ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 26, 2018

Mambo mazito huko Jangwani, Mchungahela mbele kwa mbele

By MWANAHIBA RICHARD

Dar es Salaam. Baadhi ya klabu za Ligi Kuu na ligi zingine ni klabu za wanachama ambazo hulazimika kufanya uchaguzi kuwapata viongozi wao tofauti na klabu ambazo zipo chini ya kampuni ambazo uongozi wake unaundwa na Bodi ya Wakurugenzi.
Miongoni mwa klabu za wanachama ni Yanga ambayo ni klabu kongwe na sasa inatakiwa kufanya uchaguzi wao kuwapata viongozi watakaoongoza kuanzia Januari 13 mwakani hasa nafasi ambazo viongozi wao walijiuzulu.
Uchaguzi wa sasa unaendana na uchaguzi wa mwaka 2016, ambapo Yanga iliingia kwenye mgogoro na Shirikisho la Soka nchini (TFF) kupitia Kamati ya Uchaguzi ya shirikisho hilo kama ilivyo sasa.
Mwaka huo pia TFF ilitaka kusimamia uchaguzi wa Yanga jambo ambalo lilipingwa vikali hata wagombea waliochukuwa fomu kupitia TFF baadaye walilazimika kurudishwa klabuni baada ya kufikia muafaka kwamba Yanga ijisimamie yenyewe uchaguzi kupitia kamati yao ya uchaguzi ila TFF wawe waangalizi tu kama ilivyo kawaida mara nyingi.
Kwa mujibu wa taratibu zao za uchaguzi klabu inapofanya uchaguzi wake Kamati ya Uchaguzi ya TFF yenyewe inawakilishwa na mwakilishi wao ili kuangalia jinsi mchakato mzima unavyokwenda hadi wanapopata viongozi wapya.
Uchaguzi wa Yanga umekuwa katika mvutano mkubwa kati ya Yanga wenyewe na TFF, mvutano wao ni kwamba asilimia kubwa ya wanachama wa klabu hiyo wanadai kumtambua Yusuf Manji kama Mwenyekiti wao hata kama aliandika barua ya kujiuzulu tangu mwaka jana.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini ya Yanga, George Mkuchika hivi karibuni aliwaambia Wanayanga kwamba Manji aliandika barua ya kukubali kuendelea kuwa Mwenyekiti wao baada ya kuombwa abatiishe maamuzi yake ya awali.
TFF wenyewe awali walikubaliana na taarifa ya Yanga kwamba bado wanamtambua na hivyo aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Clement Sanga kumuondoa nafasi hiyo kwa kukosa sifa kwani alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga ingawa baadaye alijiuzulu nafasi hiyo pia.
Uchaguzi wa Yanga uliingiliwa pia na serikali kwa kuitaka TFF isimamie uchaguzi huo kwasababu kwamba Kamati ya Utendaji ya Yanga haijakidhi akidi kwani kati ya wajume 13 wa kamati hiyo wamebaki wajumbe wanne tu.
Mwanaspoti ilifanya mahojiano na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Wakili Malangwe Mchungahela alielezea mambo mbalimbali kuelekea uchaguzi huo.

RATIBA
Kamati ya Uchaguiz ya TFF ilianza mchakato rasmi wa kutoa fomu za wagombea Novemba 8 hadi 13 lakini zoezi hilo baada ya kufungwa kamati hiyo iliamua kuongeza siku tano mbele ambapo lilifungwa rasmi Novemba 19.
Mchungahela anaelezea; "Mabadiliko haya hayajaharibu jambo lolote kwani ratiba inaendelea ile ile ingawa mwanzo baada ya kuongeza soku za kuchukuwa fomu tulitaka tubadilishe. Hatujabadilisha kwa vile muda unatubana hivyo tutaendelea na ratiba hii hadi siku ya mwisho hata tarehe ya uchaguzi inabaki ile ile ya Januari 13 mwakani,"

MHURI

Fomu za wagombea wote zilizopitishwa kwenye mchujo wa awali na kamati hiyo hazijagongwa mhuri lakini imeelezwa kwamba hilo sio tatizo na wala haizuii kuendelea na mchakato huo.
"Hizi fomu zimegongwa mhuri wa TFF pamoja na kusainiwa na Kaimu Mwenyekiti Thobias Lingalangala, hivyo inatosha kabisa sio lazima mhuri wa klabu uwepo, saini ya Kaimu inatosha kabisa wala hatuwabembelezi kuleta mhuri wa klabu," alisema Mchungahela

REJA YA WANACHAMA

Kamati ya uchaguzi iwe ya klabu ama ya TFF ni lazima iwe na reja ya wanachama wa klabu husika ili kusaidia kufahamu wanachama wangapi wapo hai ambao wanatakiwa kupiga kura lakini hii imekuwa tofauti kwani Kamati ya TFF bado haijapata reja ya wanachama wa Yanga.
Mwenyekiti huyo amefafanua hilo kwamba; "Reja nitaipata tu, hadi kufikia siku ya uchaguzi itakuwa imepatikana kwani kuipata sio kazi, hata kama hawataleta wao, ni lazima tuwe nayo maana itatuongoza kufahamu idadi ya wanachama wao, muda bado upo wa kupata hivyo hilo halina shaka kabisa,"

LINGALANGA KURUDI

Baada ya Mkuchika kutoa barau iliyodaiwa kuandikwa na Manji kukubali kurejea kuiongoza Yanga lakini kuanzia Januari 15 mwakani, Lingalanga aliyeteuliwa kuwa Kaimu Mwenyekiti alitangaza kuachia madaraka hayo.
Lakini hivi sasa Lingalangala amerejea na kusaini fomu za wagombea hao kimya kimya ambapo Mchungahela amesema ni sahihi Kaimu kusaini fomu hizo kwa mujibu wa taratibu na kanuni za uchaguzi.
"Sisi tunamtambua Lingalangala ndio maana amesaini hizi fomu, yeye ndiye aliyechaguliwa kukaimu nafasi hiyo, habari za kujiuzulu kwake kumpisha Manji sisi hatuna maana hatumtambui Manji kama Mwenyekiti wa Yanga kwa mujibu wa Katiba ya Yanga kwani alijiuzulu mwenye kwa maandishi, hivyo Lingalanga kufanyakazi za Yanga ni sahihi ikiwemo hii ya kusaini fomu za wagombea," alisema

KUGEUKA MAAMUZI YA KIKAO
TFF ilikutana na wajumbe wanne wa Yanga ili kujadili juu ya suluhisho la nani asimamie uchaguzi wao, kikoa ambacho kinadaiwa hakikufikia maridhiano ingawa Mchungahela alitangaza wamekubaliana kika kitu kiendelee kama ilivyopangwa, yeye anaelezea'
"Walikuja wajumbe wanne wa Kamati ya Utendaji ambao ndiyo wamebaki kati ya wajumbe wote baada ya wengine kujiuzulu. Wajumbe wawili walikubaliana kila kitu na sisi lakini wawili walikataa nao hao wlaikataa kwenye kipengele cha Manji tu kutomtambua kama sio Mwenyekiti wao, wenyewe walidai bado ni Mwenyekiti wakati hata Katiba yao inaelezea sifa za uongozi aliyejiuzulu.
"Hivyo wakati tunatangaza maadhimio ya kikao kile tulikuwa tumefikia makubaliano na kwamba kama wanamuhitaji Manji wamchukulie fomu lakini hawakufanya hivyo hadi zoezi linafungwa,"

OMARY KAYA ATEGWA
Kaimu Katibu Mkuu Omary Kaya ni kama ametegwa na pande zote mbili, upande wa klabu na TFF baada ya kamati ya Mchungahela kumwandikia barua ya mwaliko kuhudhulia kikao cha mchujo wa awali ama kutuma mwakilishi lakini upande wa klabu unadaiwa kumpiga 'stop' kuhudhuria kikao chochote kinachohusu uchaguzi.
"Kaya tulimwandikia barua ili afike kwenye kikao cha mchujo wa awali hata asipokuja yeye atume mwakilishi ila haijawa hivyo, sisi tunaendelea kama kawaida hata wao wasipokuja mpaka hatua ya mwisho, maana tuliwaomba tushirikiane lakini hawaonyeshi ushirikiano, hivyo watajuwa wenyewe sisi jitihada zetu naona zimegonga mwamba," alisema

CHANGAMOTO
Kusimamisha uchaguzi wa klabu kubwa hata kama hausimamiwi na TFF unakuwa na changamoto kubwa ndivyo anavyopata changamoto kubwa Mchungahela.
"Kuna changamoto nyingi sana kwenye uchaguzi huu wa Yanga, kwanza ukizingatia ni klabu ambayo ina wanachama wengi maana inafikia hatua unatukanwa matusi ambayo mtu hutarajii, ila hainikatishi tamaa kwani ni moja ya mambo ambayo ukiwa kiongozi unakutana nayo, ila vigezo, sifa na kila kitu kinachotakiwa kufuata kwenye uchaguzi huo kitafuatwa na kusimamiwa," alisema.
Mchungahela alisema michakato miwili tayari imefanyika kuchukuwa na kurudisha fomu pamoja na mchujo wa awali ambapo wagombea wote sasa wamejulikana na hao ndiyo wanaingia hatua nyingine ya usaili na kama watawekewa pingamizi.

Mwanaspoti

No comments: