ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 3, 2020

Simba, Yanga kuwasha mitambo kwa KMC



WINFRIDA MTOI NA ZAINAB IDDI – DAR ES SALAAM, MTANZANIA

VIKOSI vya Simba na Yanga vinatarajia kucheza mechi za kujipima nguvu dhidi ya KMC, ikiwa ni matayarisho ya kurejea katika mikiki mikiki ya Ligi Kuu Tanzania Bara, ambayo imepangwa kuendelea Juni 13, mwaka huu.

Timu hizo zilianza mazoezi wiki iliyopita, baada ya Serikali kuruhusu shughuli za michezo kuendelea, baada ya kuridhishwa na kupungua kwa kasi ya maambukizi ya ugongwa wa corona.

Ligi Kuu ilikuwa ilisimama tangu Machi mwaka huu, baada ya serikali kupiga marufuku shughuli zinazosababisha mikusanyiko ikiwemo michezo, ikiwa ni tahadhari ya kuepuka kusambaa kwa virusi vya corona.

Hatua hiyo ilililazimisha Shirikisho la Soka Tanzania(TFF) kusimamisha Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Daraja la Pili na mashindano mengine yaliyo chini yake.

Baada ya timu hizo kuanza mazoezi ya pamoja, makocha wa vikosi vyote wameona ni muhimu kucheza mechi za kirafiki kupima utimamu wa mwili wa wachezaji wao.

Akizungumza na MTANZANIA juzi baada ya mazoezi ya timu ya Yanga, yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Chuo cha Sheria, Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mashindano wa klabu hiyo, Thabit Kandoro, alisema benchi la ufundi la timu yao limeomba michezo miwili ya kirafiki, kabla ya kuingia kushindana.

Alisema kwa kutambua umuhimu wa michezo hiyo, uongozi umekubali ombi hilo na kutafuta timu zenye uwezo wa kuipima Yanga na wanatarajia kuanza na KMC.

Kandoro alisema pamoja na ombi la makocha, pia wameona kuna umuhimu wa mashabiki kukiona kikosi chao kwa sababu ni muda mrefu, hivyo wameamua mchezo huo upigwe Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

“Mechi hii tunatarajia itachezwa Uwanja wa Uhuru kuanzia saa kumi jioni, mashabiki wataruhusiwa kuingia kwa kuzingatia muongozo wa Wizara ya Afya na Wizara ya Michezo,” alisema.

Alifafanua kuwa, tangu ligi hiyo isimame, Kamati ya Mashindano ya klabu yao ilikuwa kazini kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa ili kutimiza malengo waliyojiwekea.

“Hata kabla ya ratiba kutoka, tulikuwa tumeshajipanga kwa tahadhari kuwa muda wowote ligi itakaporejea kusiwe na changamoto nyingi, tutahakikisha timu inacheza mechi zake zote katika hali nzuri,” alisema Kandoro.

Naye Kocha Msaidizi wa Yanga, Charles Mkwasa, alisema program zao za mazoezi zinakwenda vizuri.

“Kuna vitu vichache ambavyo wachezaji hawajazingatia wakiwa nyumbani, ndiyo ninavyofanyia kazi hasa kama vile stamina, si unajua kila mmoja alikuwa anafanya kivyake lazima kuwaunganisha,” alisema Mkwasa.

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa KMC, Hererimana Haruna, alisema mchezo huo anatarajia utakuwa mzuri na atajua ni sehemu gani anatakiwa kufanyia marekebisho.

“Tuna wiki ya pili tangu tumeanza mazoezi, mechi hii itatufanya tufahamu ni wapi tumefika na pale palipobaki ili tuingie uwanjani kutafuta pointi tatu tukiwa fiti kabisa,” alisema Haruna.

Alieleza kuwa kabla ya kukutana na Yanga, leo wanatarajia kucheza dhidi ya timu ya Daraja la Kwanza ya Trans Camp, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Uhuru.

“Tunacheza mechi tatu za kirafiki, tunaanza na Transit Camp, kisha Yanga na Simba, nina imani mechi zote hizi zitatuwela sehemu nzuri,”alisema Haruna.

No comments: