Advertisements

Friday, February 15, 2019

A-Z KIJANA ALIYEUAWA NA POLISI ARUSHA

ARUSHA: Kijana Richard Peter Lombo (29) ameuawa kwa kupigwa risasi na askari Polisi wa Kituo cha Polisi Usariva mkoani Arusha Alhamisi iliyopita kwa kile ambacho kimedaiwa na polisi kuwa alikuwa kibaka.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP Longinus Tibishubwamu akizungumza kwa njia ya simu alisema kuwa kijana huyo alikuwa kibaka na alitaka kumnyang’anya silaha askari. Kamanda alisema katika purukushani hiyo ilisababisha risasi kufyatuka na kumpata kijana huyo kifuani.

Hata hivyo, kaka wa marehemu Richard, Issa Juma alidai kuwa alikuwa na marehemu wakati wa tukio na alishuhudia askari akimfyatulia risasi kifuani nduguye na akafariki dunia papohapo kituoni. Akielezea tukio hilo baba mzazi wa marehemu, mzee Peter Lombo alikuwa na haya ya kusema:

“Nakumbuka siku ya Alhamisi saa mbili na nusu usiku walikuja nyumbani kwangu askari na mwenyekiti wa kitongoji cha Mabadilisho jirani wakasema wanawahitaji vijana wangu wamefanya tukio.

“Niliwatoa ndani, wakawafunga mikono na askari wakaenda nao kituoni. Kesho yake saa 5.30 walikuja askari hapa nyumbani na kunichukua wakanipeleka kwa afisa usalama wa wilaya, nikaambiwa twende kituoni.

“Tulipofika kituoni niliwekwa kikao, nikaambiwa unajua nini kuhusu historia ya mwanao, niliwaambia baada ya mwanangu kumaliza chuo, niko naye nyumbani akifanya shughuli zangu.

“Nikawahoji, ni kitu gani kinaendelea? Wakasema hakuna tatizo, nikawauliza mwanangu kama amekufa mnieleze, wakasema ni kweli amekufa. Nililia sana kwa dakika tano kisha niwaomba wanionyeshe mwili wa mwanangu.

“Wakasema mtoto wako yupo mochwari, nikasema basi naomba nikauone mwili, wakasema hutaenda mwenyewe, tutakupeleka.

“Walinipeleka Hospitali ya Mount Meru na kuuona mwili. Kijana wangu alikuwa amepigwa risasi ya kifuani na kutokea mgongoni. Nililia sana, nikatoka kurudi nyumbani.

“Nilikwenda nyumbani kisha nikaenda ofisi ya wilaya ya CCM ambako mimi ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Kata, nikaonana na diwani na afisa mtendaji wa kata, nikasaidiwa, wakasema watashughulikia tatizo langu.”

Mzazi huyo wa marehemu alitaka sheria ifuate mkondo wake kwa wale askari waliomuua mwanaye.

Baadhi ya wakazi wa Usariva walisema kitendo alichofanyiwa marehemu kilikuwa ni kibaya na alikamatwa bila kuhusishwa viongozi wa mtaa huo.

“Nimejisikia vibaya sana kwa kijana huyu kuuawa kwa sababu hatujasikia au kuona akifanya vitendo vya kihalifu” alisema mmoja wa wakazi wa eneo hilo.

Stori: Mwandishi Wetu, Amani

No comments: