Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akimkabidhi Mwenyekiti wa Chama cha Umoja wa Waalimu cha Akiba na Mikopo (CHAUWAMI) SACCOS Justin Mwanasimeta Shilingi 56,700,000/= kwaajili ya kuwarudishia waalimu wastaafu waliojiunga na chama hicho.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameshangazwa na kitendo cha waalimu wastaafu wa vyama vya akiba na mikopo (SACCOS) mkoani humo kudhulumiwa shilingi 96,456,250/= badala ya kuwa mfano wa kuigwa kutokana na kuwa mstari wa mbele katika kudai haki zao pamoja na kuongezewa mishahara kutoka serikalini.
Amesema kuwa inashangaza kuona waalimu hawa wenyewe kwa wenyewe kwenye vyama vyao wanadhalilishana na kunyayasana badala ya SACCOS zao kuwa za kuigwa kutokana na kuzisimamia wenyewe na sio kudhulumiana huku wengine wakiwa na hali mbaya kiuchumi na hivyo kuwataka viongozi wa vyama hivyo kuwa waadilifu na kufanya kazi kwa misingi ya sheria.
“Hizi SACCOS za waalimu zinapaswa kuwa za mfano wa kuigwa, kwasababu zinasimamiwa na wao wenyewe, lakini hapa tunaona kabisa kwamba waalimu tena wastaafu ‘wanapigwa’, wengine wana hali mbaya, wamedhalilishwa na kunyanyaswa kwa muda mrefu, viongozi wa vyama hivi vya SACCOS lazima muwe waadilifu,” Alisisitiza.
Aliongeza kuwa mkoa upo katika harakati za kuimarisha vyama vya ushirikia na lengo hilo halitafikiwa endapo kutakuwepo na viongozi wabovu, wasiofaa, ambao hawajali maslahi ya wanachama wao, amabao ndio wametufikisha hapa mpaka tukawaagiza TAKUKURU wawashughulikie hao viongozi.
Wakati akichanganua mgawanyo wa fedha hizo katika taarifa ya ubadhilifu huo Mkuu wa Taasisi ya Kuzui na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Rukwa Hamza Mwenda alisema kuwa shilingi 56,700,000/= zitarejeshwa kwa Waalimu Wastaafu 39 wa SACCOS ya CHAUWAMI ambayo inahusisha waalimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na Kalambo.
Pia alisema kuwa Shilingi 39,756,250/= zitakabidhiwa kwa viongozi wa Nkasi Teachers SACCOS. Shilingi 1,345,000/= zitarudishwa kwa kwa SACCOS ya MAKUPA iliyopo wilayani Nkasi ikiwa ni fedha ambazo zilikopeshwa kwa wananchama lakini wakagoma kuzirejesha kwenye SACCOS kwa mujibu wa masharti ya muda wa marejesho ya mikopo yao.
“Uongozi wa awali wa SACCOS ya Nkasi Teachers uliandaa nyaraka na kuwakopesha watu wasio wanachama kinyume cha sheria ya Vyama vya Ushirika Namba 6 ya Mwaka 2013. Uchunguzi huu ulitokana na taarifa ya COASCO ambayo waziri wa Kilimo alimkabidhi Mkurugenzi Mkuu TAKUKURU kwaajili ya kuifanyia kazi, fedha hizi zimerejeshwa na leo tutaomba uwakabidhi viongozi wa Nkasi Teachers SACCOS na zitaingizwa katika akaunti ya chama leo,” Alieleza.
Akiongea kwa niaba ya waalimu wenzie Mwalimu Mstaafu Benard Mpepo alitoa shukrani kwa serikali kwa kuwa na chombo thabiti cha kutetea haki za wanyonge na kubainisha kuwa haki hiyo ilikuwa ngumu kuipata lakini kutokana na umakini wa chombo hicho hatimae wamepata haki yao.
Makabidhiano hayo yametokea jana (11.6.2020) wakati wa hafla fupi ya kukabidhi fedha hizo kwa waathiriwa wa vitendo vya rushwa mbele ya Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo na kuhudhuriwa na waalimu wastaafu na watumishi wengine wa serikali wa Idara za Ulinzi na Usalama.
No comments:
Post a Comment