Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Mafunzo ya Lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Sikitu Saimoni akiongea na watoa huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya wa mikoa ya Dodoma na Singida wakati wa mafunzo ya virutubishi mchanganyiko yanayoendeshwa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kwa kushirikiana na TFNC jijini Dodoma
Kaimu
Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Mafunzo
ya Lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Sikitu
Saimon amesema kwamba Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kupitia mradi
wa Boresha Lishe umepanga kugawa virutubishi mchanganyiko katika mikoa ya
Dodoma na Singida kwa ajili ya kupambana na utapiamlo kwa watoto chini ya miaka
2.
Sikitu
amebainisha hayo wakati wa mafunzo ya matumizi ya virutubishi mchanganyiko kwa
watoa huduma za afya wa mikoa ya Dodoma na Singida yanayofanyika kwa siku 3
kuanzia tarehe 01/04/2019 hadi tarehe 03/04/2019 katika ukumbi wa Ujenzi jijini
Dodoma. Mafunzo hayo yametolewa kwa washiri kutoka vituo 40 vya wilaya za Bahi,
Chamwino, Ikungi na Singida Vijijini.
Sikitu
amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo watoa huduma katika vituo vya
kutolea huduma ili waweze kuwasimamia na kuwaelekeza walengwa juu ya njia
sahihi ya matumizi ya virutubishi hivyo kwa ajili ya kupambana na utapiamlo.
“Tanzania sasa tunakabiliwa na aina mbili za
utapiamlo: utapiamlo wa virutubishi vilivyozidi na utapiamlo wa upungufu wa
virutubishi. Aina ya kwanza ya utapiamlo inawakabili sana watu wazima lakini
hii aina ya pili inawakabili sana watoto wadogo chini ya miaka mitano. Athari
ya utapiamlo kwa mtoto, humuathiri ukuaji wake kimwili na kiakili, na matokeo
yake hata shuleni tunapata wanafunzi wasiofundishika au wasioelewa.
Hivyo wakati
sahihi wa kupapambana na utapiamlo kwa mtoto ni katika siku 1000 za mwanzo ya
maisha yake kwa kuhakikisha mama anapokuwa mjamzito anapewa lishe bora, na
mtoto anapozaliwa kwa miezi sita ya mwanzo anyonyeshwe maziwa ya mama pekee, na
anapotimiza umri wa miezi sita hadi miaka miwili ni kuhakikisha anapewa chakula
kilichoongezewa virutubishi mchanganyiko” amesema Sikitu Saimon.
Afisa Lishe
kutoka WFP, Neema Shosho, amesema kwamba mradi wa Boresha Lishe unatekelezwa
katika Wilaya nne za mikoa ya Dodoma na Singida ambazo ni Bahi na Chamwino kwa
mkoa wa Dodoma, Ikungi na Singida Vijijini kwa mkoa wa Singida.
Pia amesema
kwamba mradi huu unatekelezwa kwa muda wa miaka 5 kuanzia mwaka 2017 na
utakamilika mwaka 2022 ambapo awali mradi ulikua unagawa unga wa kutibu
utapiamlo wa kadiri na unga lishe kwa wajawazito, wanawake wanaonyonyesha, na
watoto wadogo wenye umri chini ya miaka miwili, zoezi lililokuwa linafanyika
kila mwezi kwa mwaka mzima.
“Baada ya
kufanyika tathimini na kubaini kuwa chakula kinachozalishwa na kaya katika
maeneo ya mradi kinakuwa hakina virutubishi vya kutosha. Hivyo tukaona njia
bora ni kuwapatia virutubishi mchanganyiko ambavyo vitaongezwa kwenye chakula.
Kwa hiyo sasa tunabadilisha utaratibu, hatutakuwa tunagawa tena unga kama awali
kwa kipindi chote cha mwaka mzima bali tutakukwa tunagawa katika kipindi cha mahitaji
hasa wakati wa kiangazi kuanzia mwezi Oktoba hadi mwezi Machi” Amesema Neema
Shosho.
Neema Shosho, Afisa Lishe kutoka Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) akiongea na washiriki wa mafunzo ya virutubishi mchanganyiko yanayotolewa na WFP kwa kushirikiana na TFNC kwa watoa huduma wa vituo vya kutolea huduma za Afya wa mikoa ya Dodoma na Singida.
Mery Kibona, Afisa Lishe Mtafiti kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania akiwaonesha virutubishi mchanganyiko watoa huduma wa vituo vya afya wakati wa mafunzo ya siku tatu ya virutubishi hivyo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ujenzi jijini Dodoma kuanzia tarehe 01/04/2019 hadi tarehe 03/04/2019
No comments:
Post a Comment