ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, October 31, 2020

WAGOMBEA TISA WA URAIS WAMUUNGA MKONO DKT.MAGUFULI KWA USHINDI WAKE

Na.Alex Sonna,Dodoma

Asiyekubali kushindwa si mshindani msemo huu umeungwa Mkono na wagombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka Vyama 9 kati ya 15 wametoa pongezi na kusema kuwa wapo tayari kushirikiana na Rais Mteule Dkt.John Magufuli kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) aliyeibuka kidedea katika Kiti cha Urais katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika siku ya Jumatano October 28,2020 na sasa wameungana na Msemo wa Dkt.Magufuli kuwa Maendeleo hayana Chama ambao alikuwa akiutumia kwenye Mikutano ya Kampenzi zake.

Aidha wamesema kuwa ushindi mnono alioupata Dkt.Magufuli unatokana na juhudi zake katika kuiongoza nchi kwa uzalendo wake,uadilifu na uchapakazi mkubwa aliounyesha katika kuleta maendeleo kwa wananchi.

Wagombea hao waliomuunga Mkono Rais Mteule Dkt.Magufuli ni vyama vya Siasa vya NCCR-Mageuzi,SAU,NRA,ADC,AAFP,UMD,DP,UPDP na Demokrasia Makini.

Kauli hiyo wameitoa leo jijini Dodoma walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari wagombea hao wamesema Dkt.Magufuli ameibuka kidedea kutokana na ushindi wa kishindo wa kura 12,516,252 hivyo hakuna sababu ya mtu yoyote ya kutomuunga mkono katika kuleta maendeleo kwa wananchi wote.

Naye Mgombea wa Urais wa chama cha UPDP Twalib Kadege amesema kuwa Dkt.Magufuli wakati wa kampeni zake alitumia mikutano yake kwa kuwaambia na kuwaeleza mambo makubwa aliyoyafanya na anayotarajia kuyafanya huku akiwaomba wachague CCM bila ya matusi wala jazba na wananchi wote makini walimuelewa na wakampa kura za kishindo

“Tumezunguka wote katika kipindi cha Kampeni huku tukinadi sera zetu ila mwenzetu amevuna alichopanda,kutoka na kazi nzuri aliyoifanya katika kipindi chake cha miaka mitano na mtu yoyote anayefanya vizuri kwa wananchi wake kwa kuwaletea maendeleo yaliyobora lazima wamuunge mkono kwa kumpa kura hivyo mimi nimeridhika kuwa ni haki yake kupewa kura kutokana na jinsi alivyoongoza hakuwa na matusi ameeleza alichofanya na atakachofanya baada ya kuchaguliwa”amesema Bw.Kadege
Kwa upande wake mgombea wa Urais wa Chama cha NCCR Mageuzi Jeremiah Maganja ametoa pongezi kwa Tume ya taifa ya uchaguzi (NEC) kutokana na kuendesha uchaguzi uliokuwa wazi na wenye haki kwa kufuata sera nzuri toka kwenye vyama vyao.

Hivyo kwa pamoja bila kujali vyama vyao kwa kauli moja wameamua kumuunga mkono Dkt.Magufuli aliyechaguliwa na kutangazwa na Tume ya uchaguzi (NEC).

Maganja ametoa wito kwa wananchi kuwa kipindi hiki wanatakiwa kuwa makini na watulivu na wasikubali kudanganywa wala kugawanywa na baadhi ya wanasiasa kufanya mambo kinyume na taratibu za kisheria za nchi.

Ikumbukwe kuwa jana Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilimtangaza Dkt.John Pombe Magufuli kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushindi mnono wa kura 12,516,252 sawa na asilimia 84.4 akifuatiwa na Tundu Lisu wa Chama cha Demokrasia (CHADEMA) mwenye kura 1,933,271 sawa na asilimia 13.03 huku Bernard Membe kutoka Chama cha ACT-Wazalendo akiwa amepata kura 81,129 sawa na asilimia 0.54

No comments: