ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, October 18, 2020

Hoja Tano za Muungano Zapatiwa Ufumbuzi

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) leo Jumamosi Oktoba 17, 2020 Ikulu Dar es Salaam zimesaini hati za makubaliano kuondoa hoja za muungano zilizopatiwa ufumbuzi.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali hizo mbili wakiongozwa na makamu wa rais, Samia Suluhu Hassan na waziri mkuu, Kassim Majaliwa, waziri wa nchi, ofisi ya makamu wa rais (muungano na mazingira), Mussa Azzan Zungu ameyataja mambo hayo kuwa ni ushirikishwaji wa SMZ katika masuala ya kimataifa na kikanda, ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mengine ni gharama ya kushusha mizigo katika bandari ya Dar es Salaam kwa mizigo inayotoka Zanzibar, utafutaji na uchimbaji wa mafuta ya gesi asilia na utaratibu wa vikao vya kamati ya pamoja ya kushughulikia masuala ya muungano.

Zungu amesema hatua hiyo inachangiwa na kikao cha kamati ya pamoja kwa ajili ya kushughulikia masuala ya muungano kuridhia hoja hizo tano za muungano zilizopatiwa ufumbuzi hivyo ziondolewe katika orodha ya hoja za muungano.
Akizungumza katika hafla hiyo, Majaliwa amesema katika kipindi cha miaka mitano Serikali imefanikiwa kuonyesha dhamira kwa vitendo katika kuimarisha muungano.

Amesema mafanikio hayo yamechochewa na utendaji kazi wa Samia anayesimamia wizara inayoshughulika na masuala ya muungano na mazingira.

“Kufuta hati hizi ni kielelezo tosha kwa serikali ya SMZ na Jamhuri ya muungano namna zilizojikita katika kutatua changamoto mbalimbali za muungano kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.”

“Mfano ni kuondolewa kwa kodi ya ongezeko la thamani na kufuta malimbikizo ya deni lililokuwa limefikia Sh22.9bilioni kwa shirika la Zeco kutokana na umeme uliouzwa na Tanesco. Pili, Rais Magufuli alifuta sherehe za muungano wakati wa Covid-19 na kuelekeza Sh500milioni za sherehe hizo ipatiwe Zanzibar,” amesema Majaliwa.

Akihitimisha hotuba yake Majaliwa alinukuu sehemu ya ujumbe aliotoa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere Machi 6, 1997 Accra Ghana kwamba, “Umoja hautatupatia utajiri lakini utatufanya Waafrika tusipuuzwe na kudharauliwa .”

Amesema muungano huo ndio chimbuko la umoja na mshikamano wa kitaifa uliopo,” hivyo basi tukiwa tunaelekea kwenye uchaguzi Oktoba 28 mwaka huu, Nitoe rai wananchi kujitokeza kumpigia kura mgombea urais wa Zanzibar Dk Hussen Mwinyi na Dk John Magufuli.”GPL

No comments: