ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, January 26, 2019

Tanzania yashinda Tuzo Maonesho ya Kimataifa ya Utalii, India



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tanzania yashinda Tuzo Maonesho ya Kimataifa ya Utalii, India

Ubalozi wa Tanzania, New Delhi, Taasisi za Serikali na kampuni binafsi mbalimbali za utalii nchini zimeshiriki Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Mwaka 2019 nchini India yajulikanayo kama OTM 2019 [Outbound Travel Mart-2019] kwa lengo la kutangaza na kutafuta fursa mpya za soko la utalii nchini humo.

Maonesho hayo maarufu na makubwa kabisa katika ukanda wa Asia-Pasifiki yalianza tarehe 23 Januari, 2019 na yamemalizika leo tarehe 25 Januari, 2019, Maonesho haya hufanyika kila mwaka katika Jiji la Mumbai na kushirikisha taasisi mbalimbali za utalii duniani.

Taasisi za Serikali zinazoshiriki ni Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Kituo cha Kutangaza Utalii wa Zanzibar India [Zanzibar Tourism Promotion Centre]. Kwa upande wa kampuni binafsi ni Leopard Tours, Zara Tours, Ngarawa Hotel and Resort, DOTCOM Safaris Ltd na Jackal Adventures.

Katika Maonesho hayo, Banda la Tanzania limeibuka Mshindi wa Kwanza kwa upande wa Banda bora lilopambwa kwa unadhifu na kuvutia watu wengi [The winner of Best Decoration Award].

Balozi wa Tanzania nchini India Mhe. Baraka Luvanda amesema kuwa maonesho hayo ni fursa adhimu kwa nchi kutangaza vivutio vya utalii ambapo wafanyabiashara wapatao 15,000 wanaojishughulisha na masuala ya utalii walishiriki kutoka katika mataifa zaidi ya 50 duniani. Washiriki wamepata fursa ya kupeana taarifa muhimu kuhusu mwelekeo na maendeleo ya biashara ya utalii katika maeneo mbalimbali duniani, vivutio vipya pamoja na kufanya biashara.

Akiwa katika maonesho hayo, Balozi Luvanda alieleza kuwa maonesho yalisaidia washiriki kukutana na wadau na kuanzisha uhusiano wa kibiashara unaotarajiwa kufungua soko la utalii nchini baada ya wadau hao kupata maelezo ya kutosha kuhusu vivutio vilivyopo nchini na faida zake. Kwa ujumla, India ina soko kubwa la utalii. Tunategemea idadi ya watalii kutoka India wanaokwenda Tanzania itaongezeka mara dufu baada ya kuanza kwa safari za ndege za Shirika la Ndege la Tanzania [Air Tanzania] moja kwa moja kutoka Tanzania kuja India ambapo zinategemewa kuanza kabla ya mwezi wa Juni 2019.

‘Nachukua fursa hii kwa dhati kuwapongeza sana Maafisa wote walioshiriki katika Banda letu la Tanzania la Maonesho kwa kazi nzuri iliyowezesha ushindi huo wa kwanza kwa upande wa Banda bora lilopambwa kwa unadhifu na kuvutia watu wengi [The winner of Best Decoration Award]”, alisema Balozi Luvanda.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
25 Januari 2019

Waziri wa Nchi anayeshughulikia masuala ya Utalii wa India, Mhe. K. J. Alphons akiwa katika banda la Tanzania. Kulia kwake ni Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda akiwa na washiriki wengine katika Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Mwaka 2019 Jijini Mumbai, India tarehe 23 Januari, 2019

Picha ya pamoja ya washiriki baada ya kupokea Tuzo ya ushindi wa kwanza kwa upande wa Banda bora la maonesho lilipambwa kwa unadhifu na kuvutia watu wengi [The Winner of Best Decoration Award] katika Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Mwaka 2019 Jijini Mumbai, India tarehe 25 Januari, 2019.

Wageni mbalimbali wanatembelea banda la Tanzania ili kupata maelezo kuhusu vivutio vya utalii nchini.

Wageni katika banda la Tanzania wakipata maelezo kuhusu fursa na vivutio vya utalii nchini.

No comments: