Advertisements

Wednesday, February 19, 2020

Watoto wawili wafariki, 11 hoi kwa kula chapati zenye sumu

Kampala, Uganda. Watoto wawili kati ya 13 wa familia moja nchini Uganda wamefariki dunia baada ya kula chapati zinazosadikiwa kuwa na sumu.

Watoto hao wanadaiwa kula chapati hizo baada ya kuzipika wenyewe kwa kutumia dawa ya kuua wadudu wa mazao wakidhani ni mafuta.

Polisi nchini Uganda ilisema kuwa watoto wengine 11 wamelazwa hospitalini na hali zao ni mbaya.

Kwa mujibu wa Gazeti la Daily Monitor la Uganda, watoto wote wanatoka katika familia moja iliyopo eneo la Budumba, Magharibi mwa nchi hiyo ambako wanadaiwa kuandaa chakula hicho wakati wakati wazazi hawakuwapo nyumbani.

Inadaiwa kuwa watoto hao wenye umri kati ya miaka mitano na sita walijipikia wenyewe vitafunwa hivyo ambavyo vinafahamika kwa jina la kabalagala.

“Inasemekna walitumia dawa ya kuua wadudu inayonyunyizwa katika matikiti maji na mboga za majani wakidhani ni mafuta ya kupikia.

“Muda mfupi baada ya kula vitafunwa hivyo walianza kutapika na kupelekwa katika Hospitali ya Busolwe ambako wawili kati yao walifariki dunia,” liliandika gazeti hilo.

Mkuu wa polisi wa eneo hilo, kamanda Ceasar Tusingwire alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

“Walionusurika wanaendelea na matibabu lakini bado hawajapa nguvu,” alisema kamanda Tusingwire.

Kamada Tusingwire alisema miili ya waliokufa inafanyiwa uchunguzi na baada ya kukamilika watakabidhiwa familia zao kwa taratibu za mazishi.

Hata hivyo, kamanda Tusingwire alisema jeshi la polisi limeshaanzisha uchunguzi rasmi wa tukio hilo na mara baada ya kukamilia utatolewa.

Mmoja wa wahudumu wa afya waliozungumza na gazeti hilo ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema “tunajitahidi kuhakikisha watoto hao wanarejea katika hali yao ya kawaida.

Mhudumu huyo alisema wengi wa watoto hao walifikishwa hospitalini hapo wakiwa katika hali mbaya kutokana na kula kiwango kikubwa cha sumu.

No comments: