi alivyoibua mjadala akitamka ‘kidumu Chama cha Mapinduzi’

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan
By Waandishi wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Butiama/Dar. Salamu ya “kidumu Chama cha Mapinduzi” aliyotoa kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shana Butiama mkoani Mara wakati wa hafla ya kumbukizi ya miaka 19 ya kifo cha Baba wa Taifa, imeibua mjadala kwenye mitandao ya kijamii, huku mwenyewe akisisitiza angependa vyama vingine vife.

Akiwa katika mashindano ya Mwalimu Nyerere Historical Marathon yaliyohusisha mbio za riadha, baiskeli na matembezi ya kilomita mbili yaliyofanyika wilayani Butiama, Oktoba 13, Kamanda Shana alisema salamu hiyo ni maalumu kwa sababu ni ya chama kilichoasisiwa na kuongozwa na Mwalimu Nyerere.

Kabla ya kutoa salamu hiyo, kamanda huyo aliyemwakilisha Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro, katika hafla hiyo aliwaeleza waliohudhuria kuwa ana salamu maalumu ambayo angependa kuwafundisha na kuwataka waitikie kama ishara ya kumuenzi Mwalimu.

Huku akipunga ngumi ya mkono wa kulia hewani na kuwahimiza wahudhuriaji nao kufanya hivyo, Kamanda Shanna alisikika akisema, “Leo naomba niwafundishe salamu mpya, nikisema kidumu Chama cha Mapinduzi mnatakiwa kuitikia kidumu milele.”

Akizungumzia suala hilo jana baada ya kuulizwa na Mwananchi iwapo ofisa wa polisi anaweza kuwa shabiki wa siasa, msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa alisema limetokea mkoani Mara hivyo atafutwe kamanda wa polisi wa mkoa huo kulizungumzia.

“Mpigie kamanda wa Mara, huko ndiko alikofanya hilo tukio, msikilize yeye ndiye ana nafasi nzuri ya kulizungumzia,” alisema Mwakalukwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Juma Ndaki alisema Shanna alipotoka kwa sababu jeshi hilo halishabikii chama chochote cha kisiasa.

Ndaki alisema hivyo huku akihoji kwa kufanya hivyo wanachama wa vyama vingine watamfikiriaje na kumuangaliaje.

Kamanda huyo alisema watu hao wataona kama hayupo upande wao.

“Kijeshi hakufanya sawa, ila ungemuuliza mwenyewe nadhani angekuwa na majibu mazuri. Sipo kwenye nafasi nzuri ya kuzungumzia, (ila) ninachojua jeshi halifungamani na chama chochote, ni la watu wote,” alisema kamanda huyo.

Hata hivyo katika mahojiano na Mwananchi, kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Shanna kuhusiana na ‘clip’ hiyo, alisema kama ifuatavyo;

Mwandishi: Kamanda habari yako, umeonekana kwenye video inayosambaa mitandaoni ukikisifiwa Chama cha Mapinduzi, taratibu za Jeshi la Polisi zinaruhusu hilo?

Shana: Wewe dini gani?

Mwandishi: Mkristo kamanda

Shana: Umewahi kuwasalimia Waislamu kwa salamu yao.

Mwandishi: Kamanda ungenipa jibu tu kuwa ulikuwa unawasalimia CCM kwa salamu yao au vipi kwa muktadha wa swali lako la dini?

Shana: Ninasema hivi, ile haikuwa sherehe ya CCM yalikuwa maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 19 tangu kufariki Baba wa Taifa. Nikawaambia njia pekee ya kumuenzi Baba wa Taifa ni kutaka chama alichokiasisi kidumu, ambacho ni CCM.

Mwandishi: Pamoja na hivyo kamanda maadili ya polisi yanaruhusu hilo?

Shana: Nenda kasikilize ile video vizuri urudi kwangu, salamu niliyotoa mimi hata CCM wenyewe hawasalimiani hivyo, nilisema kidumu Chama cha Mapinduzi, sijasema CCM oyee.

Mwandishi: Kwa hiyo kamanda unataka kusema nini, naona kama sielewi.

Shana: Huelewi nini, hata leo ukiniuliza unamzungumziaje Mwalimu Nyerere, nitajibu kidumu Chama cha Mapinduzi ambacho alikiasisi.

Mwandishi: Sawa kamanda mimi nimeelewa nitajitahidi kuwaelewesha wasiokuelewa.

Shana: Kawaeleweshe shauri yao wasiponielewa.

Akifafanua, kwa nini amerekebisha kiitikio kuwa “kidumu milele” badala ya mwitikio uliozoeleka wa “kidumu chama tawala”, kamanda huyo alisema angependa kuona CCM inadumu milele na vyama vingine (shindani na CCM) vife kwa sababu hicho ndicho chama cha ukombozi na kilichoasisiwa na waasisi wa Taifa.

“Kama kikifa (CCM) hatutakuwa tunamuenzi (Mwalimu Nyerere), kinatakiwa kudumu milele na hivyo vingine (vyama vya upinzani) vifie mbali huko,” alisema Kamanda Shanna huku akishangiliwa katika mashindano hayo.

Wakati akisema na kutamka maneno hayo, kiongozi huyo wa ngazi ya juu wa polisi mkoani Mwanza alikuwa katika sare rasmi za jeshi hilo, huku nyuma yake akiwa amesimama askari ambaye ni mpambe wake aliyevalia sare za polisi Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU).

Akiwa katika hali ya hamasa na bashasha, Shanna aliyehamishiwa mkoani Mwanza Agosti 15 akitokea Mkoa wa Pwani alitumia hafla hiyo kummwagia sifa Rais John Magufuli kwa kuishi na kutekeleza kwa vitendo ndoto na maono ya Mwalimu Nyerere ikiwemo sera ya elimu bure kwa kila mtoto.

“Mwalimu Nyerere alipigania haki sawa kwa Watanzania ikiwemo elimu bure kwa wote. Baadaye tulianza kulipia na hata mimi nililipa kidogo, lakini sasa Serikali inayafanya yale aliyopigania Mwalimu Nyerere kwa kutoa (elimu) bure. Lazima tumpongeze Rais Dk John Magufuli,” alisema Shanna.

Alisema hata maisha ya Watanzania hivi sasa ni mazuri hadi askari wa majeshi nchini ambao masilahi na mishahara yao imeboreshwa.

“Hata sare zetu siku hizi ni mpya, safi na nadhifu, lazima tumpongeze (Rais Magufuli). Ninyi Abyatyama (Watu wa Butiama) tunatakiwa kumuenzi Mwalimu Nyerere kuanzia hapa kiwilaya, kimkoa na hatimaye kitaifa maana nyumbani kumenoga,” alisisitiza.

Wakati viongozi wa Serikali na CCM waliohudhuria hafla hiyo ambayo mgeni rasmi alikuwa Spika wa Bunge mstaafu, Pius Msekwa walionekana kufurahia maneno hayo, mmoja wa wastaafu serikalini aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina gazetini alikosoa akisema ni kinyume cha maadili ya utumishi wa umma kwa kiongozi wa polisi kuonyesha mapenzi na itikadi za kisiasa hadharani.

“Kwa maneno yake ni dhahiri huyu (Kamanda Shanna) hawezi kuwatendea haki wanachama wa vyama vingine vya siasa. Nimesikia amemwakilisha IGP Sirro sijui kama ndiye aliyempa maneno haya aliyoyasema au haya ni yake binafsi. Itoshe tu kusema amepotoka na kukiuka maadili,” alisema mstaafu huyo.

“Mfumo wa vyama vingi vya siasa uko kikatiba na kisheria, hata kama RPC ni muumini na mwanachama wa CCM hakupaswa kuonyesha hilo hadharani kwa sababu kwa nafasi yake anawahudumia Watanzania wa vyama vyote na sheria inamkataza kuwa na itikadi kisiasa.”

Katibu wa Chadema Mkoa wa Mara, Chacha Heche alisema alichokifanya Kamanda Shanna ndio uhalisia anauona miongoni mwa viongozi na watendaji wa jeshi hilo.

“Tofauti yake na wenzake ni kwamba yeye (Shanna) katoka hadharani kuthibitisha kinachofanyika kwa kificho,” alisema Heche.

Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Serengeti, Rhobi Magoiga alisema alichokisema Shanna ndicho kinachotekelezwa na watendaji serikalini nyakati za chaguzi mbalimbali kwa kuhakikisha mgombea wa CCM anatangazwa kuwa msindi kwa gharama yoyote.

“Kama RPC anataka CCM idumu milele unategemea mpinzani atatangazwa mshindi kwenye uchaguzi ili CCM isidumu milele?” alihoji Magoiga.

No comments: