Advertisements

Sunday, May 31, 2020

Red Cross waitikia wito wa RC Rukwa kwa kutoa msaada kwa waathirika wa Mafuriko ya Ziwa Tanganyika

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Winnie Kijazi akipokea aagodoro na mablanketi kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Rukwa kutoka kwa Mratibu wa Chama cha Msalaba Mwekundu Mkoani Rukwa Michael Mshingo (kulia)
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Winnie Kijazi akikabidhi mablanketi 100 na Magodoro 100 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Kalambo mh. Julieth Binyura (kushoto)
Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mh. Julieth Binyura (mbele katikati) pamoja na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Winnie Kijazi (wa pili toka kulia mbele) na Mratibu wa Chama cha Msalaba Mwekundu mkoa wa Rukwa Michale Mshingo (wa pili toka kushoto mbele) katika picha ya pamoja na wataalamu wengine. 
Baadhi ya Wanachama wa Chama cha msalaba Mwekundu wakipakia magodoro na mablanketi katika lori kwaajili ya kupelekewa waathirika wa mafuriko ya maji ya ziwa Tanganyika Wilayani Kalambo.

Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania (Red Cross) kimeitikia wito uliotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo kwa kutoa Magodoro 100 na mablanketi 100 ili kuzisaidia kaya zaidi ya 300 zilizokosa mahala pa kulala baada ya nyumba zao kumezwa na maji ya ziwa Tanganyika baada ya ziwa hilo kutapika na kuathiri vijiji vya Kasanga, Kilewani na Kipwa vilivyopo Kata ya Kasanga, Wilayani Kalambo.

Hivi karibuni Mh. Wangabo aliziomba taasisi, mashirika na wadau mbalimbali nchini kuona uwezekano wa kuzisadia kaya hizo ili wananchi hao waweze kujihifadhi na mvua, baribdi pamoja na kuwapa misaada ya kiafya kutokana na vyoo vya maeneo hayo kuchukuliwa na maji na hivyo kuwepo uwezekano mkubwa wa magonjwa ya mlipuko kutokana na vinyesi kusambaa na hivyo aliwataka wananchi hao kuchukua tahadhari za kiafya.

Wakati akipokea msaada huo kutoka Chama cha Msalaba Mwekundu na kukabidhi kwa mkuu wa Wilaya ya kalambo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa Winnie Kijazi alifikisha maelekezo ya Mkuu wa Mkoa kuwa wananchi waliopo katika maeneo hayo wanatakiwa kuhama na hivyo kumtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kufanya haraka kuwahamisha wananchi hao katika maeneo ambayo halmashauri imeyatenga.

“Wananchi Waelewe kwamba serikali inapotoa misaada, basi ni kwaajili ya kuwasaidia wakati wa dharura, lakini kuendelea kujiepusha kuishi kwenye maji kwasababu kwakweli ni hasara, serikali ina mambo mengi ya kufanya, mmeona barabara zimejengwa vizuri, mmeona hospitali zimejengwa vizuri, ni hela nyingi serikali inatumia kwahiyo wasikae wakategemea kwamba serikali italeta na hii mwenyekiti (wa halmashauri) utusaidie kwenye mikutano yako uwaelimishe wananchi watoke wkenye hayo ameneo,” Alisema.

Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mh. Julieth Binyura wakati akipokea msaada huo alikishukuru Chama cha Msalaba Mwekundu kwa kuwapa msaada huo na kuwataka wananchi wa maeneo yaliyoathirika kutoka kwenye maeneo hayo na kuanza kujenga katika maeneo yenye miinuko huku akiwataka kujikinga na magonjwa ya kipindupindu pamoja na Corona.

“Nawaasa tu wananchi kwamba watakapokuwa wamepata blanketi na magodoro, basi tunaomba kwasasa kwa vile mvua zimepungua waanze kujenga maeneo ya mwinuko na tayari tumeshawaelekeza, Afisa Ardhi ameshaelekeza, na vipimo wameshapewa wao ni kwenda kujenga kwenye mwinuko na kuondoka kwenye ziwa ambapo tayari limeshajaa maji na mpaka sasa maji yanaendelea kujaa bado halijapungua kwasababu kuna sehemu ambazo mvua bado zinanyesha,” Alisisitiza.

Aidha, Mratibu wa Chama cha Msalaba Mwekundu Mkoani Rukwa Michael Mshingo aliwaomba wananchi wa Mkoa wa Rukwa kujiunga na chama hicho ili kuweza kuongeza nguvu kazi ya chama hicho katika kutoa huduma kwa jamii ndani ya mkoa na pia kuwaomba wananchi hao kuendelea kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa Corona kwa kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni pamoja na kuvaa barakoa.

Mbali na Chama cha Msalaba Mwekundu kutoa Magodoro na Mablanketi yenye thamani ya Shilingi milioni 8 pia Mbunge wa jimbo la Kalambo ambaye pia ni Naibu Waziri OR-TAMISEMI Mh. Josephat Kandege nae ametoa turubai 50 pamoja na tani moja ya unga huku Mkuu wa mkoa akitoa turubai 16 na sukari kilo 100.

No comments: