Mbunge wa jimbo la Vunjo ,Mh James Mbatia akizungumza wakati wa mkutano wake uliofanyika katika Mji Mdogo wa Himo.
Baadhi ya wananchi wakimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Vunjo Mh ,James Mbatia wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika jimboni hapo.
Mbunge wa jimbo la Vunjo,James Mbatia akifanya dua na baadhi ya viongozi mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Ghalani Mji Mdogo wa Himo.
Kilimanjaro.
MWENYEKITI wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na Mbunge wa Vunjo,
James Mbatia amewamegea siri wananchi wa mji mdogo wa
Himo juu ya mazungumzo yake na Rais Dk. John Magufuli, Ikulu Jijini Dar es
Salaam.
Alidai alikwenda kumueleza malalamiko ya wananchi kuhusu amri ya Mkuu
wa Wilaya ya Moshi ya kusitisha ujenzi wa barabara na kusababisha hasara ya
mabilioni ya shilingi.
“Haya yote nimemueleza Mheshimiwa Rais (Magufuli) niwe mkweli,
nilibahatika hapo katikati Mheshimiwa Rais akaniita akasema hivi, narejea sauti
ya Rais aliniambia na ameshaagiza ofisi zake na wengine wameniita Dodoma,
barabara za wana Vunjo atachangia yeye binafsi kama John Pombe Magufuli, pili
serikali yake itachangia na tatu atakuja kama Amiri Jeshi Mkuu kufungua
barabara hizi yeye mwenyewe kama John Pombe Magufuli,”alisema
Mbatia alikuwa
akizungumza na wananchi wa Kata ya Makuyuni katika Mamlaka ya Mji mdogo wa
Himo, Wilaya ya Moshi wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya
ghalani.
Mradi wa upanuzi na ujenzi barabara za vijijini kwa kiwango cha
changarawe unaodaiwa kusisitishwa katika Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro,
unahusisha barabara zenye urefu wa kilometa 389.3 ambazo zilikuwa zigharimu Sh.
bilioni 12.077 kutokana na utafiti wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini
(Tarura) wa mwaka huu.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kippi Warioba anadaiwa
kusimamisha kazi ya ujenzi wa barabara hizo na hivyo kusababisha hasara.
Zaidi Mbatia alisisitiza: “Sasa tuone ni nani
zaidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na maendeleo ya watanzania,
maendeleo hayana itikadi za vyama. Kwa nini amefanya hivyo, kwa sababu Jimbo la
Vunjo tumekuwa wa kwanza Tanzania kuweza kujipanga wenyewe mpaka hatua
tuliyofikia ya kujiletea maendeleo yetu wenyewe na tujipongeze wana Vunjo.
"Hizi barabara zikiwa vizuri si tunazitumia sote, barabara za
Makuyuni zikiwa nzuri zitaendelea kutumiwa na watu wote hata kama Mbatia sitakuwa Mbunge…Mimi sijawahi kumtukana Rais, sasa
atakuja yeye mwenyewe.”
Mbatia alikutana na
Rais Magufuli na kufanya mazungumzo naye Ikulu, Novemba 13 mwaka huu akiwa
pamoja na wanasiasa wengine Mh. John Cheyo (UDP), John Shubuda na
mfanyabiashara Rostam Aziz.
Katika mkutano huo, Mbatia aliwaeleza wananchi
hao kwamba amekopa fedha zaidi ya Sh. milioni 500 Benki ya CRDB kwa ajili ya
kununua mitambo ya ujenzi wa barabara hizo.
“Mimi nimenunua mitambo sawa, mingine tunakodisha sawa lakini tukasema
wananchi waanze kuchangia mafuta kwenye hiyo mitambo hiyo, kwa mfano Kijiji cha
Mshihiri mpaka leo hii wameshachangia takribani Sh. milioni 26 lakini
ukichanganya zote pamoja na za Ashira ni zaidi ya Sh. milioni 30 na kitu
huko,”alieleza
Akijibu maswali ya wananchi kuhusu kukwama kwa ujenzi wa barabara za
Samanga/Sembeti, Mbunge huyo alisema Mungu sio Athuman na akawataka wananchi
hao kusubiri kwanza ili mdomo wake usiteleze kwa vile wana kesi mahakamani.
Wakati anahitimisha mkutano huo, Mbatia
aliipongeza Kamati ya Maendeleo ya wana Vunjo (VDF) chini ya Askofu Mstaafu wa
KKKT Dayosisi ya Kaskazini Dk. Martin Shao, mashekhe wetu, mapadri wetu na
wachungaji na viongozi wote, akisema yeye binafsi toka sakafu ya moyo wake hana
chuki na mtu yeyote na anamshukuru Mungu amesikia na Mheshimiwa Rais (Magufuli)
amesikia dua zao.
Mwisho
No comments:
Post a Comment