Advertisements

Thursday, February 20, 2020

Yanga hii inapotea dakika hizi

By Charles Abel, Yohana Challe

Dar es Salaam. Tatizo la wachezaji wa Yanga kukosa pumzi na stamina ya kutosha kuhimili dakika 90 za mchezo huenda likaigharimu katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Wakati benchi la ufundi likihaha kutibu tatizo sugu la ubutu wa safu ya ushambuliaji sasa lina kibarua kipya cha kuongeza hali ya ufiti kwa wachezaji wake vinginevyo hali itakuwa ngumu kwa upande wao

Licha ya kuwa inaanza vizuri kipindi cha kwanza na kumiliki mpira huku ikitengeneza idadi kubwa ya nafasi za mabao, mambo yamekuwa magumu kwa Yanga dakika 45 za mwisho.

Udhaifu huo umezipa mwanya timu pinzani kuishambulia Yanga kipindi cha pili na hata kufunga mabao ambayo wakati mwingine huinyima Yanga pointi.

Kukosa pumzi na stamina huiweka katika wakati mgumu safu ya ulinzi ya Yanga ambayo hulazimika kufanya kazi ya ziada kuondoa hatari ambazo huelekezwa langoni mwao.

Tatizo hilo lilianza dhidi ya Kagera Sugar Uwanja wa Uhuru Januari, 15 ambapo licha ya kucheza vizuri kipindi cha kwanza, mambo yalikuwa magumu katika dakika 45 za pili ambazo walijikuta wakiruhusu mabao mawili na kupoteza mchezo huo kwa mabao 3-0 baada ya kutanguliwa kwa bao moja mwanzoni.

Kasoro hiyo ilijirudia katika mchezo dhidi ya Singida United lakini udhaifu wa wapinzani wao kutumia nafasi uliifanya Yanga kulinda ushindi wake wa mabao 3-1.

Baada ya mchezo na Singida, Yanga ililazimika kubaki nyuma kujilinda muda mrefu kipindi cha pili katika mchezo uliofuata dhidi ya Mtibwa Sugar ambao ilishinda bao 1-0. Hali hiyo ilijirudia dhidi ya Lipuli iliyoshinda mabao 2-1.

Wakati wengi wakiamini Yanga ingepata ushindi mnono baada ya kuongoza kwa mabao mawili kipindi cha kwanza, mambo yalibadilika na kuzidiwa kwa kiasi kikubwa na Lipuli ambayo ilipata bao la kufutia machozi katika muda huo.

Hali hiyo iliendelea kujitokeza dhidi ya Ruvu Shooting iliyopata ushindi wa bao 1-0, pia katika sare ya bao 1-1 na Mbeya City na baadaye Prisons.

Licha ya kocha Mbelgiji Luc Eymael kusema atafanyia kazi tatizo hilo, linaonekana kuendelea kuota mizizi na ushahidi ni timu hiyo ilivyocheza dhidi ya Polisi Tanzania, juzi.

Pamoja na kucheza vyema kipindi cha kwanza ambacho ilipata bao la kuongoza, hali ilikuwa tete kipindi cha pili ambacho ilijikuta ikielemewa na wapinzani wao ambao walisawazisha bao hilo na kufanya mechi imalizike kwa sare.

Ni kama ilikuwa bahati tu kwa Yanga dhidi ya Polisi Tanzania juzi kwani, wapinzani wao kabla ya kufunga bao hilo la kusawazisha, walipachika jingine ambalo lilikataliwa.

Polisi ilikuwa mwiba kwa Yanga kipindi cha pili, ikimiliki mpira, kutengeneza nafasi na kulishambulia lango la Yanga kama nyuki hadi filimbi ya kumaliza mchezo ilivyopulizwa.

Ikiwa itashindwa kufanyia kazi changamoto hiyo, Yanga inaweza kujikuta katika wakati mgumu kutokana na ufinyu wa ratiba ambao kila timu itakabiliana nao.

Timu za Ligi Kuu zitalazimika kucheza zaidi ya mechi 10 kuanzia sasa hadi Machi 15 wakati ligi hiyo itakapokuwa mapumzikoni kupisha mechi za timu ya taifa za mashindano mbalimbali.

Hata hivyo Eymael amegoma kuizungumzia kasoro hiyo kwa undani na kudai uwanja uliwagharimu dhidi ya Polisi na ameahidi kuifanyia kazi kasoro hiyo kabla ya mechi zijazo.

“Kwa sasa siwezi kuzungumzia wachezaji wangu kuhusu kiwango chao kuwa wanapunguza kasi hasa kipindi cha pili, ninachoweza kusema wote walikuwa fiti kwenye mchezo huo isipokuwa Tariq ndio hayupo sawa.

“Nadhani hali ya uwanja tuliotumia uliuona ulivyokuwa na makosa tuliyofanya wapinzani wetu waliyatumia vizuri, tutajitahidi kupata matokeo mazuri katika michezo inayofuata,” alisema Eymael.

Kiungo na nahodha wa Yanga, Papy Tshishimbi alisema watajitahidi kumaliza kasoro hiyo.

“Huu ni mpira kuna wakati mchezaji anaweza kufanya vizuri na wakati mwingine asifanye vizuri hivyo sisi wachezaji tunawaahidi mashabiki wetu tutajitahidi mechi zijazo tuweze kufanya vizuri wasikate tamaa,” alisema mchezaji huyo.

No comments: