Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewashauri wananchi wote wanaoharibu misitu kwa kuchoma moto kwaajili ya kuwinda panya waanze kufuga kuku ili kuweza kuokoa mazingira huku
akiwataka wakurugenzi wa halmashauri za Mkoa huo kuhakikisha wanamuandalia mipango mikakati ya halmashauri zao katika upandaji wa miti ikiwa ni kufuata agizo la serikali la kuitaka kila halmashauri kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka.
Alisema kuwa moja ya matokeo ya shughuli hizi za kibinadamu ni uharibifu mkubwa wa mistu na vyanzo vya maji unaoweza kusababisha madhara makubwa kama kukosa mvua kwa wakati, uzalishaji mdogo wa chakula na hata maradhi mbalimbali yanayotokana na uharibifu wa mazingira na kuongeza kuwa ufanisi wa zoezi hili la upandaji miti unatia shaka kutokana na kutosimamiwa vizuri na Viongozi wa Halmashauri zetu zote.
“Kwa hiyo naagiza Wakurugenzi wote wa Halmashauri zetu kuwasilisha mpango mkakati wa upandaji miti kwa kipindi cha Mwaka huu, ikiwa ni pamoja na kubainisha idadi ya miti waliyonayo na mahali ilipo pamoja na ya Wadau wao wa utunzaji wa Mazingira, na maeneo ya kupanda. Mpango huu unifikie ndani ya siku tano kuanzia leo,” Alisisitiza.
Vile vile alizitaka Taasisi za Serikali kama shule, magereza na vyuo vya elimu kuanza kutumia nishati mbadala ikiwemo ya “biogas” katika shughuli zao za mapishi ya chakula na kupunguza kasi ya matumizi ya kuni kwani mkoa una mitambo 2 ya “biogas” katika Manispaa ya Sumbawanga katika Vijiji vya Mtimbwa na Ntendo ambayo inatumika kama darasa la kujifunzia ujuzi wa kutengeneza biogas kutokana na mabaki ya mifugo yetu.
Wakati akisoma taarifa ya halmashauri juu ya zoezi la upandaji miti, Afisa Ardhi na malisili wa halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Juma Chande alieleza kuwa katika msimu wa mwaka 2018/2019 katika kata 8 kati ya kata 27, halmashauri imeshapanda miti 292,899 ambayo ni asilimia 17.4 ya lengo na ufafanua kuwa halmashauri inaendelea kutoa elimu ya kutunza mazingira, kupanda miti na kilimo mseto huku akitaja changamoto zinazorudisha nyuma juhudi hizo.
“Miongoni mwa changamoto ni muitikio mdogo wa wananchi katika utunzaji wa mazingira pamoja na hamasa nyingi kutolewa kwao, mila na tamaduni za wananchi za uwindaji wa panya mathalani kusababisha uchomaji wa miti wakati wa kiangazi mfano maeneo ya vijiji vya Msandamuungano, Sandulula na Mpwapwa hivyo kuathiri misitu iliyopandwa.” Alimalizia.
No comments:
Post a Comment