Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro Mathayo Masele wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Halmashauri ya wilaya ya Malinyi unaofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) akiwa katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi mkoani Morogoro mwishoni mwa wiki.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimpa maelekezo Mkuu wa Idara ya Ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Ulanga Luis Ndumbaro wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi mkoani Morogoro mwishoni mwa wiki. Kulia kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa wilaya ya Ulanga Ngollo Malenya.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (Kulia) akielekea kukagua ofisi za Ardhi za halmashauri ya wilaya ya Ulanga wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi mkoani Morogoro mwishoni mwa wiki. Wa pili kulia ni Mkuu wa wilaya ya Ulanga Ngollo Malenya na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ulanga Juma Kapilima.(PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro kumpatia maelezo kuhusiana na uamuzi wake wa kuondoa kasma ya ardhi na mipango miji kwenye bajeti ya mapato ya ndani baada ya sekta hiyo kuhamishiwa Wizarani.
Uamuzi huo wa Dkt Mabula unafuatia kuelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Ngollo Malenya kuwa moja ya changamoto inayoikabili sekta ya ardhi kwenye wilaya yake ni ukosefu wa fedha za uendeshaji wa ofisi uliosababishwa na halmashauri kuondoa kasma ya ardhi na mipangomiji baada ya sekta hiyo kuhamia wizara ya ardhi jambo alilolieleza limesababisha utekelezaji majukumu ya kila siku kuwa magumu.
Akiwa katika ziara yake ya siku moja katika wilaya hiyo mwishoni mwa wiki, Naibu Waziri huyo wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alimtaka Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ulanga Juma Kapilima kumpa taarifa ya maandishi kuhusiana na suala hilo kwa kuwa Waraka uliotolewa kuhusiana na suala hilo unaeleza wazi kilichohamishiwa wizarani ni Mamlaka ya Nidhamu na Ajira pekee.
‘’Hii ni serikali moja, ofisi ya Mkurugenzi ni Mamlaka ya upangaji, nataka maelezo ya msingi maana waraka unajieleza na ulienda kwa Makatibu Tawala wa Mikoa na Wilaya na hata mishahara ya watumishi wa sekta ya ardhi bado inalipwa na TAMISEMI’’ alisema Dkt Mabula,
Kwa mujibu wa Mkuu wa wilaya ya Ulanga, mbali na changamoto ya ukosefu wa fedha katika sekta ya ardhi, wilaya yake inakabiliwa pia na uchache wa watumishi hususan katika fani za Mipango Miji, Uthamini, Uchoraji Ramani na Watunza Kumbukumbu alioueleza kuwa unasababisha shughuli zilizopangwa kutofanyika kwa ufanisi.
Aidha. Naibu Waziri Mabula alionesha kutoridhishwa na kasi ya zoezi la urasimishaji na upimaji viwanja kwenye wilaya ya Ulanga na kueleza kuwa halmashauri hiyo inatakiwa kuongeza kasi katika mazoezi hayo mawili ili kuwa na mji uliopangika na kuepuka ujenzi holela.
Aliongeza kwa kusema, katika zoezi la urasimishaji linaloendelea nchini halmashauri ya Ulanga inatakiwa kukaa na wananchi pamoja na makapuni ya urasimishaji ili kukubaliana gharama za urasimishaji na kusisitiza kiwango cha shilingi 150,000 kilichowekwa na Wizara kinaweza kupungua ili kuwafanya wananchi wengi kushiriki,
‘’Kuna halmashauri zimekubaliana na makampuni ya urasimishaji ambapo gharama zimepungua hadi kufikia 60,000 hivyo ninyi hapa msing’ang’anie kiwango cha 150,000 maana kinaweza kupungua kulingana na ugumu wa kazi na idadi ya watu waliojitokeza kurasimishwa’’. Alisema Dkt Mabula
Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ametembelea wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro na kuitaka wilaya hiyo kuongeza kasi ya upimaji, upangaji na umilikishaji ardhi na kuzingatia kupanga mji wa kiserikali utakaojumuisha taasisi zote za umma.
Aidha, Dkt Mabula alikagua ujenzi wa jengo la halmashauri ya wilaya ya Malinyi pamoja na nyumba ya Mkuu wa wilaya unaofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambapo alionesha kufurahishwa na kasi ya ujenzi wa majengo hayo mawili yanayotarajiwa kukabidhiwa rasmi mwanzoni mwa mwaka ujao 2020.
No comments:
Post a Comment