ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, November 29, 2018

TAARIFA YA KUTOKEA KWA KIMONDO MKOANI KAGERA

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MADINI
TAASISI YA JIOLOJIA NA UTAFITI WA MADINI TANZANIA
TAARIFA YA KUTOKEA KWA KIMONDO MKOANI KAGERA

Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imepokea taarifa ya kudondoka kwa kitu kilichokuwa na mwanga mkali na cheche kikitokea angani kilichosababisha ngurumo na mitetemo midogo mnamo majira ya saa tatu usiku wa tarehe 27/11/2018. Kutokana na taarifa hizo GST imebaini kuwa kitu hicho inawezekana kuwa ni kimondo.

Vimondo ni majabali ya miamba ambayo yanapatikana katika mfumo wa Sayari wa ulimwengu (outer space) katika anga za mbali. Majabali hayo ni sehemu ya vipande vya sayari ndogo (asteroids) au vipande vikubwa vya miamba (meteoroids) vilivyovunjika kutokana na sababu ya nguvu za asili.

Kuvunjika kwa sayari ndogo na vipande vikubwa vya miamba husababisha vipande vya miamba kuzunguka bila mpangilio katika mihimili hivyo hugongona na kupoteza uelekeo na kuingia katika anga la Sayari yetu ya dunia. Kutokana na uzito mkubwa wa majabali hayo na nguvu ya uvutano ya dunia (gravitational force), majabali hayo hudondoka kwa kasi kubwa kwenye uso wa Dunia. Msuguano baina ya majabali hayo na hewa iliyopo katika anga la Dunia husababisha kutokea kwa cheche za moto na mwanga mkali wakati yanadondoka.

Hapa nchini Tanzania kumewahi kudondoka kimondo katika Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe kilichogunduliwa mwaka 1930 na kinakadiriwa kuwa na uzito wa tani kumi na mbili (12) chenye ukubwa wa kimo cha mita 1.22, upana wa mita 1.63 na urefu wa mita 3.3. Kimondo hiki ni mojawapo ya vimondo vizito kumi vinavyojulikana ambacho ni cha nane kwa ukubwa duniani na cha pili kwa ukubwa Afrika. Kimondo hiki ni kati ya vimondo vinavyofahamika duniani kudondoka katika sehemu ya nchi kavu kwenye uso wa dunia, kwani vipo vingi vilivyodondoka katika sehemu za majini kama kwenye bahari na maziwa mbalimbali duniani.

Kwa kawaida vimondo hivi havina athari kwa watu na mali zao kama havijaanguka katika miundo mbinu iliyopo. Aidha, vimondo hivi husababisha mitetemo midogo vinapodondoka katika uso wa dunia. Hata hivyo tukio hili ni la kawaida na hutokea maeneo mbalimbali duniani na hadi sasa jumla ya matukio zaidi ya 1,400 yamesharipotiwa.

Hivyo GST inapenda kuwatoa hofu wananchi wa mkoa wa Kagera na kuwaomba waendelee kufanya kazi zao za maendeleo.

IMETOLEWA NA TAASISI YA JIOLOJIA NA UTAFITI WA MADINI TANZANIA 29/11/2018

No comments: