ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 1, 2019

KIKUNDI CHA GONGA GONGA CHAFANYA UKARABATI NA USAFI ZAHANATI YA MJI MWEMA,KIGAMBONI


Mganga Mfawidhi wa zahanati ya Mji Mwema, Dk. Beno Constatino, akitoa mkono wa pongezi kwa Vijana wa kikundi cha Gonga Gonga, muda mfupi baada ya kumaliza shughuli za ukarabati na usafi wa mazingira wa Zahanati hiyo, mwishoni mwa wiki.


KIKUNDI cha Gonga Gonga kinachojishughulisha na shughuli za useremal, wamejitolea  kufanya ukarabati na usafi katika Zahanati ya Mji Mwema, iliyopo wilayani Kigamboni, Dar es Salaam.

Kikundi hicho kiliweza kutengeneza milango iliyokuwa inasumbua ikiwemo ya vyoo, vyumba vya madaktari na maeneo mengine huku pia wakirekebisha vifaa vya umeme ikiwemo feni za majengo hayo.

Mbali na kufanya ufundi mdogomdogo pamoja na kuweka vifaa vipya, vijana hao walifanya usafi wa mazingira ikiwemo kufyeka majani na kuzibua mtaro wa maji machafu uliokuwa maeneo  ya zahanati hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Katibu wa Gonga Gonga, Ali Rajab  Ali, alishukuru kwa nafasi  waliyopewa na uongozi wa zahanati  hiyo na kusema walichofanya ni kuonesha  kuunga mkono juhudi mbalimbali  katika jamii.

“Tunashukuru kwa kupewa nafasi  ya kufanya  tukio hili, kwani lengo  letu kubwa ni kuhakikisha tunawatoa kwenye msongo wa kufikiria kifaa fulani hakifanyi kazi ama mlango haifungi.
Kwa umoja wetu pia tumefanya usafi wa mazingira maeneo yote yanayozunguka zahanati” alisema Ali.

Mganga Mfawidhi wa zahanati ya Mji Mwema, Dk. Beno Constatino, alikipongeza  kikundi hicho kwa namna walivyojitolea kufanya shughuli  za kijamii kwenye zahanati hiyo huku akiwaomba kuwa na utaratibu huo  mara kwa mara.

Dk. Beno alisema awali walikuwa wanapata changamoto kwenye hasa milango ukiwemo mlango wa leba.

Dkt. Beno alibainisha kuwa, awali walikuwa wanapata changamoto kwenye mlango huo wa leba na hata walikuwa wakiamua kusafirisha mgonjwa kuhamishiwa kituo cha Vijibweni.

Nae Mwenyekiti wa Gonga Gonga, Seleman Omari  amesema wameamua kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali hivyo kujitolea kwao huko ni kuungana na Rais katika kauli yake ya Hapa kazi. 

“Tunaungana na Serikali kuhakikisha kazi zinafanyika kwa ufanisi mkubwa  kwa madaktari na wauguzi ama wagonjwa wanaofika hapa kuwa mazingira salama.
Kwa ujuzi wetu wa ufundi tumejitolea kufanya shughuli hii bure kabisa kwani inawasaidia ndugu zetu na pia hata sie wenyewe” alisema  Omari.

Aidha, Omari aliongeza kikundi hicho cha Gonga Gonga kimesajiliwa kisheria  na kipo toka mwaka 2005 wakiwa vijana  sita na baadae kuhamasishana na  sasa kufikia 22 ambapo  wanashughulika na ufundi mkubwa wa useremala,  Sanaa za vitu vya uselemala, Umeme, Kilimo na mambo mengine.


Vijana wa Kikundi cha Gonga Gonga cha Mji Mwema, Kigamboni wakikarabati mlango wa chumba cha leba cha  Zahanati ya Mji Mwema. Mwishoni mwa wiki.




Vijana wa Kikundi cha Gonga Gonga wakifanya usafi wa eneo la mtaro wa maji machafu kwenye Zahanati ya Mji Mwema, Kigamboni mwishoni mwa wiki.



Vijana wa Kikundi cha Gonga Gonga cha Mji Mwema, Kigamboni wakifanya usafi cha choo  cha wagonjwa cha Zahanati ya Mji Mwema.

Pichani chini ni matukio mbalimbali ya Vijana hao wa Gonga Gonga:




















Pichani chini Vijana wa Gonga Gonga wakiwa kwenye Karakana yao iliyopo Mji Mwema  wakiendelea na kazi baada ya kumaliza shughuli za kufanya ukarabati na usafi katika Zahanati ya Mji Mwema.








No comments: