Mapenzi ni hisia. Unapokuwa umempenda mtu, ukawa na malengo naye halafu akaanza kukuumiza, kukunyanyasa au kukufanyia usaliti inafika mahali unahisi kwamba uliyenaye si wako. Haijalishi mmetoka wapi, haijalishi mlikuwa na ahadi gani lakini kuna wakati mnafika na mmoja wenu anaamua kukaa pembeni. Anaamua kukuacha.
Anajinasua kutoka kwenye himaya yako maana haioni furaha yoyote zaidi ya mateso. Moyo wake unakuwa umejaa majeraha ya kutosha, upendo wote unatoweka hivyo hawezi kuwa sawa kirahisi. Anakuwa kama mtu aliyechomwa sindano ya ganzi, hata umfanye nini ili akupende inamchukua kazi sana kukubaliana na wewe. Moyo wake umechoka. Suluhisho pekee analoliona ni kukaa mbali na wewe. Akikuona anakumbuka maumivu, kumbukumbu za matukio mabaya zinamjia na kutokea kukuchukia.
Kwa kawaida, mtu wa aina hii awali anakuwa alikupenda kwa dhati. Yawezekana alihitaji mfike mbali lakini mwisho wa siku, anashindwa. Maumivu yamekuwa sehemu ya maisha yake, anaamua kukaa pembeni. Ndugu zangu, ni vyema sana mnapokuwa kwenye uhusiano, mshughulikie sana suala la furaha ya mioyo yenu maana moyo ndio kila kitu katika maisha ya uhusiano.
Kila mmoja awe tiba ya moyo wa mwenzake. Kila mmoja aone ana wajibu wa kuisaka, kuilinda amani ya moyo wa mwenzake. Usikubali kabisa kumuona mwenzako ana sononeko la moyo. Kataa kuwa sehemu ya maumivu ya mwenzako. Iwekeni hiyo kama kanuni ya maisha yenu kwamba katika hali yoyote, hakikisheni mnakuwa na amani ya moyo. Hata mgombane vipi lakini msiruhusu kuipoteza amani ya moyo.
Mwenzako akikukosea, akikasirikika, kaa naye mbali hasira zikiisha basi rudi ukiwa na akili mpya maana wakati mwingine, kuondoka eneo la ugomvi kunaweza kusaidia kuepusha shari. Thamani ya mwenzi wako ni rahisi sana kuishusha pindi unapokuwa kwenye hasira, baadaye ukija kutafakari ni rahisi kujutia kile ulichokifanya.
GPL
No comments:
Post a Comment